Kujiuzulu Ndugai ni ukomavu wa fikra

DAR ES SALAAM

Na Javius Kaijage

Januari 6, mwaka huu ni siku ambayo Job Ndugai alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya uspika wa Bunge, hivyo kuandika historia mpya katika kitabu cha Tanzania.

Ni historia mpya kwa maana kwamba kumbukumbu zinaonyesha kuwa tangu Tanganyika (Tanzania Bara) kupata uhuru wake Desemba 09, 1961 hakuna kiongozi yeyote wa mhimili mkuu kwa maana ya Serikali, Bunge au Mahakama aliwahi kujiuzulu akiwa madarakani.

Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, mkoani Dodoma alichukua uamuzi huo kutokana na kauli yake ya kumpinga hadharani Rais Samia Suluhu Hassan kuhusiana na suala la mikopo yenye riba nafuu.

Baada ya Ndugai ambaye kimsingi alikuwa kiongozi wa mhimili muhimu kutofautiana na Samia, wananchi mbalimbali walianza kumpinga wakiwamo wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa nje ya chama chake.

Ni kweli Ndugai kama binadamu mwingine na raia wa Tanzania ambayo inaheshimu haki za binadamu alikuwa na haki ya kusema au kutoa maoni yake, changamoto inakuja kutokana na nafasi yake ya uongozi.

Kwa wanaompinga wanasema ni kweli inawezekana alikuwa yuko sahihi katika suala la kupinga mikopo lakini kwanini akumuendea Rais Samia na kumshauri kama aliona kuna tatizo?

Haya mchakato mzima ulifanyika hadi mkopo ukapatikana na yeye akiwamo katika mchakato huo, kwanini ageuke Yuda Iskariote mbele ya safari na kuamua kuongelea pembeni?

Kwanini awamu zilizotangulia zilikopa ili kuendesha nchi na nchi haikupigwa mnada, ije kupigwa mnada katika awamu ya Rais Samia?

Kwanini Ndugai ambebeshe Rais Samia mzigo mkubwa wa deni la taifa kana kwamba deni lote limeanzia katika uongozi wake ilhali lilianzia katika awamu zilizotangulia?

Aidha, inasemekana Dk. John Magufuli alikopa japo ilikuwa ni kimyakimya lakini Ndugai hakuwahi kumpinga, hivyo kuibua maswali mengi kwamba yamkini alimuogopa kiongozi huyo, hivyo analeta dharau katika uongozi wa Rais Samia.

Kutokana na hilo wengine wamekwenda mbali kwa kusema Ndugai anasukumwa na tabia za mfumo dume ndiyo maana amefanya hivyo katika uongozi wa Rais Samia.

Wananchi wakiwa katika mtazamo huo, Rais Samia kwa upande wake wakati akizindua awamu nyingine ya  ujenzi wa reli ya mwendokasi kutoka Dodoma hadi Tabora,  alionyesha dalili za kuhusishwa kupinga mikopo yake na masuala ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Ni wazi baada ya Ndugai kuona anasakamwa, aliamua kujitokeza mbele ya kamera na kinasa sauti kwa lengo la kumuomba msamaha Rais Samia huku akikiri kwamba amekosea kwa kauli ya kumkatisha tamaa mkuu wa nchi na kuahidi kuwa hatarudia kufanya hivyo.

Licha ya kuomba msamaha bado kelele za kutaka awajibike ziliongezeka na ndipo kwa ukomavu wake wa akili akaamua kung’atuka ili kulinda masilahi ya nchi na chama chake.

Ni ukweli usiopingika, Ndugai amechukua uamuzi mzito wa kujiuzulu nafasi yake ya uongozi lakini ameonyesha njia kwamba kiongozi unapohisi umekosea au umeteleza na watu unaowaongoza wakakosa imani na wewe, basi jiweke kando ili wengine waongoze jahazi.

Ndiyo, Ndugai ni Spika wa kwanza kujiuzulu lakini si kiongozi wa kwanza kufanya hivyo katika taifa letu, kwa sababu wapo wengi waliwahi kufanya hivyo ili kulinda heshima zao na taifa kwa ujumla.

