Wadau mbalimbali wanaotoa huduma za aina tofauti katika Kituo cha Mbasi yaendayo mikoani na nje ya ncha cha Ubungo jijini Dar es Salaam wamehushutuma uongozi wa kituo hicho kwa kile walichokiita kuwa ni utaratibu mbovu wa uendeshaji.

Kituo hicho cha mabasi kwa sasa kiko katika kipindi cha mpito kutokana na kuwa chini ya matengenezo. Kinachowatia hofu watoa huduma kituoni hapo ni mfumo mzima wa kuendesha ambao wanasema kuwa hauna taratibu maalum. Kituo hicho kiko chini ya Mamlaka ya Jiji la Dar es Salaam.

Kuna waliothubutu kusema kuwa wanadhani kwamba kwa kipindi hiki ambapo kituo hicho kinafanyiwa ukarabati labda huduma za zingekuwa na gharama ya chini kidogo kutokana na kwamba hakuna miundo mbinu inayofanya kazi.


Kuna makundi tofauti katika kituo hicho ambapo kila kundi lina shutuma yake dhidi ya uongozi wa kituo hicho kwa jinsi ambavyo kimekuwa kikitoa huduma zake.


Kuna wadau ambao wanaona kuwa kituo hicho sasa kimegeuka kuwa kama mradi wa mtu binafsi au wa kundi la watu fulani kutokana na kubuni mbinu mpya kila siku za kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ukusanyaji wa mapato ambao unawaumiza wahusika na hasa wafanyabiashara ndani ya kituo hicho.


Mbali na utaratibu wa ukusanyaji wa mapato kitu kingine kinacholalamikiwa katika kituo hicho ni kuwa na ulinzi wa watu ambao hawatambuliki kisheria ambao wamekuwa wakibeba jina la askari wa ulinzi shirikishi.


Kadhalika utaratibu mpya wa utoaji wa vitambulisho maalum vya kuingilia ndani ya kituo hicho kwa wale ambao ni watoa huduma kwa abiria, yaani makarani na wafanyakazi wengine katiba mabasi ya abiria umeibua mjadala mkubwa kati ya uongozi wa stendi na wadau wengine.


Jambo jingine linalolalamikiwa ni faini ambazo wamekuwa wakitozwa watu ndani ya kituo hicho kwa kisingizio cha kubughudhi abiria.


Juu ya hayo yote kuna malalamiko ya kwamba uongozi wa kituo hicho umekuwa ukifanya mambo yake kwa kutanguliza ubabe kuliko njia ya makubaliano.

 

Kodi ya mabanda ya biashara

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, utaratibu unaotumika kwa watu kupata mabanda ya biashara ndani ya kituo hicho ni wa aina tofauti.


“Ukitaka banda humu ndani kuna mzee mmoja ambaye anahusika, kwanza unatakiwa ulipe hela ya kununua banda hilo au hata kama ni kontena, pili baada ya hapo unatakiwa kulipa ada ya kila mwezi,” Kilisema chanzo chetu cha habari.


Aidha kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari kituoni hapo kuna wafanyabiashara wanaolipa hadi kiasi cha sh 1,500,000 kwa mwezi. Halikikadhalika kuna wanaolipa Sh 30,000 hadi 40,000/ kwa siku.


“Hapa kila mtu ana bei yake, tatizo la humu ndani hakuna kiwango kamili kichoeleweka, alafu kwa mfano mimi hapa nalipa Sh 40,000 kila siku lakini huwa sipewi risiti kwasababu hata mimi hapa kuna mtu tena kanikodisha ambaye ndiye namlipa,” kilisema chanzo cha habari.


Ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hao wanapata faida, wamelazimika kufanya biashara hizo kwa muda wote, yaani kwa saa 24 kwa kubadilishana zamu. Katika hali hiyo kuna wengine wana umeme ambao inasemekana wanatumia jenereta, lakini pia kuna wale ambao hawana umeme ambao ufanya biashara zao hata nyakati za usiku.


