Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imewaelekeza walimu wa shule za msingi nchini kutowarudisha nyumbani wanafunzi ambao wazazi wao wameshindwa kuwalipia michango mbalimbali na badala yake waachwe kuendelea na masomo.

Hayo yameelezwa leo Aprili 5,2024 Jijini hapa na Waziri mwenye dhamana ya Elimu nchini Prof.Adolf Mkenda wakati akifunga Mkutano wa mwaka wa pamoja wa tathmini ya Sekta ya elimu kwa mwaka 2023/2024 uliohusisha wadau mbalimbali wa elimu kwa lengo la kujadili changamoto zilizopo kwenye Sekta hiyo na kuleta mageuzi katika elimu.

Amesema hakuna utaratibu wa kiserikali wa kumrudisha mwanafunzi nyumbani kwa kukosa michango kwa kuwa dhana ya elimu bila ada inaelekeza mtoto asinyimwe kwenda shule kwa kukosa michango na kufafanua kuwa hakuna adhabu yoyote itakayofanya mtoto akose masomo.

Waziri Mkenda amesema licha ya changamoto zilizopo kwenye Sekta hiyo,Walimu wanapaswa kuheshimiwa ili kuwafanya wanafunzi kuwa bora huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa elimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuleta mageuzi kuanzia ngazi ya chini hadi vyuo vikuu.

Kwa upande wake Kamishina wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amebainisha mambo muhimu yaliyojadiliwa katika kaikao chicho kilichowachukua muda wa siku tatu ambapo ameeleza kuwa wamejadili na kuazimia kwenda kuyafanyia kazi maeneo 10 ambayo yataleta ufanisi katika wa kisekta.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni kuboresha vikao na mikutano ya pamoja ya tathimini katika sekta ya elimu ili kuleta matokeo chanya na kuboresha mpango wa chakula na lishe mashuleni ambapo wameazimia ikiwezekana sheria itungwe ya kuwataka wazazi wachangie masuala mazima ya elimu pale inapobidi kwani bila afya akili hakuna.

Maeneo mengine ni kupeleka Sera za mitaala ili kulahisisha wadau na walimu katika utendaji kazi,kutaka elimu ya juu iakisi mabadiliko yote yalifanyika kuanzia elimu ya ngazi ya chini, bila kusahau kuimalisha ushirikiano kati ya wizara na wadau Mbalimbali wanaotoa elimu hapa nchini na nje ya nchi na kuhakikisha wanajikita katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi bila kusahau hisabati pia na kutafuta mbinu na mikakati ili kupata rasilimali kuendesha elimu.

Dkt. Mtahabwa pia ametaja eneo lingine kuwa ni maboresho ya elimu ya watu wazima ambayo mfumo wake umesahaulika , lakini pia uchangishwaji wa elimu kwa jamii.

By Jamhuri