Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimebaini kuwepo kwa mambo saba waliyoyapendekeza yaondolewe kwenye Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi 2024 pamoja na Sheria ya Masuala ya Vyama vya siasa.

LHRC kimesema miongoni mwa mambo hayo ambayo walipendekeza yaondolewe kwenye sheria hizo lakini bado yapo ni pamoja na watumishi wa umma kuendelea kuwa sehemu ya Tume pamoja na maamuzi ya tume na matokeo ya urais kutohojiwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 4, 2024 Mkurugenzi Mtendaji kituo hicho, Dkt. Anna Henga amesema miongoni mwa mambo ambayo LHRC na wadau wengi walishauri, Tume kuajiri watumishi wake yenyewe ili kuipa uhuru wa kutosha katika utekeleza wa majukumu yake na kuongeza uaminifu kwa wadau wa uchaguzi.

Amesema hata hivyo pendekezo hilo halikuchukuliwa badala yake watumishi wa umma wameendelea kuwa sehemu ya Tume.

“Mathalani, kifungu cha 6 cha Sheria imeondoa neno Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji, na kuweka neno watumishi wa umma waandamizi kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

“Pia kifungu cha 7 cha sheria kimeendelea kuwatambua Wakurugenzi wa Halmashauri kuwa maofisa uandikishaji wapiga kura, Aidha kifungu cha 8 kimeendelea kuwatambua watumishi wa umma kuwa waratibu wa uchaguzi katika ngazi za mikoa,” amesema.

Amefafanua, kwa tafsiri ya kisheria ni kwamba, Wakurugenzi wa Halmashauri kwa nafasi zao ni watumishi waandamizi wa umma hivyo licha ya kutotajwa kwa nafasi zao bado wanaweza kuwa wasimamizi wa uchaguzi suala ambalo linaendelea kutotibu wala kuleta afueni ya mifumo ya uchaguzi ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu.

Amesema katika eneo ambalo LHRC na wadau wengine wa demokrasia walipendekeza ni matumizi ya teknolojia katika mchakato wa uchaguzi kwenye hatua zote yaani uandikishaji, uchukuaji na uwasilishaji wa fomu za uteuzi wa wagombea, upigaji kura na kutangazwa kwa matokeo.

“Kwa mfano, vifungu vya 12, 16(5), 34(2) a 50(7) vya sheria tulipendekeza uandishikishaji na uwasilishwaji wa fomu za wagombea ufanyike kwa njia za kielektroniki. Hata hivyo baada ya kupitishwa kwa sheria hii tumebaini kuwa kifungu kimepitishwa kama kilivyokuwa kwenve muswada.

“Eneo lingine ni kifungu cha 166 kinachoweka takwa la matumizi ya teknolojia kuwa hiari ambapo LHRC na wadau wengine tulipendekeza matumizi ya teknolojia kwa mujibu wa kifungu cha 166 cha sheria kuwa ya lazima lakini baada ya kupitia sheria tumebaini kuwa kifungu hiki kimebaki kama kilivyo,” amesema.

Kuhusu suala la mgombea binafsi, Dkt. Henga amesema licha ya kuwepo kwa maamuzi mbalimbali ya Mahakama za ndani na za kikanda zilitoa maamuzi ya kuwepo wa mgombea binafsi lakini bado kumekuwepo na kusita kufanya maamuzi ya kurekebisha Katiba na sheria juu ya suala hilo.

“Kwa mfano Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu katika shauri Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Serikali ya Tanzania!, kwa mujibu wa Ibara ya 39(1) (c) na Ibara ya 671) ( b) pamoia na masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 1979, mtu hatakuwa mwanachama wa chama cha siasa, Sifa za kuchaguliwa kuwa Rais, Mbunge au diwani isipokuwa kama ni mwannachama wa chama cha siasa.

“Mbunge au diwani ni lazima awe anatokana na chama cha siasa, hir inathibitisha kutochukuliwa kwa maoni ya wadau tuliotaka uwepo wa mgombea binafsi, licha ya LHRC na wadau wengine kupendekeza mabadiliko madogo ya katiba Katika ibara za 67(0)(b) na 39(1)(c) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ili kuruhusu uwepo wa mgombea binafsi lakini bado Serikali haijafanyia kazi,” amesema

Amesema ni imani yao kwamba, uwepo wa mgombea binafsi utatachochea ukuaji wa demokrasia pamoja na kuongeza wigo wa watanzania kuwa na haki ya kuchaguliwa bila kulazimika kupitia mkondo wa vyama vya siasa.

Hata hivyo, amesema kwa upande mwingine, LHRC na wadau walipendekeza maamuzi ya Tume ya Uchaguzi kuhojiwa Mahakamani kwa njia za mapitio au mashauri ya kikatiba hata hivyo bado maamuzi ya tume yatakuwa ya mwisho na hayatahojiwa Mahakamani.

“Pia moja ya eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu ni vyombo vya habari kutotenda haki kwa wagombea wote kwa usawa wakati wa urushaji wa matangazo na vipindi vya kampeni.

“Kumekuwa na malalamiko kwa vyombo va habari kupendelea wagombea wa upande mmoja hii ilitokana na upungufu uliopo katika sheria zetu za uchaguzi kutokuwa na mifumo ya kuviwajibisha vyombo vya habari vinavyokiuka taratibu wakati wa kampeni,” amesema.

Kuhusu matokeo ya urais kutohojiwa mahakamani, amesema kwa mujibu wa ibara ya 41(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwapo mgombea wa kiti cha urais atatangazwa na Tume ya uchaguzi kuwa ameshinda ushindi wake hautahojiwa mahakamani.

“Tunatambua kuwa sharti hili ni la kikatiba hivyo ili kufanyiwa marekebisho ni lazima tufanye mabadiliko madogo ya katiba ili kuifanya marekebisho ibara ya 41(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ili matokeo ya Urais yaweze kuhojiwa mahakamani,” amesema

Hata hivyo amesema LHRC imebaini masuala chanya kadhaa yaliyomo katika Sheria hizo mpya ambayo ni pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa, Jiji na Wilaya kuondolewa kuwa wasimamizi wa uchaguzi ingawa wamebaki kuwa waandikishaji wa uchaguzi.

Amesema sheria pia imeweka sifa ya mtu kuwa msimamizi wa uchaguzi; (i) awe hajawahi kutiwa hatiani katika shauri la nidhamu au kosa lolote la jinai; awe hajawahi kuadhibiwa kwa kifungo kinachozidi miezi sita (6) na hajawahi kuwa kiongozi wa chama cha siasa.

“Pia sheria imefuta suala la wagombea kupita bila kupingwa katika ngazi zote (Rais, Ubunge na Madiwani), sharti la Mwenyekiti, Makamu Mwenyetiki na waiumbe wa Tume ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji Kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi kufutwa kwa sharti la kulipia ada yakupata upya kadi ya mpiga kura iliyoharibika au kupotea,” ameongeza.

Aidha ametoa wito kwa serikali kuwasilisha muswada wa sheria utakaotoa fursa ya kufanya mabadiliko ya katiba ili kuruhusu baadhi ya masuala ambayo kwa uasili wake hayawezi kufanyiwa marekebisho bila kugusa Katiba.

By Jamhuri