Tupande miti kukuza uchumi wetu (3)

Sehemu ya pili ya makala hii, mwandishi alieleza juu ya kuletwa nchini mbegu za mikalatusi kutoka Australia (ambako kuna zaidi ya aina 600 ya miti hiyo) kwa ajili ya kufanyiwa majaribio. Endelea…

Mbegu za miti aina ya Mipine zililetwa kutoka Ulaya na Amerika ya Kusini, Kati na Caribbean. Mbegu za miti aina ya mitiki zilitoka maeneo ya Mashariki ya Mbali — Burma na Malaysia.

Mbegu za Micyprus zilitoka nchi za Ulaya kama vile nchi au kisiwa na Cyprus. Hivyo, baada ya mbegu mbalimbali za miti kutoka nchi mbalimbali kuingizwa nchini na kupokewa na Kituo cha Utafiti wa Miti Lushoto, zilikuwa zinasambazwa katika maeneo ambayo nimekwisha kuyataja ili kufanyiwa majaribio ya ukuaji wake.

Aina za miti mchanganyiko zilioteshwa kwa pamoja kwenye eneo moja kulingana na hali ya hewa ya mahali husika (kiwango cha mvua kwa mwaka, joto, ubaridi, aina ya udongo pia kwa kuzingatia hali halisi ya mahali mbegu zilikotoka).

Majaribio au utafiti wa aina hii unasadikiwa kuanza enzi za Wajerumani mwaka 1905 walipoingiza mbegu za mitiki na kuanza majaribio katika maeneo ya Longuza, Tanga na Mtibwa mkoani Morogoro.

Kazi ya utafiti wa misitu iliongezwa nguvu wakati wa Waingereza kuanzia miaka ya 1920.  Kufika miaka ya 1940 na 1950 ilioneka baadhi ya aina za miti zilikuwa zinaota na kukua vizuri (good species performance).

Mathalani miti aina ya mitiki ilionekana kustawi vizuri sehemu za mwambao zenye joto na miinuko midogo. Miti aina ya Mipine na Micyprus ilionesha kustawi vizuri hasa sehemu zenye ubaridi, mvua nyingi na udongo mzuri usiokuwa na mfinyazi mwingi.


Mbegu za mikalatusi zilioteshwa karibu sehemu nyingi nchini na kuweza kustawi bila ya matatizo maana iko mikaratusi aina zaidi ya 600. Kwa hali hiyo, kuweza kupata aina ya mikalatusi inayoota na kustawi vizuri katika maeneo ya mvua nyingi au maeneo kame au ya wastani halikuwa suala gumu. Kutokana na sababu hiyo mikalatusi imetapakaa karibu maeneo mengi nchini.

Hadi miaka ya 1950 Serikali ya wakoloni iliweka utaratibu wa kupanda aina hizo kwa kuanzisha mashamba ya miti. Hadi Tanganyika inajitawala mwaka 1961 mashamba 14 ya miti yalikuwa yameanzishwa katika maeneo yafuatayo: Buhindi (Sengerema), Kawetire (Mbeya), Kiwira (Rungwe), Meru (Arusha), West Kilimanjaro (Siha), North Kilimanjaro (Rombo), Shume-Magamba (Lushoto), Matogoro (Songea), Rondo (Lindi), Rubare (Bukoba), Rubya (Ukerewe) na Sao Hill (Mufindi).

Katika maeneo hayo ilipandwa mikalatusi ambayo ni aina ngumu na pia miti aina ya Mipine kama Pinus patula, P. elliotii, P. carribea na Micyprus mfano Cupressus lusitanica ambayo ni miti laini (softwood species).

Vilevile kulianzishwa mashamba mawili ya miti migumu (hardwood species) na katika mashamba hayo miti aina ya misaji (Tectona grandis) au kwa jina lililozoeleka ni “Mitiki” au miti majani mapana kama wanavyoifahamu wakazi wa Jiji la Tanga.

Mashamba ya miti migumu yapo Longuza (Muheza) na Mtibwa (Mvomero). Vilevile mitiki pamoja na mivule (Faudherbia excelsa) na mininga (Pterocarpus angolensis) michache ilioteshwa kwenye Shamba la Miti Rondo, Lindi.

