Vidonda vya tumbo na hatari zake (Hitimisho)

Katika sehemu ya 17 ya makala haya, Dk. Khamis Zephania, pamoja na mambo mengine, alielezea dawa za viua vijasumu, vizima asidi na upasuaji. Sasa endelea kumfuatilia zaidi katika sehemu hii ya mwisho…

Karibu watu 300,000 kote duniani hufanyiwa upasuaji kutokana na madhara yaletwayo na vidonda vya tumbo ambayo huzalisha magonjwa mengine. Vyakula: Kipengele kikubwa katika matibabu ni kula mlo sahihi na tabia nzuri katika namna ya kula vyakula.

Ni muhimu sana kula mlo wenye nyuzinyuzi. Ni muhimu pia kula mlo wenye mafuta kidogo sana.

Upungufu wa vitamini K pia umehusu kupatikana kwa vidonda vya tumbo. Vitamini K huzuia kutoka damu huweka mazingira mazuri ya kupona.

Miili yetu hutengeneza vitamini K ya kutosha, lakini watu ambao hawana vitamini hii husababisha kupata vidonda. Vitamini K hupatikana katika nyanya, jibini (chizi), viini vya yai, ini na katika mboga nyingi za majani zenye rangi ya kijani.

Tafiti zinaonesha kwamba vitamin C, vitamin E na vitamin B6 viko chini sana kwa watu wenye vidonda vya tumbo.

Vitamini A ni muhimu sana kwa uponyaji wa ute telezi. Zinki kwa upande wake huongeza kasi ya uponyaji wa vidonda vya tumbo.

Pia ule mlo kidogo kidogo. Unapokula mlo kidogo kidogo unaepusha kuzalisha asidi nyingi ya mmeng’enyo wa chakula, lakini kula mara kwa mara kuzuia asidi hii kushambulia kunyanzi za tumbo.

Juisi ya kabichi ina msaada katika kutibu vidonda vya tumbo. Andaa juisi ya kabichi (kabeji) na tumia robo kikombe kila siku. Kunywa mara tu baada ya kuiandaa.

 

Epuka maziwa. Ingawa maziwa hutuliza tumbo na huzimua asidi ya tumbo, lakini pia husisimua uzalishaji wa asidi zaidi, ambayo baadaye itachoma eneo la kidonda.

 

Epuka vitu vinavyoshawishi uzalishi mwingi wa asidi. Epuka kahawa, pombe, juisi za sitriki    (citrus juices), vyakula vya moto na vyakula vya kusisimua. Vitu hivi huchoma tumbo na hushawishi uzalishaji wa asidi ya tumbo.

 

Watu wenye vidonda vya tumbo ni vizuri zaidi kwao kuepuka vyakula vyote vya kukaangwa; pia bizari, pilipili, haradali; matunda mabichi; maharage; figili; tango, vyakula vya moto sana au vya baridi sana; vyakula vya ‘Tomato sauce’ (vina asidi nyingi iliomo ndani yake); vinywaji vyenye gesi, vyakula vya mafuta, chai nzito (strong tea) au kahawa. Vinywaji hivi vinaweza kuongeza asidi ambayo tumbo lako  linaizalisha.

Siyo rahisi kuepuka vyakula vyote hivyo. Unaweza kuangalia ni chakula gani zaidi kinachokudhuru, na unaweza kukiepuka.

Kwa ujumla, vyakula vinavyotakiwa kuliwa na mgonjwa wa vidonda vya tumbo ni vile ambavyo havileti kiungulia, havileti ugumu wa mmeng’enyo wa chakula, havichomi kunyazi za tumbo.

 

Vidonda vya tumbo vina kawaida ya kurudi hata kama vimetibiwa kwa ukamilifu. Ni bora kujizuia kula vyakula ambavyo tumevieleza. Na uangalifu mkubwa katika matumizi ya dawa ‘NSAIDs’ na aspirin.

 

Dawa asilia: Matibabu asilia yana msaada mkubwa sana kwa magonjwa mengi. Kuna mamia kwa maelfu ya magonjwa ambayo hutibiwa kwa matibabu asilia.

 

Matumzi ya dawa asilia yamekuwepo tangu na tangu kabla ya historia kuandikwa. Kabla ya dawa za kemikali, matibabu haya yalikuwa yakitibu maradhi ya binadamu.


Hadi leo matibabu ya dawa asilia bado yanawavutia watu wengi sana; na zaidi kutokana na dawa za kemikali kuleta side effects nyingi.


Matibabu asilia ni salama zaidi na hayasababishi magonjwa mengine. Mengi ya matibabu haya yametumiwa kwa maelfu ya miaka iliyopita. Moja ya faida zake kubwa ni kwamba huweza kutibu maradhi mengi kwa wakati mmoja.


Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa sasa H. pylori anaweza kuuawa kwa matibabu asilia ya mimea tiba.


Licha ya kwamba matibabu ya vidonda vya tumbo ya kiasili ni mazuri sana, lakini unatakiwa kuwa mwangalifu sana kuchagua matibabu mazuri yatakayokuponesha kabisa.

Wapo watu ambao hudai wana dawa za vidonda vya tumbo, lakini dawa hizo huleta nafuu kidogo au hazileti nafuu kabisa.

2833 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!