Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kongwa mkoani hapa imesema ina mpango wa kuboresha miundombinu katika maeneo ya kihistoria wilayani hapo ili kuwa moja ya sehemu zitakazovutia watalii.

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa wilaya ya Kongwa Remidius Mwema wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Marathoni yenye lengo la kutangaza utalii na historia ya ukombozi wa nchi za kusini mwa afrika.

Hatua hiyo imekuja huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) likiwa limeridhia kujenga kituo cha kitaifa mkoani Dodoma kwa ajili ya makumbusho ya urithi wa ukombozi ili kuhifadhi historia hiyo muhimu kwa Bara la Afrika.

Mwema ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuenzi maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kutambua mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afika na kwamba maeneo yote yaliyotumiwa na wapigania Uhuru yatabaki kuwa kumbukumbu ya kipekee.

Mkuu huyo wa wilaya ya Kongwa amezitaja nchi hizo ambazo viongozi wake waliweka kambi wilayani hapo kuwa ni takribani nchi tano ambazo ni Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Msumbiji na Angola.

“Ni muhimu Sehemu ya fedha zitazopatikana kwenye mbio hizo kusaidia kuboresha maeneo ya kihistoria yanayo patikana wilayani hapa hususani maswala ya kielimu hasa ukarabati wa madarasa yaliyotumiwa na madawati, ” amesema

Naye,Msimamizi na mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika Boniface Kadili amesema kuwa Kongwa inakwenda kuingizwa kuwa kituo cha urithi wa taifa na baadaye kwenye urithi wa dunia kwani ina vigezo vyote.

Amesema hatua hiyo ni muendelezo wa program ya urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika wenye lengo la kutambua na kuhifadhi kumbukumbu za harakati za kutafuta uhuru wa nchi za Afrika ambapo nchi ya Tanzania
ilishiriki katika kutoa msaada kwa nchi hizo.

Amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara kupitia kituo cha urithi imetenga fedha maalum kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mahandaki yaliyotumiwa na viongozi wa nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo handaki la Kongwa ambalo lilitumiwa na hayati Samora Machel akiwa kongwa kwa ajili ya kujihami na hatari.

“Nitumie fursa hii kuelekeza kuwa maadhimisho ya siku ya Afrika ambayo hufanyika Mei 25, kila mwaka, yafanyike hapa Kongwa kitaifa ili kuendelea kuitangaza eneo hili na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utaliii uliopo Kongwa, ” amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, White Zuberi ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa tangu mwaka 2010 wamekuwa wakipambana ili kufanya Kongwa ipate hadhi inayostahili.

Amesema mara kaadha amekuwa akipokea ugeni kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao wanakuja kwa lengo la kuona makaburi ya mashujaa wao wa ukombozi lakini bado hawaoni umuhimu wa kuyahifadhi na kuyatunza kwa ajili ya kuyaenzi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

“Mwaka 1995 kikosi cha Jeshi kiliondolewa Kongwa baada ya wapiganaji kuondoka lakini tunashukuru sasa Rais Samia Suluhu Hassan amerudisha kambi ya Jeshi kwenye eneo la kihistoria,” amesemamafunzo

Wilaya ya Kongwa ni moja ya maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa Bara
la Afrika ambapo yanapatikana makaburi ya wapigania uhuru waliopoteza
maisha wakati wa vita vya ukombozi pamoja na handaki la kijeshi
lililotumiwa na Rais wa Msumbiji Samora Machel kwa ajili ya kujificha .

By Jamhuri