Kwako Waziri wa Mambo ya Ndani

Mheshimiwa Kangi Lugola,

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sisi askari wastaafu wa Jeshi la Polisi tunakupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya ingawa kuna changamoto za hapa na pale.
Tunakutia moyo na tunaomba Mungu akuzidishie hekima katika utendaji wako.
Ndugu Waziri, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kubwa. Inaundwa na Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji; na Uhamiaji. Kutokana na ukubwa huo, wakati mwingine si rahisi kufahamu kila jambo pengine mpaka ujulishwe.
Ndugu Waziri, sidhani kama unatambua kuwa hadi sasa karibu askari Polisi wote tuliostaafu mwaka 2017 bado tunaishi makambini kutokana na kutolipwa pesa za kusafirisha mizigo yetu kwenda makwetu.

Kila tunapouliza kwa viongozi wetu mikoani tunajibiwa kifupi tu kuwa makao makuu hawajatoa pesa. Baadhi ya wastaafu ambao wamebahatika kulipwa mafao yao walijisafirisha wenyewe.
Ndugu Waziri, kama tulivyotangulia kusema kuwa hata Jeshi la Magereza lipo chini yako, cha kushangaza wenzetu wa Magereza wote waliostaafu mwaka 2017 na mwaka huu wa 2018; na hata wanaotazamiwa kustaafu Oktoba, 2018 wameshalipwa pesa za kusafirisha mizigo.
Ndugu Waziri, sisi Polisi kuna tatizo gani, wakati wote ni wa baba mmoja na katibu mkuu ni wetu sote?

Ndugu Waziri, ebu fikiria mtu amestaafu lakini bado anaendelea kuishi kambini. Wewe uliwahi kuwa askari Polisi, hakuna jambo usilolifahamu.
Tunateseka. Tunaomba tupewe fedha zetu ili twende makwetu.

Asante,
Wastaafu wa Jeshi la Polisi.