Mbowe FNi jambo la kushangaza na kusikitisha kuona wapinzani wanapokosa jambo la kuikosoa Serikali ya Awamu ya Tano, wanaanza kukosoa maneno yao wenyewe. Wanakosoa hata kile ambacho wamekuwa wakiimba muda wote kwa namna ya ‘tukipata madaraka ni lazima tufanye namna fulani’. 

Yapo madai ambayo wapinzani wameyashikilia mpaka sasa kwamba iwapo wao watapata madaraka ya kuiongoza nchi, watafanya hivi na vile, watafuta hiki na kile, wataleta hiki na kile, lakini baadhi ya mambo hayo wanayoyasema wakiona yanatendeka kwa wakati huu, kwa kufanywa na Serikali iliyo madarakani, badala ya kusema sawa Serikali imepatia wanaanza kulalamika.

Mfano, yapo madai kwamba wapinzani wakipata madaraka, kitu cha kwanza watauzima Mwenge wa Uhuru. Jambo hilo wanalisema bila ya aibu. Lakini ikitokea kwa wakati ikasemwa kwamba Mwenge usiwe unakimbizwa kila mwaka ni lazima wapinzani watakuwa wa kwanza kulalamika kwa nini inakuwa hivyo, ilmradi tu waoneshe wamepinga, ni kitu cha ajabu sana.

 Mara zote wapinzani wamekuwa wakiilalamikia Serikali kuwa inafuga uzembe, watumishi wa umma hawaelewi maana ya utumishi wao, kwamba wananchi wanahangaika kana kwamba nchi haina watumishi, maendeleo ya nchi yanakwama kwa sababu ya watumishi wa umma kukosa uzalendo. Kwamba watumishi hao wanafanya kazi kana kwamba hawalipwi mishahara na kama vile wanafanya kazi ya kujitolea na kadhalika na kadhalika.

Lengo la wapinzani lilikuwa kwamba wao wakiingia madarakani ni lazima wawafukuze au kuwaachisha kazi watumishi wote wasiokidhi viwango vya utumishi wa umma.

Jambo la kushangaza ni kwamba leo hii maneno hayo ya wapinzani yanafanyiwa kazi na Serikali isiyojibana kwenye itikadi, ikifanya kazi kwa manufaa ya umma ikiwa inatekeleza maoni yote ya wananchi yaliyo na hoja bila kujali kama yanatoka kwa wapinzani au kwa walio madarakani, wapinzani wanaanza kupiga kelele kwamba Serikali ya Magufuli imevuka mipaka!

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ameishangaza nchi kwa kile alichokichukulia kama kuikemea Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, kwamba imezidisha vipimo kwa mwendo wake wa fukuzafukuza unaoendelea kwa wakati huu nchini kote. Sielewi analolikemea na kulitetea Mbowe ni lipi hasa.

Yeye anadai kwamba operesheni hiyo inafanyika kwa kuwasimamisha kazi watumishi hao huku uchunguzi ukiagizwa kufanywa wakati tuhuma dhidi yao zikiwa zimeishatangazwa hadharani. Mpaka hapo simwelewi Mbowe anakusudia kuwaambia nini wananchi.

Ina maana mtu akituhumiwa kaua mtu anataka mtuhumiwa asikamatwe mpaka uchunguzi juu ya mauaji hayo utakapoisha? Ni kwamba mtu akituhumiwa kaua mtu jambo la kwanza ni kukamatwa na kuwekwa ndani ndipo uchunguzi unapoanza. Huwezi kusema kwa nini mtuhumiwa wa mauaji akamatwe kabla ya uchunguzi. Uchunguzi ukiisha na mtuhumiwa kuonekana hana kosa ndipo mtu huyo anapoweza kuwa huru au kuhukumiwa akibainika kafanya kweli.

Madai ya Mbowe ya kwamba mpaka sasa idadi ya watumishi zaidi ya 160 wameishafukuzwa kazi tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani sioni kama yana maana yoyote, kwa sababu nchi iliyo na idadi ya wananchi wanaokaribia milioni tano watu 160 ni idadi ndogo. Na watu wasio na ajira, tena wenye uwezo wa kuutumikia umma kwa moyo mkunjufu, wanazidi hata 1, 600,000.

Kwa hiyo, kwa nini tuwaonee huruma watu hao 160 ambao tena uwajibikaji wao una kasoro bila kuuangalia utitiri wa watu wasio na ajira?

Mbowe ana uelewa mkubwa wa kitu hicho, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inachokifanya ni kitu ambacho hata kama upinzani ungeingia madarakani ungekifanya, ila kinachomuuma ni kile ambacho amekuwa akikidai mara kwa mara kwamba Magufuli anatekeleza sera za upinzani. 

Hilo ni jambo linalonishangaza sana. Kwa nini yeye aamini kwamba Serikali ya CCM ipo kuwafanyia wananchi mambo ambayo hayafai na upinzani peke yake ndiyo uliokuwa ukiweza kuwafanyia wananchi mambo ya maana?

Jambo lolote zuri likifanywa na CCM, hata kama wapinzani walikuwa wakililalamikia sana, watageuka na kuliona baya wakisahau kwamba hata wao walikuwa wanasemea kulifanya!

Tabia hii ya wapinzani kutaka kuwaaminisha wananchi kuwa kila kinachofanywa na Serikali kinalenga kuwaonea na kuwakomoa watu inapaswa ikomeshwe mara moja. Sababu ni tabia ya kuwapotosha wananchi kwa lengo la upinzani kujitafutia mapenzi ya kulazimisha kwa wananchi, ni tabia ya kuwapotosha wananchi.

Tuseme kama Serikali iliyokuwapo ilikuwa ikifanya vizuri kwa kuwaachia watumishi wa umma wakajifanyia wanavyotaka – ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma, utumiaji mbaya wa ofisi za umma, ukosefu wa uwajibikaji na kadhalika – ina maana wapinzani walikuwa wakipinga kitu gani ambacho walidhani wangekiboresha kama wangeingia madarakani? 

Kama yanayofanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Tano yote yana dosari, ikiwa na maana ya kwamba bora yaliyopita yote yangeachwa yakabaki vilevile, kwa nini upinzani uliendelea kuwapo?

Ni kwamba upinzani ulikuwapo kwa vile ulikuwa ukiona dosari katika Serikali ya Awamu iliyopita, sasa kwa nini dosari hizo zinapofanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya sasa upinzani uanze kulalamika? Au inachukuliwa kwamba dosari zilizokuwa zikionwa na upinzani tu ndani ya Serikali, lakini zinapofanyiwa kazi na Serikali ileile upinzani unajiona kama unamalizwa?

Ni jambo la kujiuliza kwamba upinzani upo kulinda dosari ndani ya Serikali iliyopo madarakani au kutaka dosari ziishe? Na dosari zinapoisha kwa nini upinzani uanze kulalamika? Kama ilivyokuwa mwanzoni mwa Uhuru wa Tanganyika, upinzani ukiona hakipo cha kukipinga kwenye Serikali iliyo madarakani, unaweza kuamua kujiunga nayo. 

Nadhani hiyo haitakuwa dhambi ya mauti. Waingereza wanasema ‘If you cannot beat us join us’ wakiwa na maana ya kwamba kama huwezi kutushinda ni bora ukajiunga nasi.

By Jamhuri