Hadi Desemba 2012, Tanzania Bara ilikuwa na hekta takribani 90,000 za mashamba ya miti zikiwamo zaidi ya hekta 6,000 za mashamba ya miti migumu katika eneo la Longuza na eneo la Mtibwa.

Mashamba yote ya miti yanamilikiwa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii. Vilevile wapo baadhi ya watu binafsi na kampuni kama Njombe Wattle Company; Green Resources; Mufindi Paper Mill (MPM) na Tree Farm (katika mikoa ya Iringa na Njombe) pamoja na Kilombero Valley Teak Company (KVTC) mkoani Morogoro wameweza kuanzisha mashamba ya miti. Inakisiwa kuwa hadi Desemba 2012 takribani hekta 500,000 za mashamba ya miti nchi nzima zilikuwa zimeoteshwa na watu binafsi na kampuni hasa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Kagera.

Kwanini tupande miti kwa wingi?

Kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita kumekuwapo ongezeko kubwa la watu ikilinganishwa na idadi ya watu isiyozidi milioni 10 tuliyokuwa nayo wakati wa kupata Uhuru  mwaka 1961. Inakisiwa kuwa sasa Tanzania ina watu zaidi ya milioni 44.

Watu wakiwa wengi, matumizi ya mazao yatokanayo na rasilimali misitu kwa shughuli za kibinadamu za kila siku, nayo huongezeka.

Kwa miaka mitatu (Mei 2010 hadi Juni 2013) Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na msaada wa fedha kutoka Serikali ya Finland, iliweza kupima misitu ya asili na iliyopandwa na miti iliyopo nje ya misitu kwa nchi nzima.

Takwimu zilizopatikana zinaonesha kuwa eneo lenye misitu na mimea au uoto wa asili linakadiriwa kuwa hekta milioni 48 kwa Tanzania Bara. Eneo hilo linaonekana kuwa nusu ya lote la Tanzania Bara.

Kwa haraka haraka mwananchi wa kawaida anaweza kusema iwapo tunalo eneo kubwa lenye misitu na uoto wa asili kiasi hicho, kwa nini tuhangaikie kupanda au kuotesha miti zaidi?

Kusema kweli hata kama takwimu zimeonesha ukubwa huo wa eneo lenye misitu au uoto wa asili, asilimia kubwa ni maeneo ambayo hayana miti inayofaa kwa matumizi na faida ya binadamu; bali ni vichaka na uoto mwingine wa asili.

 

Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).

Napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha Watanzania walio vijijini na mijini kwamba misitu ya asili katika maeneo mbalimbali nchini imeharibiwa mno (highly degraded). Isitoshe, bado kasi ya uharibifu wa misitu ya asili ni kubwa kuliko unavyodhania maana matumizi ya mashine za moto (power or chain saws) yameongezeka sana.

Kinachosababisha misitu ya asili kuharibika sana ni kutokana na shughuli za kibinadamu. Kwa mfano, kufyekwa kwa shughuli za kilimo, ufugaji na kukata aina mbalimbali za miti kwa wingi kwa ajili ya mbao, nguzo, kuni na mkaa.

Kutokana na kasi ya kukata miti ya asili kuwa kubwa mno, hali ya mazingira nayo imeathiriwa sana. Kwa nchi kama Tanzania ambayo shughuli za uzalishaji huduma na mali kupitia viwanda, hazijawa nyingi sana kama ilivyo kwa nchi tajiri, kiwango cha uharibifu wa mazingira kupitia viwanda si cha kutisha. Isipokuwa uharibifu wa mazingira ni mkubwa kutokana na kufyeka misitu na kuichoma moto kila mwaka wakati wa kiangazi.

Usimamizi na udhibiti wa shughuli za binadamu katika misitu na mapori umekuwa mdogo sana kiasi cha kusababisha hali ya misitu kutoridhisha na kutoweka kwa kasi sana.

Hali ilivyo kwa upande wa mazingira si nzuri maana maeneo mengi ya misitu ya asili yameharibiwa mno kiasi cha kuhatarisha uhai wa viumbehai wengine kama wanyama, ndege na wadudu mbalimbali. Ili kukabiliana na hali hiyo ya ongezeko kubwa la matumizi ya rasilimali misitu, na athari zake kubwa kwa mazingira ni muhimu kwa Watanzania wengi wakapanda miti kwa wingi.

Itaendelea

 

Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).


3240 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!