“Bila kufanya hivyo hatuwezi kupata hela ya kulipa kodi, na humu ndani ukishindwa kulipa unafukuzwa mara moja analetwa mtu mwingine, Usishangae pia kuona bidhaa za humu ndani ziko juu kidogo kwa bei ni katika hali ya kuhakikisha tunapata hela ya kulipa kodi na hatimaye kubakiza faida kidogo” kilisema chanzo chetu cha habari.


Mvutano juu ya ulinzi shirikishi

Gazeti Jamhuri lilipata taarifa kuhusu suala la ulinzi shirikishi ambalo ilisemekana kwamba ni moja ya matatizo makubwa ambayo yamekuwa yakisumbua wadau na wafanyabiashara na wakati mwingine abiria. Kituo cha mabasi cha Ubungo kinalindwa na askari wa jiji, halikadhalika kuna askari wengine wa kikosi cha ulinzi shirikishi ambao wamekuwa wakitupiwa lawama nyingi kwamba wako kinyume na sheria kituoni hapo.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu ambao wamekuwa wakifanya biashara katika kituo hicho miaka nenda rudi, ni kwamba hao wanaofahamika kama ulinzi shirikishi, baadhi yao wanasemekana kuwa walikuwa wezi na vibaka katika siku za nyuma humo kituoni.


“Mimi nimekuwa hapa miaka mingi, hawa unaowaona wakijifanya ulinzi shirikishi zamani wengi wao walikuwa vibaka humu ndani, na kama unabisha waulize kama wanatambulika kisheria na wakwambie wametoka mitaa gani,” alisema kijana mmoja ambaye alisisitiza kuwa jina lake lisitajwe kwa ajili ya kulinda usalama wake.


Aidha Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Ubungo, Kirito Mnzava amesema kuwa ofisi yake haiwatambui askari wote wanaojiita ulinzi shirikishi walioko ndani ya kituo cha mabasi cha Ubungo.


“Kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa ulinzi shirikishi, inabidi taratibu zianzie katika ngazi ya mitaa na hapa kwetu tunakuwa na orodha ya wote ambao ni ulinzi shirikishi na mitaa wanayotokea, sasa wale wa ubungo, hatuwajui hata mitaa wanayotokea, na pia sisi hapa kama Ofisi ya Mtendaji Kata ya Ubungo hatuwatambui kisheria,” Amesema Mnzava.


Aidha kuna tetesi kwamba vijana hao ambao wa ulinzi shirikishi kituoni hapo waliwekwa na Chama cha Mawakala wa Mabasi kwa kushirikiana na Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), hali ambayo Mnzava anasema kuwa pia ni kinyume na sheria.


“Mbali na ulinzi shirikishi kuundwa kuanzia ngazi ya mitaa, lakini pia hakuna mtu, taasisi au kikundi binafsi ambacho kinaruhusiwa kuunda ulinzi shirikishi, kwahiyo bado nasisitiza kuwa hawa wako kinyume na sheria,” Amesema Mnzava.


Aidha kuna taarifa kwamba askari wa ulinzi shirikishi hao wamekuwa wakitembea na pingu na wakati mwingine kuwafunga watu wanapowakamata. “Hii nayo ni kinyume na sheria, kazi ya ulinzi shirikishi ni kumkamata mtuhumiwa na kumpeleka panapotakiwa, kama ni kituoni, au Ofisi ya Serikali za mitaa au kwa Ofisi ya Mtendaji, zaidi ya hapo ni kuvunja sheria,” amesema Mnzava.


Anaongezea kwa kusema kuwa ndiyo maana baada ya kuundwa kwa vikosi vya ulinzi shirikishi huwa wanapata semina maalum kutoka kwa Jeshi la Polisi kuwafundisha mbinu mbalimbali za kuwakabili waharifu.


Taarifa zilizolifikia Gazeti Jamhuri ni kwamba kuna mchango wa 1,000 kila siku kwa ajili ya askari wa ulinzi shirikishi. Katibu wa chama wamiliki wa mabasi (TABOA), Enea Mrutu alisema kuwa umuzi huo wa kuchangia kiasi hicho cha fedha ulipitishwa na mkutano mkuu na hivyo hakuna wa kulipinga hilo.


