Afisa wa cheo cha juu wa Korea Kaskazini amemlaumu Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence kwa kuwa “mjinga” na kuonya kuwa kutakuwa na maonyeshano ya ubabe wa nyuklia ikiwa mazungumzo yatafeli.

Choe Son-hui alisema Pyongyang haitaweza kuibembeleza Marekani kwa mazungumzo.

Siku za hivi karibuni pande hizo mbili zimeonya kuwa mkutano wa Juni 12 unaweza kuharishwa au kufutwa kabisa.

Korea Kaskazini ilisema itafikiria tena iwapo itahudhuria mkutano ikiwa Marekani itaendelea kusisitiza kuwa iachane na mpango wa silaha za nyuklia.

Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumanne alisema Korea Kaskazini ndiyo ingetimiza masharti ya kufanyika kwa mazungumzo hayo.

Choe Son-hui amehusika kwenye mazungumzo mara kadha na Marekani kwa karibu miaka kumi iliyopita.

Alimuita Mike Pence mjinga kwa kuifananisha Korea Kaskazini, taifa la nyuklia na Libya, ambayo anasema ilikuwa na vifaa vichache tu ilivyokuwa ikicheza navyo.

“Kama mtu ambaye nimehusika kwenye masuala ya Marekani, siwezi kuficha mshangao wangu kufuatia matamshi kama hayo ya kijinga yanayotoka kinywani mwa Makamu wa Rais wa Marekani,” alisema.

Bi Choe alisema Pyongyang haikuwa inabembeleza kufanyika mazungumzo. “Ikiwa Marekani itakutana nasi au kutukabili kinyuklia inafuatia na uamuzi na tabia za Marekani.”

Mshauri wa masuala ya ulinzi wa Marekani John Bolton naye aliikasirisha Korea Kaskazini wiki iliyopita kwa kusema kuwa utatumiwa mfumo wa Libya katika kuondoa zana za nyuklia.

 

By Jamhuri