Zilipokuja habari za gazeti hili makini kuhujumiwa kwa nakala zote hili kununuliwa, watu wa hapa hawakuamini. Nilikuwa kwenye kijiwe cha kuvuta sigara – si unajua kila eneo la kazi pametengwa eneo la kupunguzia baridi – nilipozisikia.
Eti kwamba kibopa mmoja, mawakala wake, marafiki au wadau kwenye biashara na labda kashfa, walikuwa wamezuia gazeti kuwafikia walengwa. Nilipokuwa kijiweni, baada ya kuwa nimefungua na kusoma kwenye soft copy, habari ndefu iliyofanya gazeti lihujumiwe kwa kununuliwa lote na kutumbukizwa kwenye choo cha shimo au kuchomwa moto, kichwa changu ghafla kilikuwa na maswali mengi. Hakuna anayeweza kusema nilikuwa naichafua nchi yangu kwa kueleza jambo lile, lakini pia hakuna atakayesema aliyenunua gazeti lote la JAMHURI nchi nzima ni mtu mzuri. Mmoja wa jamaa waliokuwa wakisokota tumbaku kwa ajili ya kuvuta, akauliza huyo mtu ana mtandao mkubwa kiasi gani na anajiamini vipi hadi afanye hivyo! Maana kitu kama hicho kingetokea hapa London au upande wowote wa Uingereza, si tu kwamba mhusika angeshindwa bali pia angekamatwa na polisi ndani ya muda si mrefu na tume ingechunguza na kuweka wazi kila kitu. Michezo ya kufichaficha mambo ni ya kizamani.

Kwa mtu mwenye usafi na nia safi, na anayefanya kazi au biashara safi, anatakiwa kuwa muwazi na mkweli na kuacha vyombo vya habari vifanye kazi zake. Mawaziri kadhaa wameachia ngazi wenyewe hapa Uingereza baada ya tetesi kidogo tu kuvuma kuhusu mambo kadhaa waliyofanya – kama kusaidia wadau kupanda cheo au kuingiza wapambe wasiohusika kwenye misafara ya kiuwaziri. Kusema kweli, wanaachia ngazi kwenye mazingira yanayokuwa hayajajifunua wala kuwa na dalili za kuweza kujulikana – wanajitokeza wenyewe na kusema; ‘basi, yaishe’. Yametokea kwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Dk. Liam Fox, majuzi, alipomjumuisha rafiki yake mmoja milionea kwenye msafara wa kiwaziri. Sasa inapofika mahali mtu anaandikwa, anajidai kuwa na mtandao mkubwa na kuanza kununua mafungu ya nakala ili habari isiwafikie wananchi, kwa kweli inatia kichefuchefu. Angefanya hivyo yeyote hapa angedakwa na kila mtu kwenye jamii angemsonya na angeishia kulipa hata faini na fidia.

Lakini kwa kuwa tumejijengea mfumo wa ajabu kidogo hapo nyumbani, hakuna mtu anayethubutu hata kutaja jina la huyo ‘jeuri’ aliyefanya hivyo. Nimesoma ujumbe mwingi sana kuhusu suala hilo, lakini kila mtu anaishia kusema tu kwamba gazeti limehujumiwa, na wanaoona huruma wanalia na kusema huyo mtu mbaya sana, machozi yanatoka tu na mwisho watu na ardhi vinaloana, basi! Unajua ni kwa nini yote yanakuwa hivyo? Ni kwamba ukimtaja mhusika, basi uwe tayari kupokea polisi wakija kukukamata au mhusika akuburute mahakamani kwa kumchafulia jina. Eti kafanya uchafu wake, kahujumu gazeti na kuzuia umma kufikishiwa habari, halafu akitajwa anang’aka na kuamuru ‘vijana wake’ kwenda kukamata watu au mawakili wake kuwaburuta mahakamani wahusika na kudai fidia, huku mwenyewe akiwa amejirundikia mabilioni benki. Kuwa masikini ni ghali sana, ndiyo, kweli kuwa masikini hugharimu sana kwa sababu mwenye mapesa atazidi kuyasaka na kuwakalia wanyonge bila sababu yoyote.

Wale wasio nayo wanaoanika ukweli wa jinsi wanyonge wanavyoonewa kwa mali zao kutapanywa, kumegwa, kuuzwa au kuharibiwa, wanaishia kukamatwa, kudhalilishwa na kuitwa majina ya kila aina. Jamaa aliyekuwa anavuta moshi uliotoka kwenye sigara zetu bila yeye kuvuta, akivutiwa na story yetu. Alikuwa na hamu ya kumjua mhusika kwa sababu aliwahi kukaa Dar es Salaam na hufuatilia habari za Afrika Mashariki mtandaoni, japo kwa Kiingereza. Nami kama ilivyokuwa kwa wadau wakuu na wenye mapenzi mema hapo Dar, niliishia kusema labda mhusika aliandikwa kwenye hilo gazeti na yeye hakupenda. Tukaanza kufikiria ingekuwa hapa Uingereza mtu angeanzia wapi. Maana ukiacha magazeti yanayouzwa kwa peni 50 (Sh 1,250) ambayo kwa hapa ni kidogo sana, yapo ya bure. Ukinunua magazeti mengi lazima uulizwe unayapeleka wapi, maana si kama hapo Bongo mhusika – kwenye meza, mbao au venda anataka magazeti yamwishie akafanye shughuli nyingine au akapumzike.

Hapa, pamoja na ubaya unaoweza kuwatawala watu hawa, kuna maadili yasiyokiukwa bwana we! Na story inaweza kuwa kwenye magazeti yote japo kwa ukubwa au udogo tofauti, isipokuwa zile ambazo ni ‘exclusive’. Sasa kwa hayo magazeti ya bure sijui jamaa angeagiza malori ili kukusanya nakala hizo au angefanyaje; maana nakala kibao zinasambazwa kila kituo cha treni, zinamwagwa na kwa kumwagwa hivyo maana yake kila mtu ana nakala yake, na vituo vilivyo vingi, ikitokea mtu akajaribu kununua au kuyakusanya, basi Waingereza hawangekuwa na cha kufanya bali ‘kucheka hadi wafe’! Wanacheka kwa maana wanajua kitendo afanyacho anajipalia mkaa.

By Jamhuri