“Haya ni moja ya makubaliano tuliyofanaya katika mkutano mkuu kwahiyo hakuna wa kuyapinga labda aitishe mkutano mwingine,” Amesema Mrutu kwa njia ya simu kutokea mkoani Kilimanjaro.


Kwa upande wa uundaji wa kikosi cha ulinzi shirikishi, Mrutu alisema kuwa  Kituo cha Ubungo kina sheria zake, kwahiyo pale si mpaka kuleta ulinzi shirikishi ambaye katoka katika serikali za mitaa.


“Ukishasema kituo cha mabasi cha ubungo, basi ujue kuna sheria zake, tuliamua kuunda ulinzi wetu baada ya kuwatoa wale wote ambao walikuwepo awali, Walikuwa ni wezi hatari, labda nikueleze kwamba hawa tulio nao kwa sasa wanafanya kazi vizuri, sitaki kuwatetea sana uenda wana mapungufu yao ila kuna unafuu sana,” amesema Mrutu kwa njia ya simu.


Kuhusu suala la pingu, Mrutu alifafanua kwamba kwa kawaida kila ulinzi shirikishi anatakiwa kuwa na askari wa jiji wanapokuwa kazini, kwahiyo askari wa jiji au askari polisi ndiye anakuwa na pingu na wala siyo Ulinzi shirikishi.


Suala la vibali maalum vya kuingilia (Gate Passes)

Hivi karibuni kumeanzishwa utaratibu mpya katika kuhakikisha kwamba wapiga debe pamoja na watu wengine ambao hawana kazi maalum wanapungua kituoni hapo.


Hili nalo limelalamikiwa na wengi, hasa wale makarani ambao walikuwa wakifanya kazi katika mabasi mbalimbali.


Gharama ya kitambulisho kimoja ni Sh 20,000, ambazo zinatakiwa kulipwa na kampuni kwa ajili ya wafanyakazi wake.


Hata hivyo baadhi ya wafanyakazi wa mabasi wamelalamikia zoezi la ucheleweshaji wa kupatikana kwa vitambulisho hivyo,  hivyo kusasababisha watu kuendelea kukamatwa wakati wakisubiri kupewa vitambulisho.


“Zoezi hili japokuwa linatoa nafasi kwa watu wachache lakini pia kuna ucheleweshaji wa vitambulisho hivyo, hali ambayo inasababishwa sisi kukamatwa, kwa mfano mimi kama leo nilitaka nisije kwasababu jana walitukamata nikatoa Sh 50,000, hawa jamaa hawana utaratibu na leo tena wanaweza wakakukamata ili uwape tena 50,000, amesema kijana mmoja.


Chini ya utaratibu mpya, kila kampuni inatakiwa kuwa tu anasema kwamba waliamua jambo hili katika mkutano wa wadau wote, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa watu.


“Awali tulipofanya mahesabu tukaona kuwa endapo tutakuwa na watu zaidi ya 2-6 tunaweza kujikutana tunakuwa na watu 600, tukakubaliana idadi huyo, kila mdau anajua hilo kwa na hakuna wakulipinga,” Alisema Mrutu.


“Unajua hapo Ubungo ni kama tuko katika vita, mwanzoni hali ilikuwa mbaya kwa maana ya wizi na vibaka walikuwa wengi, kwahiyo kwa sasa hivi ni kama kuna watu ambao wanaona kama tumewazibia riziki zao,” Alisisitiza Mrutu.


Hata hivyo vibali hivyo vimekuwa vikilalamikiwa pia kutokana na kuwa na sahihi ya kiongozi wa jiji, yaani meneja wa kituo cha Ubungo pamoja na ile ya uongozi wa TABOA, tofauti na vile vya awali anbavyo vilikuwa na sahihi ya mmiliki wa gari ambaye ni mwajiri karani husika pamoja na sahihi ya jiji.

 

By Jamhuri