Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Maambukizi ya malaria yametajwa kupungua kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya mjini huku hali ikiwa bado mbaya vijijini mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kitengo cha kudhibiti Malaria Manispaa ya Tabora umebaini kuwa vijijini hali ya maambukizi bado ni kubwa ikiringanishwa na mjini.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya ugawaji vyandarua bure kwa wananchi wa Kata ya Isevya Manispaa ya Tabora ikiwa ni mpango wa serikali wa kudhibiti Malaria nchini, Mratibu wa Malaria wa Manispaa hiyo Devota Msele, alisema maambukizi ya ugonjwa huo yamepungua, kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya mjini huku hali ikitajwa kuwa mbaya maeneo ya vijijini.

Devota, alitaja sababu za kupungua kwa ugonjwa huo baadhi ya maeneo ya mjini kuwa ni mabadiliko ya wananchi katika kufanya usafi wa mazingira na kuondoa mazalia ya mbu.

“Maeneo ya vijijini hali bado ni mbaya na miongoni mwa sababu ni kuendelea kuwapo kwa dhana potofu ya matumizi ya vyandarua kwamba vinapunguza nguvu za kiume na kuwapo kwa hali ya uchafu unasababisha mazalia ya wadudu wasumbufu kama kunguni na mbu ndani ya nyumba,”alisema.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Tabora mjini Luis Bura alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuondokana na dhana potofu juu ya matumizi ya vyandarua hivyo huku akisisitiza kuvitumia vizuri malengo ya serikali katika kupambana na Malaria yatimie.

“Serikali kwa kushirikiana na wafadhili inatumia fedha nyingi kugharamia vyandarua hivi ambavyo vinaratibiwa na Bohari ya Dawa (MSD), lengo ni kuwakinga watu wake dhidi ya ugonjwa wa Malaria ni wajibu wetu watendaji kuvisimamia na wananchi kutumia ipasavyo,”alisema.

Alitumia fursa hiyo kupiga marufuku matumizi ya vyandarua hivyo kufugia kuku,kuvulia samaki na kuzunguushia uzio kwenye matuta ya bustani za mboga mboga ambapo na kusisitiza kuwa atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa MSD Tabora Adonzedek Tefurukwa alitoa wito kwa wananchi waliopatiwa vyandarua hivyo kufuata maelekezo na kueleza kuwa Vyandarua hivyo vimewekewa dawa ya kuua mbu na haina madhara kwa binadamu.

Alisema Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa kinara kwa maambukizi ya Malaria ambapo una asilimia 23.4 kitaifa hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanatumia ipasavyo vyandarua hivyo.

By Jamhuri