“Sheria inatutaka tufanye uchunguzi wa tuhuma zozote na katika hili, CAG alitakiwa atupe taarifa. Lakini sisi baada ya kusikia bungeni tulimwandikia barua kumwomba atupatie ripoti ya mambo yanayotuhusu (ili) tuanze kuyashughulikia haraka,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah.
Hata hivyo, Dk. Hosea aliyenukuliwa na baadhi ya magazeti alikataa kusema ni kina nani watachunguzwa, akidai kuwa kifungu cha 37 cha Sheria ya Takukuru ya Mwaka 2007 kinazuia kuzungumzia mchakato wowote unaohusu uchunguzi wa tuhuma za rushwa.

Alikuwa akizungumzia ufisadi ulioibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na ripoti yake kuwasilishwa na kujadiliwa katika Mkutano wa Saba wa Bunge.

Akionyesha kuwa hatanii, Dk. Hoseah amesema watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine, watafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP) kwa hatua za kisheria.

Hivyo ndivyo alivyosema na kufanya nizikumbuke ahadi alizotoa huko nyuma; nzito kuliko zote ikiwa ni ile aliyodai akiwa mjini Arusha mwaka jana kwamba Takukuru ilikuwa ikiandaa kesi kubwa tatu za rushwa ambazo zingetikisa nchini.

Sitaki afikiri kuwa simwamini anapozungumzia utendaji au mikakati ya taasisi yake, lakini namtilia shaka kunapokosekana utekelezaji wa ahadi anazotoa na kushindwa pia kuzungumza chochote kinachoendelea.

Ndiyo maana niliposoma ahadi yake mpya nikakumbuka ile ya zamani alipowaambia waandishi wa habari jijini Arusha mwaka jana, kuwa Tanzania ingeshuhudia kesi kubwa tatu za rushwa zilizokuwa tayari zikingoja tu kupelekwa mahakamani, lakini hakutaja hata moja au kugusia mazingira yake yoyote.

Alisababisha watu wafikirie maeneo ambayo yangeweza kuzihusu, likiwamo la tuhuma za wizi wa fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Walilazimika kufikiri hivyo kutokana na maswali ya waandishi wa habari aliyoulizwa na jinsi alivyojibu, yote yakihusu watuhumiwa wa EPA wanaodhaniwa kulindwa na Serikali. Akaombwa awaambie Watanzania kuhusu undani na ukweli wa madai hayo.

Katika hali hiyo, jibu alilowapa akiwataka wajiandae kushuhudia kesi kubwa zaidi za rushwa zikifunguliwa “hivi karibuni na kuitikisa Tanzania”. Jibu hilo lilimfanya kila mmoja asubiri kwa hamu ili kujua ni kina nani wangepelekwa mahakamani.

Alisema pia kuwa moja ya kesi hizo ni za rushwa iliyotokana na mchakato wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 katika Mkoa wa Iringa. Ikaondolewa mahakamani huku Takukuru ikitakiwa iyarekebishe mashitaka na kuifungua upya. Nayo alisema ingerejeshwa kwa hakimu ndani ya siku chache.

Lakini tangu hapo hakuna kesi yoyote kati ya hizo alizozisema iliyofunguliwa. Hata iliyotakiwa kufanyiwa marekebisho tu ili irejeshwe mahakamani, nayo imebaki kinywani mwake.

Nimesema sitaki ionekane kwamba siiamini sana Takukuru wala ahadi zinazotolewa na Dk. Hoseah kwa niaba ya taasisi hiyo ya umma, lakini hilo haliwezi kunifanya nishindwe pia kuitilia shaka kwa namna moja au nyingine.

Ripoti ya fedha za Serikali iliyotolewa na CAG inaonyesha, kwa mfano, kuwapo ubadhirifu wa Sh milioni 874.9 za Wizara ya Maliasili na Utalii, Sh bilioni 1.1 zilizopelekwa Wizara ya Afya, Sh bilioni 1.3 za mauzo tata ya kiwanja cha Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) na Sh bilioni mbili zilizopotea katika Bodi ya Pamba Tanzania.

