Tunapoongelea upimaji ifahamike kuwa upimaji upo wa aina nyingi. Kutokana na hilo upimaji unaoongelewa hapa ni upimaji miliki. Lakini tunaongelea upimaji miliki wa ardhi mijini na siyo vijijini. 

Upimaji wa ardhi miliki ni upimaji ambao lengo lake ni kummilikisha mtu ardhi. Kummilikisha mtu ardhi siyo kumuuzia ardhi. Kummilikisha mtu ardhi ni kutambua ardhi yake kimipaka na kumpatia nyaraka mahsusi (specific) inayohusiana na umiliki (hati).

Kwa maana hii wanaomiliki ardhi ambazo hazijapimwa hatuwezi kusema wamemilikishwa ardhi. Bila kujali ardhi hizo ni za kwao na wamezinunua kwa pesa zao. Kwa kusema hivyo haimaniishi kuwa ambao hawana hati au hawajapima ardhi zao basi siyo wamiliki, hapana, isipokuwa ni kuwa tu kwamba hawajamilikishwa kisheria na mamlaka za Serikali. 

Kutokana na hilo, ardhi iliyopimwa na ile ambayo haikupimwa hutofautiana hadhi na thamani kwa kiasi kikubwa.

1. Nyaraka zinazohitajika ili upimiwe ardhi

(a) Barua kwenda kwa mkurugenzi. Anayetaka kupimiwa ardhi anatakiwa kuandika barua kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri husika. Barua ni nyaraka ya kwanza kabisa ambayo unatakiwa kuwa nayo. Ni katika barua hiyo ambamo utaeleza nia yako ya kutaka kupimiwa ardhi na matumizi ya ardhi yako kama ni makazi, kiwanda n.k.

(b) Kuambatanisha mkataba wa mauziano. Katika hatua hii mkataba wa mauziano utatambuliwa kama nyaraka ya umiliki. Mkataba huu ndiyo utakaokutambulisha kama mmiliki wa ardhi husika. Huu unaambatanishwa kwa sababu mmiliki wa ardhi ndiye mwenye jukumu la kuomba kupimiwa.

Hivyo kuambatanishwa kwa mkataba kunathibitisha kuwa mmiliki ndiye anayeomba kupimiwa kwa mujibu wa sheria. Ni vyema mkataba wa umiliki ukawa ni ule mkataba wa kisheria ulioandaliwa na kushuhudiwa na mwanasheria.

(c) Barua iliyotajwa hapo juu katika kifungu ‘a’ hakikisha ina muhuri wa mwenyekiti wa serikali za mtaa, saini pamoja na mhuri wa mtendaji. Mwenyekiti na mtendaji atakayetumika siyo wa pale unapoishi bali pale lilipo eneo unalotaka kupima.  Kama eneo lipo unapoishi basi utamtumia huyohuyo wa eneo unaloishi.

2. Hatua za kupimiwa

Hatua hizi ni muhimu kuzifahamu kwa kuwa unapokuwa katika mchakato huu, unahitaji sana kujua kazi yako imekwama wapi na kwa nani ili kama kulalamika ujue pa kuanzia.  Wanaofanya kazi za ardhi watajua namaanisha nini.

Barua niliyotaja hapo juu itawasilishwa kwa mkurugenzi wa manispaa. Barua hiyo itakuwa imeambatanishwa na nyaraka nilizotaja hapo juu. Manispaa inayotumika siyo ile unayoishi bali ni ile lilipo eneo husika. 

(a) Baada ya barua hiyo kufika kwa mkurugenzi basi huwasilishwa kitengo cha ardhi.  Kila manispaa ina kitengo cha ardhi. Hapo hushughulikiwa na afisa ardhi ambaye kazi yake kubwa itakuwa ni kuthibitisha uhalali wa umiliki wa mwombaji. 

(b) Ikitoka hapo kwa afisa ardhi inaenda mipango miji.  Afisa ardhi huipeleka kwa afisa mipango miji kwa fomu ijulikanayo kama SF 47. Kazi kubwa ya afisa mipango miji ni kutizama iwapo eneo linaloombwa kupimwa lipo katika ramani ya mipango miji. Kama limo katika ramani basi ataangalia matumizi aliyoomba mwombaji kama yanafanana na yaliyoainishwa katika ramani walizonazo.

(c) Afisa mipango miji akishathibitisha na kuhakiki basi atatuma fomu maalum SF 47 kwa afisa ardhi mteule. Huyu kazi yake ni kujaza fomu maalum SF 37 ambayo ni ya maombi ya kupimiwa ambayo ataiwasilisha kwa afisa upimaji. Atafanya hivyo kwa kuambatanisha ramani husika.

(d) Mwisho mpima ardhi atatoa maelekezo kwa mpimaji mahsusi ambaye ndiye sasa atakayefanya kazi ya kuja kufanya vipimo na utapimiwa ardhi kwa ajili ya usalama na kuipandisha thamani ardhi yako. 

Haya yote yatafanyika kwa kufuata Sheria namba 4 ya Ardhi na Kanuni zake.

 

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUBBLOG.

2271 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!