NA MICHAEL SARUNGI

Kutopitia mafunzo ya soka kutoka vyuo vya
kufundishia soka na Watanzania kukosa
uvumilivu kunaweza kuwa sababu ya
kumkwamisha Kocha wa sasa wa Taifa
Stars, Mnigeria Emmanuel Amunike.
Wakizungumza na Gazeti la JAMHURI kwa
nyakati tofauti baada ya kocha huyo
kutangaza kikosi cha Taifa Stars
kitakachoingia kambini kwa ajili ya mechi ya
kuwania kufuzu kucheza fainali za AFCON
2019 dhidi ya Uganda, wadau wa soka
nchini wamesema kocha huyo anahitaji
ushirikiano, vinginevyo atakuwa sawa na
waliopita.
Wamesema mchezaji anaweza kuwa mahiri
wakati wake, hiyo haina maana anaweza
kuwa na mafanikio anapoamua kuwa kocha
katika ngazi ya klabu au timu ya taifa,
kinachotakiwa ni ushirikiano wa karibu

kutoka kwa wadau wote.
Kocha wa Mbao ya jijini Mwanza, Amri Said,
amesema Amunike ana jina kubwa katika
medani za soka barani Afrika na duniani,
hasa baada ya kuacha historia nzuri ya
uchezaji katika ngazi ya klabu hadi timu ya
taifa ya Nigeria na kuwataka Watanzania
kuwa wavumilivu na kumpa muda wa
kutosha.
Amesema kwa bahati mbaya wachezaji
wengi hapa nchini wanakabiliwa na
changamoto nyingi hadi kufikia mafanikio,
kutokana na wengi kufanya juhudi binafsi
tofauti na nchi kama Nigeria, ambako kuna
shule nyingi za soka.
Nchi za Afrika Magharibi na Kusini zina
vyuo vingi vya kufundisha vijana wenye
vipaji misingi na kanuni za mchezo wa soka
kuanzia umri mdogo, kitendo kinachotoa
wigo mpana kwa kocha kuchagua vijana
anaotaka kufanya nao kazi kuanzia timu ya
vijana hadi wakubwa.
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky
Maxime, amesema Amunike anahitaji
ushirikiano wa karibu kutoka kwa wachezaji
na wadau wenye nia ya dhati na kuachana
na tamaa ya kutaka kupata maendeleo ya
zimamoto bila mipango.

Amesema pamoja na changamoto nyingi,
wachezaji nao wanapaswa kujitambua na
kukubali kujifunza kutoka kwa wachezaji
wenzao wenye mafanikio makubwa barani
Afrika na duniani kwa ujumla, kwa
kuachana na uvivu na mambo mengine
yanayoweza kukwamisha juhudi za
mwalimu.
Maxime amemtaka kocha kujitengea muda
wa kuwajumuisha baadhi ya vijana wenye
vipaji kutoka timu za vijana wenye uwezo
wa kuja kuitumikia timu ya taifa kwa miaka
ijayo ili kuja kuchukua nafasi za kaka zao
ambao miaka michache ijayo watastaafu.
Ofisa Habari wa Ndanda FC, Idrissa
Bandari, amesema Amunike ni jina kubwa
katika medani ya soka, lakini kupata
mafanikio akiwa kocha ni jambo tofauti,
kikubwa ni kuhakikisha anapata ushirikiano
kutoka kwa wadau wote wa michezo.
Wapo wachezaji waliokuwa mahiri
walipokuwa wakicheza, walipogeukia
ukocha walikutana na vikwazo vingi vilivyo
sababisha kuacha, mfano ni Diego
Maradona, aliyepewa jukumu la kufundisha
timu yake taifa lake lakini hakupata
mafanikio yoyote hadi anajiuzulu nafasi
hiyo.

Bandari amesema kikubwa ni wadau wote
wa michezo kumpa muda na ushirikiano
utakaomwezesha kufanikisha mipango yake
ya muda mrefu na mfupi pasipo kupata
mashinikizo ya kuingiliwa katika kazi yake,
bila kufanya hivyo anaweza akajikuta
anamaliza muda wake na kuondoka bila
cha maana.
Tayari Kocha Mkuu wa Taifa Stars,
Amunike, ametangaza majina ya wachezaji
watakaoingia kambini Jumatatu kujiandaa
na mchezo dhidi ya Uganda, mchezo
unaotarajiwa kufanyika Septemba 8, 2018
kuwania kufuzu kucheza fainali za AFCON
2019.

Mwisho

By Jamhuri