Nyingine ni Sh bilioni 1.8 walizolipwa wafanyakazi hewa serikalini, Sh bilioni nane za ununuzi wenye utata, Sh bilioni 15.4 zinazohusu ukwepaji kodi, Sh bilioni 21 za mabilioni ya JK, Sh bilioni 29.646 za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Sh bilioni 49 katika Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali.

Wizi huo pia umepoteza Sh trilioni 1.3 kupitia mabadiliko yasiyoidhinishwa na vyombo vinavyohusika, Sh trilioni tatu zilizotolewa kama dhamana na Sh trilioni tano zilizotumika kununua magari ya Serikali.

Kinachonikera katika taarifa ya Dk. Hoseah, ni kudai Takukuru imeanza kuwachunguza watendaji wote waliohusika kwa namna moja au nyingine na upotevu wa mabilioni hayo ya fedha za umma.

Nakerwa kwa sababu wizi uliobainishwa na CAG katika ripoti yake haukuanza mwaka huu bali upo miaka yote. Najiuliza kwa nini Takukuru haikuwahi kuwachunguza watuhumiwa na badala yake ikawaacha waendelee kuhujumu uchumi wa nchi?

Hata Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali Kuu (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) nazo zinafichua uozo unaotisha, lakini Takukuru imekuwa haisemi wala kufanya chochote.

Naona safari hii imejitokeza, si kwa sababu ilipanga bali kwa vile Rais Jakaya Kikwete ameonyesha kukasirishwa na ripoti hiyo na kuamua kuchukua hatua yeye mwenyewe.

Takukuru imejitokeza kwa aibu ilipoona mkuu wa nchi ameshindwa kuvumilia, akakitaarifu chama chake kinachotawala (CCM) kuhusu uamuzi wake ili kukomesha wizi huo unaofanywa kila mwaka.

Takukuru inajikosha kwa Rais aliyesema “ole wao” watakaobainika kuhusika na wizi huo, hivyo inataka kuuhadaa umma ili endapo baadhi yao watashitakiwa mahakamani, basi ionekane kuwa taasisi hiyo inafanya kazi nzuri, wakati sivyo.

Kama ingekuwa makini kutekeleza wajibu wake, isingesubiri Rais akasirike ndipo ijitokeze kuanza kuwachunguza watuhumiwa; jambo ambalo hata mtoto wa shule ya msingi haiwezi kumdanganya.

Iwapo haikusubiri hadi Rais akasirike ndipo ijitokeze, Takukuru ingetuambia kwa nini haikuwa ikichunguza uozo unaobainishwa na CAG kila mwaka, badala yake imefanya hivyo baada ya mkuu huyo wa nchi kuonyesha hadharani hasira zake?

Taasisi hiyo ituambie endapo inadhani Watanzania wote hawana kumbukumbu utadhani kuku wa kisasa, na pia iseme ni kwa nini ilikuwa haizifanyii uchunguzi ripoti zote za CAG hadi ilipoona Rais amekarisika.

Ndiyo maana bado naikumbuka ahadi iliyotolewa na Dk. Hoseah mwaka jana kule Arusha ya

“Tanzania ingetikiswa na kesi kubwa tatu za rushwa ambazo zingewahusu watu maarufu nchini”.

Nimesema sitaki afikirie kuwa simuamini yeye au Takukuru, lakini kwa vile tayari alishadanganya huko nyuma na kafanya hadharani, hakika nazitilia shaka ahadi zake hadi nione watu hao wakiburuzwa mahakamani na kuiacha Tanzania ikitikisika.

Nasisitiza kuwa haiwezekani taasisi hiyo iwe inasubiri Rais akasirike ndipo ijitokeze kutimiza wajibu wake. Nasema hilo halikubaliki hata kidogo.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0713 676 000 na 0762 633 244

1150 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!