Wakati wakulima wa korosho wanaanza kufaidi – (kwa Kimwela ‘kupoka’) neema za korosho, mara mwaka ule wa 1973 serikali ikavunja ile bodi ya mazao, lakini ikaunda mamlaka maalumu kwa zao letu la korosho. Mamlaka hiyo ilijulikana kama CATA (Cashew Authority of Tanzania).
Majukumu ya mamlaka hii yalikuwa kuweka bei za korosho, kununua na kuuza korosho. CATA ilishughulikia kikamilifu zao la korosho, kupanga bei, kununua korosho, kuzi-grade kuzisafirisha na kuziuza nje ya nchi. (Angalizo: moja ya alama ya ufanisi wa CATA ni yale majengo kama ‘CATA Club’ na majumba ya watumishi yaliyopo pale Mtwara).
CATA waliweza kukusanya korosho kutoka unions zote na kuzipeleka Mtwara kwa mauzo. CATA walizihudumia pia barabara za wilayani kwenda vijijini zinakonunuliwa korosho za wakulima. Ndiyo sababu kutoka mwaka 1960 – 1972, korosho zote zilinunuliwa kutoka kwa wakulima na kuuzwa kwa wafanyabiashara wa nje kwa pamoja.

Utaratibu huu ulionekana kufanikiwa kwa sababu kule India nako kuliundwa chama kilichoitwa ‘The Cashew Corporation of India’ kilichopewa jukumu la kununua korosho ghafi kutoka nje na kuwauzia wenye viwanda vya ubanguaji kule India. Shirika hilo lilikuwa na makao makuu yake katika mji wa Cochin, Jimbo la Kerela. Uhusiano ulikuwa kati ya NAPB na Cashew Corporation of India.
Kwa njia ya NAPB baadaye ikawa CATA, ndiye alikuwa mnunuzi pekee wa korosho za wakulima na ‘exporter’ pekee wa kuzipeleka nje (buyer and exporter). Korosho zote zilitiwa katika madaraja, na India ilileta wataalamu wake kufunza wananchi namna ya kupanga madaraja ya korosho. Basi kila penye ‘union’ palikuwa na mtu anayepanga madaraja ya korosho.

Wahindi walizichambua korosho zetu na kuzipanga kiubora, zile za Tunduru, Masasi na Nachingwea, kundi lake, (walizitambua kama CD, KL) wakati zile zilizotoka Newala na Mtwara waliweka kundi lake na (kuzitambua kama AFGHI); wakati korosho kutoka pwani ya Lindi, Kilwa na Dar es Salaam zilitiwa katika kundi lake (zikatambulika kama BE). (NB. Maana ya herufi hizo sizijui) la muhimu ni kuwa korosho zote zilipangwa kwa daraja la kwanza (I) au ‘standard grade’ na daraja la II au ‘under grade’.
Kwa ujumla korosho zetu zilikuwa bora kuliko zile zilizotoka nchi jirani ng’ambo ya Mto Ruvuma. Zote ziliuzika, kadiri miaka ilivyopita ndivyo zao la korosho liliongezeka kwa wingi katika nchi hata serikali ikashawishika kujenga viwanda vya kubangulia korosho zetu kwa kujipatia kipato zaidi.

Msimu wa mwaka 1973/1974 tani 110,000 za korosho zilivunwa na kuuzwa zote. Mwaka 1974 serikali ilitafuta mtaji kutoka Benki ya Dunia – mkopo wa kujengea viwanda vya kubangua korosho.
Uchambuzi yakinifu uliotolewa wakati ule ulikubaliwa na Benki ya Dunia kuwa zao la korosho likibanguliwa humu nchini kutakuwa na faida kubwa kiuchumi.
Basi, serikali ilipanga kujenga viwanda kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza viwanda vijengwe Lindi (tani 10,000), Masasi (tani 10,000), Newala (tani 10,000), Mtama (tani 5,000) na Nachingwea (tani 5,000).

Awamu ya pili ilikuwa vijengwe Tunduru (tani 10,000), Newala II (tani 10,000), Mtwara (tani 10,000) na Masasi II (tani 5,000) baada ya vile viwanda vya awamu ya kwanza kuonyesha mafanikio yake katika ubanguaji.
Baada ya mipango hiyo mizuri yote kukamilika katika makaratasi kumetokea nini hadi leo tuko hoi watu wa Kusini? Korosho zetu haziuziki, viwanda vyetu vimekuwa magofu (white elephants – wasemavyo Waingereza) hata watalii hawavutiwi kuyatembelea? Hali ya wakulima sasa inakuwa mbaya hata kulipa karo za shule hawawezi. Korosho mkombozi wa Kusini kulikoni? Mimi ninaona mambo kadhaa yamesababisha nchi kufikia hapo hivi sasa.
Pamoja na nia njema hiyo ya serikali kuhimiza zao la korosho na kutaka zibanguliwe katika viwanda vyetu ili wakulima wafaidi bei nzuri kwa korosho zao, nia hiyo njema bila vitendo kabambe haitufikishi popote kiuchumi.
Ninazo sababu tatu ambazo nafikiri zimezorotesha uchumi utokanao na korosho.

