LHRC yalaani matukio ya mauaji albino nchini

Kufuatia mauaji ya Mkazi wa Wilaya ya Kwimba jijini Mwanza Ndugu Joseph Mathias mwenye umri wa miaka (50),kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu,kwa kushirikiana na Chama Cha watu wenye Ualbino Tanzania na Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania wamepokea kwa masikitiko taarifa hizo na kulaani mauji hayo.

Aidha wameunga mkono juhudi zinazofanywa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima ambaye tayari ameshatoa siku Saba kuhakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 7,2022 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga amesema wanachukua nafasi hii kuukumbusha umma wa watanzania kwamba kwa miaka mitano, kuanzia 2015 mpaka 2020 hakukuwa na ripoti yoyote ya mauaji dhidi ya watu wenye ualbino. Hii ni baada ya juhudi za Pamoja za Jeshi la Polisi Tanzania, Asasi za kiraia, Mahakama na Tume ya Haki za binadamu nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Novemba 7,2022

“Mwaka 2021 mwezi wa 5 mkoani Tabora kulitokea mauaji ya kikatili ya mtoto mwenye ualbino mwenye umri kati ya miaka 4 mpaka 7. Mtoto huyo mwenye ualbino mwili wake uliokotwa ukiwa umekatwa kikatili viungo mbalimbali ikiwemo mikono”. Amesema

Amesema mwaka huo huo 2021 mwezi Novemba kulitokea tukio lingine Mkoani Tanga, wilayani Lushoto ambapo mwili wa marehemu Bwana Kheri Shekigenda aliyekua amezikwa katika makaburi wilayani humo ulifukuliwa na viungo vyake kuchukuliwa.

Vilevile amesema mwaka huu 2022 mwezi Aprili, kupitia kituo cha Habari cha Azam, liliripotiwa tukio lingine ambapo bwana Mohamed Rajabu mkazi wa Dar es salaam – mkazi wa Mabibo ambaye alivamiwa na kukatwa na panga na watu wasiojulikana ambapo ilielezwa na mashuhuda kuwa walidhamiria kumkata mkono.

Pia wametoa wito wao kwa Serikali na Jeshi la Polisi kuwa upelelezi ufanyike kwa wakati na watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani na kupatiwa adhabu Kali