
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imewasilisha mafanikio yake makubwa yaliyopatikana kuanzia Februari 2021 hadi Machi 2025 katika kikao kilicholenga kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa majukumu ya LATRA ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za kuboresha sekta ya usafiri kwa njia ya barabara na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi kote nchini.
Akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo va habari leo Aprili 14, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Bw. Habibu Suluo ameeleza kuwa jumla ya leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, mizigo, na magari ya kukodi zimeongezeka kutoka 226,201 mwaka 2020/21 hadi kufikia 334,859 mwaka 2024/25.
“Hili ni ongezeko la leseni 108,658 sawa na asilimia 48, likiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 12 kwa mwaka” amesema.
Amesema kuwa LATRA pia imefungua ofisi ndogo 10 katika maeneo ya kimkakati, na kufanya jumla ya ofisi za LATRA kufikia 37 nchi nzima. Ofisi hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma, kutatua migogoro ya wadau, kutoa elimu, na kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za serikali ikiwemo TARURA na Serikali za Mitaa.
Katika hatua ya kuboresha usafiri wa umma mijini,Bw. Suluo amesema LATRA imeanzisha jumla ya njia mpya 1,007 za daladala jijini Dar es Salaam. Pia, imepanua njia zilizopo kufikia maeneo mapya kama Kisarawe, Bunju Sokoni, Buyuni Sokoni, na Kitonga. Maboresho haya yamepunguza gharama na usumbufu kwa abiria, huku yakichochea maendeleo ya maeneo ya pembezoni mwa jiji.
LATRA ilieleza kuwa imefanikiwa kufungua ofisi mpya katika maeneo kama Mbezi Magufuli, Tegeta, Mbagala (Dar es Salaam), Makambako, Kahama, Masasi, Ifakara, Korogwe, Same na Nzega. Pia, maandalizi ya kufungua ofisi nyingine tano yanaendelea katika maeneo ya Gongo la Mboto, Mkuranga, Chunya, Mufindi na maeneo mengine ya mikoa.
Naye Ofisa Habari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kosuri aliwashukuru wahariri na waandishi wa habari kwa kuendelea kuelimisha umma na kuripoti maendeleo ya sekta ya usafiri. “Wino wa kalamu zenu una mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa lenye mshikamano na maendeleo,” alisisitiza.
LATRA imedhamiria kuendelea kutoa huduma kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu, huku ikiendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa sekta ya usafiri nchini.