Mosi, ile Sera ya Vijiji vya Ujamaa ya mwaka 1974 ilirudisha nyuma zao korosho. Mashamba kadhaa kule Kusini yaliachwa porini, wenyewe walipohamishiwa kwenye vijiji vipya vilivyopangwa na serikali. Mikorosho iliungua moto, maana mashamba yale hayakupaliliwa, hivyo korosho hazikuzaa vizuri tena. Hii ilisababisha zao la korosho liporomoke kutoka mavuno ya tani 117,486 msimu wa 1974/1975 hadi tani 83,738 msimu ule wa 1975/1976. Hizi ni tani zaidi ya 33,000.
Pili, mwaka 1975 serikali ilivunja vyama vya ushirika tulivyoita ‘unions’ ambavyo vilikuwa mahali maalumu pa kuuzia korosho za mkulima. Serikali iliamua vijiji vya ujamaa ndivyo vinunue korosho. Vijiji vyenyewe havikuwa na uwezo kifedha, havikujiandaa kwa ununuzi mkubwa namna hiyo, na yale mabenki yaliyokuwa yanakopesha ‘unions’ hayakuwa tayari kukopesha vijiji vya ujamaa. Katika hali namna hii, korosho za mkulima hazikununulika ilivyotazamiwa.

Tatu, ule mpango wa kwanza uliokubaliwa mwaka 1974 wa kujenga viwanda kwa awamu mbili haukufuatwa. Waroho waliishauri serikali viwanda vyote vijengwe kwa wakati mmoja huo huo ingawa waliona zao la korosho linaporomoka.
Isitoshe watu walikuwa wamekiuka lile sharti la kusema tuone viwanda vya kwanza vinabangua namna gani, lakini kabla ya kupata mrejesho wa ufanisi huo, waroho wakaishauri serikali iendeleze ujenzi wa viwanda ile awamu ya pili. Huku ni kumfanya mtoto ajitahidi kukimbia wakati hata hajaweza kusimama na kuanza kutembea! Hili lilikuwa kosa kubwa sana kiutendaji.
Inaonekana basi serikali ingawa iliona uzalishaji wa korosho unaporomoka, ujenzi wa viwanda unaongezeka kiholela, mabenki hayakuweza kukopesha vijiji vya ujamaa kama yalivyofanya kwa ‘unions’, lakini hakuna hatua thabiti zilizochukuliwa wakati ule kuzuia hayo yasitokee, hivyo kuwahakikishia wakulima kipato cha jasho lao.

Miaka ile ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 uzalishaji wa korosho ulizidi kudorora. Serikali mwaka 1984 ilibadilisha ile mamlaka ya korosho na kuwa Bodi ya Korosho Tanzania – Tanzania Cashewnut Marketing Board (TCMB). Bodi hii bado haikuweza kuliendeleza zao hili la korosho. Basi, katika mparaganyiko namna hii, kila kitu kinaweza kutokea na kila mtu anaweza kubwata lawama zake.
Baadhi ya wafanyabiashara wenye kujiweza kifedha (labda kwa baraka za Wizara ya Kilimo) walianzisha chama cha wanunuzi wa korosho wakakiita Umoja wa Korosho Tanzania (CBAT) (Cashewnut Buyers Association of Tanzania). Umoja huu ulibuni mfuko wa kuendeleza zao la korosho ulioitwa CIDEF (Cashenuts Industry Development Fund) ili uwasaidie katika azma yao ya kununua korosho kiulaini.

Wafanyabiashara wote ulimwenguni wana tabia ile ile ya kununua vitu kwa bei ya chini kisha kuuza kwa bei ghali. Mipango ikasukwa hadi wizarani ambako kulianzishwa kitengo maalumu cha uendelezaji korosho kilichoitwa CMU (Cashew Management Unit). Kutoka mwaka 1994 mpaka mwaka 2000 wafanyabiashara walijaribu sana kuonyesha kuwa wao ndio mkombozi wa zao la korosho, na wao wana uchungu na wakulima na watasaidia kwa hali na mali.
Mimi ninaamini hiyo ilikuwa ni ‘janja ya nyani tu’, maana kuna usemi wa Kiingereza juu ya kilio cha mamba kuwa ‘shading crocodiles tears’ – yaani kutokwa machozi kwa mamba akamatapo windo lake. Mwenye usongo na korosho katika nchi hii ni mkulima.
Kule India nako lile shirika la Cashew Corporation of India lililonunua korosho zetu zote lilishavunjwa. Hivyo, wanunuzi binafsi walikuwa wanajinunulia korosho kiholela kwa viwanda vyao vya kubangulia korosho. Wakati wa vurugu za namna hii serikali yetu ikaruhusu soko huria kwa korosho! Matajiri wale wa India wakawatumia mawakala wale wafanyabiashara wa umoja wa korosho hapa kwetu.

By Jamhuri