Tunachojifunza hapa ni kwamba kiongozi muelewa akishatambua kuwa amekosea au ameteleza, iwe ni kwa njia ya ulimi au matendo, anatakiwa kuwajibika bila kutumia nguvu.

Ndugai baada ya kutambua kuwa amemkosea Rais Samia ambaye kimsingi licha ya kuwa yeye ni sehemu ya uongozi katika mihimili mitatu, lakini kiuhalisia ndiye mkuu wa nchi anayebeba majukumu mazito.

Hapo awali, Ndugai aliomba msamaha kupitia vyombo vya habari na akaona hiyo haitoshi, akaamua kujiuzulu nafasi yake ya uspika aliyokuwa ameitumikia takriban miaka sita.

Si viongozi na wanasiasa wengi ambao hufanya hivyo pindi wakikosea na kuamua kuchukua uamuzi kama wa Ndugai.
Katika mazingira ya namna hii tungeshuhudia kauli za kutatanisha ikiwamo: ‘‘Siwezi kujiuzulu nafasi yangu kwa sababu sioni kosa langu.’’

‘‘Sitajiuzulu nafasi hiyo labda kwa ngumi na mateke kwa sababu mimi sioni kosa langu.’’

Kwa hiyo si tu Ndugai angeweza kutoa matamshi hayo makali bali pia kama ingetumika nguvu nyingi kumuondoa katika nafasi yake huenda tungeshuhudia akitoa talaka CCM na kwenda kujiunga na vyama vingine, hivyo kukosa sifa za kuwa mbunge kwa mujibu wa Katiba iliyopo.

Ambacho tumekishuhudia kwa Ndugai katika barua yake ya kujiuzulu ni kuendelea kumshukuru Rais Samia aliyeko madarakani, wabunge wenzake waliomwamini, chama chake na wapiga kura wa jimbo lake.

Ni wazi Ndugai amekuwa mwalimu kwa viongozi/wanasiasa wengine wanaokuwa na kasumba ya kutunishiana misuli hata katika masuala ambayo kimsingi ni wakosaji.

Ndugai amekuwa mwalimu kwa viongozi na wanasiasa ambao hawataki kuwajibika licha ya kuwa kwa mujibu wa taratibu, kanuni, sheria na wakati mwingine katiba wako kinyume kabisa cha uhalisia.

Ndugai licha ya kumkwaza Rais Samia kwa kauli zake lakini alionekana kujutia kosa hilo, kitu ambacho ni adimu kukipata kwa wanasiasa na viongozi wengi wa sasa hivi.

Wengine hufikiri kuomba msamaha ni kuonyesha unyonge kwamba haujui kujisimamia, kumbe sivyo, kwa sababu kuomba msamaha hakukupunguzii chochote na maisha yanaendelea.

Kuwajibika kwa viongozi kama Ndugai alivyofanya kwa kuamua kuutema mkate wake hadharani si ushamba bali ni uelewa mkubwa na ukomavu usio wa kawaida.

Katika hili CCM inaendelea kuonyesha ukomavu wake kwamba kuwajibika ni sehemu ya utamaduni wake kwani hakuna mwanachama aliye juu ya chama.

Katika hili vyama vingine havina budi kuendelea kuchukua somo kuliko kuendelea kufanya ushabiki usio na maana.

Ni dhahiri ndani vyama vya siasa hususan vya upinzani tumekuwa tukishuhudia migogoro mingi isiyo na mbele wala nyuma kwa sababu ‘Umungu’ mtu hutawala na wahusika hawataki kuwajibika kwa ajili ya masilahi mapana ya vyama vyao.

Ni ukweli usiopingika, vyama vya siasa visipokuwa makini na baadhi ya wanachama wao kuna uwezekano wa kujikuta viko njia panda. Badala ya kusonga mbele vinaendelea kuporomoka.

Hakika Mheshimiwa Ndugai ameonyesha njia na viongozi/wanasiasa wengine waige na kujifunza.

Javius   Byarushengo, Barua pepe: [email protected], 0756521119