Hayati-Baba-wa-Taifa-Julias-K.-NyerereSisi Watanzania tukubali kuwa tumependelewa sana na Mwenyezi Mungu. Kwani hatukuwahi kutawaliwa kikoloni moja kwa moja na Mwingereza kama walivyokuwa majirani zetu. Wakenya wametawaliwa kama koloni la Mwingereza, Nyasaland (Malawi) kama koloni la Mwingereza, Zambia (Northern Rhodesia) kama koloni la Mwingereza, Kongo (Kinshasa) kama koloni Ia Mbelgiji na Uganda kama mlindwa tu (protectorate) na Uingereza.

Kumbe sisi Watanzania, baada ya kufukuzwa yule mkoloni Mjerumani aliyetutawala kama koloni tukabahatika kuwekwa chini ya Umoja wa Mataifa (League of Nations) ambao uliiteua Uingereza kutawala kwa dhana ya umoja huo. Hivyo tulitawaliwa kisheria na Umoja wa Mataifa ila usimamizi ule wa karibu ulikasimiwa kwa Mwingereza. Hii ndiyo bahati nzuri hatukukandamizwa na walowezi wa Uingereza kwa vile haikuwa chini ya himaya yao moja kwa moja.

Kwa bahati namna hii ya kiutawala ndipo Mwalimu Nyerere katika andiko lake lile la ‘Barriers to Democracy (1958)’ ameandika hivi, namnukuu “of all the multi-racial countries in Africa, none has the opportunities, which Tanganyika has to establish a lasting self-governing democracy. The European community is so small and so heterogeneous, that unlike the larger and more homogenous white communities in Kenya and the Rhodesias, it can never seriously entertain hopes of dominating the non-European communities. The Asian community is a business community and could not, even if it had the desire, ever dominate the other communities. Both these communities are hardly 2% of the total population. If every non-African vote were to be magnified by law to count for ten African votes, the non-African votes would still be insignificant compared with the African votes. The African knows this, and therefore, although he has his own prejudices against the two communities, he is not afraid of them (Nyerere:

Barriers to Democracy pg 1 introductory paragraph).

Mwalimu anatetewa na Mzungu na Waasia

“He has his own prejudices but he is not afraid of them”

Jamani, mnaoujua Kiingereza, ninafikiri hili mmeshalielewa. Lakini kwa manufaa ya wasomaji wengi wasiobahatika kuijua lugha hii ya kigeni, nitajaribu pia kutafsiri hayo. 

Kwa tafsiri yangu mimi nasema hivi, Mwalimu alisema, “Katika mchanganyiko mzima wa mataifa barani Afrika hakuna nchi iliyobahatika kama Tanganyika, kuweza kuandaa Serikali ya kudumu na ya kidemokrasia ya wazawa/wananchi. Wazungu ni wachache sana na wa mataifa mbalimbali, siyo kama ilivyo kwa jirani zetu wale Kenya au Rhodesia. Basi hawakuthubutu hata kufikiria kututawala sisi watu wengi hapa nchini. Vivyo hivyo, Waasia, wao wameegemea sana kibiashara hata hawana wazo la kutawala hata kama wangetamani, lakini wao kamwe wasingaliotea kutawala hapa. Kwa ujumla wageni hao (Wazungu na Waasia) idadi yao ni ndogo hivi wala hawafiki hata asilimia 2 ya wakozi wote wa nchi hii.

Kwa hali hiyo, wakuja (wageni) wote kama wangeamua kupiga kura katika uchaguzi, mathalani tuseme kila kura ya mgeni mmoja ikakuzwa kuhesabika sawa na kura za Waafrika (sisi wananchi weusi) kumi, zisingetosha kutwaa utawala katika nchi yetu kwa mujibu wa sheria za uchaguzi (popular vote). Hili Waafrika tunalijua fika na kwa hiyo pamoja na chuki za kihisia (prejudices) kwa wageni hao, mwananchi hawaogopi asilani”. (Nimejaribu nilivyoweza kutafsiri hapa).

Hiyo ndiyo hali iliyokuwapo Tanganyika kabla ya Uhuru. Ndiyo sababu, mimi naona sisi Watanzania, licha ya kubahatika kuwa na hali iliyotupendelea kuishi kama Taifa la Amani tangu enzi za kutawaliwa chini ya udhamini wa Umoja wa Mataifa (trusteeship authority) na ndiyo sababu hatukudhurika na ukandamizwaji wa ukoloni wa walowezi wa Ulaya kama majirani zetu.

Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, Taifa zima tulitoa maombi kwa Mwenyezi Mungu, uchaguzi ule ufanyike kwa utulivu na kwa amani. Mungu ametusikiliza, hapakutokea mvunjiko wa amani wakati wote wa uchaguzi. Imekuwa tofauti na Uchaguzi Mkuu ule wa 2000 uliojaa vitisho, fujo hata umwagikaji damu. Kule Pemba, baadhi ya wananchi walipoteza maisha na wengine kukimbilia huko Pwani ya Kenya kama wakimbizi.

Mwaka jana matukio namna hil hayakutokea pamoja na ZEC Unguja kufuta matokeo ya uchaguzi ule wakati vituo vingi vilishapiga kura na matokeo kubandikwa kwenye mbao za matangazo. Licha ya usumbufu ule kule Visiwani bado nchi yetu kwa ujumla ilikuwa na amani na uchaguzi mzima ulitawaliwa na utulivu. Tunamshukuru Mungu.

Amani, tunasoma kwenye Biblia, ndilo tamko la kwanza lililotolewa na Yesu Kristo, alipofufuka na alipowatokea kwa mara ya kwanza wafuasi wake pale Yerusalemu, “….akaja Yesu akasimama katikati akawaambia “AMANI IWE KWENU” (Yon. 20:19). Hivyo tunaona salamu hii ya amani ilivyoanzia. Kutoka hapo kila mtu anaona na anajua thamani ya amani. Amani inatakiwa katika nafsi yako mwenyewe na amani inatakiwa katiko jamii unamoishi. Ndiyo sababu mimi ninaamini kila mmoja wetu hapa Tanzania ni MDAU wa AMANI. Hiyo, amani haina dini, haina rangi na wala haina itikadi ya kisiasa. Kila mmoja wetu anapenda kuishi kwa amani katika kaya yake.

Mataifa yana vikosi vya ulinzi na usalama ilimradi walinde amani katika nchi zao. Bila amani nchi yoyote haiwezi kuendelea, kwa namna yoyote ile. Waingereza wana usemi huu “if you want peace, prepare for war” yaani ukitaka amani jiandae kwa vita”. Ndiyo kusema ukiwa na zana na nguvu za kivita, utaogopwa na hivyo utaishi kwa amani-hutobughudhiwa na yeyote yule. Zana zetu kuu hapa nchini ni UMOJA, UPENDO na HAKI sawa kwa wote.

Sisi Watanzania ni mafundi wa kuimba neno amani. Je, ni kweli kila mmoja wetu anaipenda hiyo amani humu nchini? Kama sote ni wadau wa amani basi misuguano hii ya kisiasa, kejeli na kebehi zinazosikika ni za nini? Hizi ni cheche za moto wa kuvunjika kwa amani. Kupo kukamiana na kukosoana hivyo navyo siyo viashiria vya amani nchini. Sote tunataka huduma bora katika afya, elimu, miundombinu na tunataka maisha bora na kadhalika. Tufanyeje katika Taifa letu tupate hayo?

Tangu tupate Uhuru, Desemba 9, 1961 katika kila Bunge wametokea baadhi ya wabunge hawaridhiki na mfumo wa demokrasia tuliyonayo kama wana mtazamo hasi na kila kinachofanywa Serikali iliyoko madrakani kama vile wao wangeweza kufanya vizuri zaidi au ni hulka ya mtu mwenye tabia ya ukorofi. Mwelekeo hasi namna hii (negative attitude) daima kwa fikra zangu unadumaza maendeleo katika nchi. Mara kwa mara tunasikia katika Bunge, baadhi ya wenye mtazamo hasi wakibwabwaja makosa (poor negative criticisms) pengine bila hata sababu za msingi.

Hali hii mimi nasema haijengi Taifa na wala haiendelezi ile dhana ya demokrasia halisi. Mtu anakaa kuwazia kutoa makosa ya wenzake tu, kwani yeye mwenyewe yuko mkamilifu au mtimilifu? Hapa duniani hayupo mtu mtimilifu hata kidogo. Tangu ile dhambi ya babu yetu Adam pale katika Bustani ya Aden, kila mzaliwa wa Adam ana upungufu wake.

Nchi za Dunia ya Kwanza (Ulaya) kama zinavyoitwa kimaendeleo, wamepitia machungu mengi tena kwa karne kadhaa ndipo wakafikiria aina ya demokrasia wanayojivunia siku hizi. Wamepitia lie hatua kihistoria tunaita “RENAISSANCE” kule Ulaya, wakaanza kuamka lakini waliuana kweli. Ukaja wakati tunaita wa mageuzi ya viwanda “INDUSTRIAL REVOLUTION” ndiyo wakati ubeberu na ukoloni vilianza kule Ulaya. Na wakati huo ndipo walianza kutafuta mahali pa kupata malighafi kwa uendeshaji wa viwanda. 

 

>>ITAENDELEA

1526 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!