Lipi kosa la huyu Mchina?

Tatizo letu wabongo (Watanzania) wengi tunadhani mvua inatoka juu mbinguni mawinguni kwa Mungu…hatujiulizi kwanini mvua hainyeshi jangwani au huko hakuna anga au Mungu hayupo?

Maneno haya yaliwekwa na mwenzetu kwenye kundi letu la WhatsApp. Niliyapenda kwa sababu yanatafakarisha. Ni mafupi, mepesi lakini yaliyojaa ukweli wenye ujumbe mzito.

Yakanifanya nirejee hotuba iliyotolewa na Rais wetu Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza. Kwa desturi kiongozi wetu wa nchi ndiye mhifadhi mkuu wa mazingira na rasilimali zilizomo ndani ya nchi yetu.

Rais Samia alihutubia kwa hisia kali juu ya uvamizi wa vyanzo vya maji, ukataji miti hovyo na kwa jumla uharibifu wa mazingira unaofanywa kwa, ama kutojua, au kwa jeuri na kiburi cha baadhi yetu. Kwa kumtazama na kumsikiliza, Rais wetu ni mkereketwa wa kweli wa mazingira. Tangu akiwa Makamu wa Rais alionyesha mapenzi makubwa kwenye eneo hili. Ndiyo maana chini yake tunaamini ataokoa maeneo mengi, likiwamo eneo la Loliondo na Ngorongoro kwa jumla. 

Asilimia 48 ya maji yanayoitunza Hifadhi ya Taifa ya Serengeti vyanzo vyake viko Loliondo, kwa maana hiyo hili ni eneo linalohitaji kutunzwa kwa kila hali.

Kilio cha Rais Samia kuhusu upungufu wa maji unaosababishwa na kuharibu vyanzo vya maji ni mwangwi unaotokana na mtangulizi wake, Rais John Magufuli. 

Kwa huluka ya Rais Magufuli, Mama Samia asingekuwa na namna ya kumpinga licha ya kwamba yeye (Makamu wa Rais) ndiye aliyekuwa mwenye dhamana ya kusimamia na kulinda mazingira.

Katika safu hii nilitofautiana na Rais Magufuli kwa kauli hiyo aliyoitoa akiwa mkoani Kagera, ya kuamuru wakulima walime hadi mtoni na wasibughudhiwe maana ‘wamejiajiri’. Kauli ile ilikuwa adui wa mazingira, na kwa kweli ililenga kuwafurahisha waharibifu kwa manufaa yake kisiasa.

Nilisema kwenye makala hiyo kuwa ile sheria ya kuacha buffer zone ya mita 60 kwenye mito haikuwekwa kwa bahati mbaya. 

Imewekwa kwa sababu nyingi na nzuri kama vile kulinda kingo za mito ili kutoleta mmomonyoko; lakini pia kutotiririsha kemikali za kilimo mtoni ambazo zinaweza kusababisha maafa kwa viumbe hai, wakiwamo binadamu.

Wale walioishi Dar es Salaam kwa miaka mingi waseme lini waliona milima ya mchanga kama ilivyo sasa Jangwani? 

Nawauliza tena wale wanaotuzidi umri, lini mliona magreda yakiweka kambi Jangwani kuondoa milima ya mchanga? 

Wale walioko Dakawa, lini waliona mchanga mwingi ukijaa namna ile? Yote haya yametokea baada ya ruksa ya Rais Magufuli. 

Watu wamelima hadi mitoni, watu wamechimba mchanga hadi kwenye kingo, na sasa mchanga unasafirishwa hadi baharini.

Wanaopita sasa Mto Ruaha ni mashuhuda. Mchanga umeendelea kujaa hata kusababisha baadhi ya maeneo kama pale Iyovi mto uyumbe. Kumejaa mchanga mwingi kweli kweli. Wakulima sasa wanalima hadi kwenye kingo. 

Wanakata miti kuandaa mashamba. Wanafanya hivyo kwa sababu iliagizwa waachwe walime maana wao ni wanyonge! Hii ni kama ya wamachinga.

Haya, baada ya Rais Samia juzi kuonyesha hasira zake, mara moja tumesikia anakamatwa mkulima mwenye asili ya China. 

Kosa lake nini? Hatuwataki wawekezaji? Kama maji anayochukua ni mengi, wako wapi viongozi kuanzia kitongoji hadi taifa? 

Nani amewapofusha kama si rushwa na kutojali kwetu sisi ngozi nyeusi? Nauliza, yule Mchina ana kosa gani hata akamatwe? 

Hatuhitaji wawekezaji wa mboga za  majani? Kwanini ajulikane baada ya tamko la rais? Kazi za makachero ni zipi? Kuzuia mikutano ya kisiasa tu?

Kama ni upungufu wa maji, kuna Mchina amezuia serikali isijenge mabwawa? Au ameambiwa ajenge akagoma? 

Bwawa la Mwanzugi kule Igunga lilijengwa mwaka 1967. Linafanya kazi kubwa na nzuri sana katika kilimo cha mpunga. Hao wazee wa miaka hiyo ilikuwaje wakawa na akili pana na kali kuliko kizazi chetu cha sasa?

Wanasiasa ndio sumu ya mazingira. Juzi tu tumewasikia wengine bungeni wakitaka wananchi mkoani Kilimanjaro waruhusiwe waingie kukata kuni na kufanya mambo mengine ndani ya msitu ambao ndiyo roho ya Mlima Kilimanjaro na viumbe waliomo katika eneo hilo tajiri kwa utalii. 

Fikiria, mbunge anasimama kutetea uvurugaji wa hifadhi! Nampongeza kwa dhati kabisa Askofu Dk. Shoo kwa ujasiri wa kuwakemea viongozi hao. 

Tunawahitaji kina Askofu Shoo wengi sana katika nchi yetu. Askofu Shoo ni mkweli. Hana unafiki. Neno lake na litawanyike na kupokewa kote nchini.

Ndugu zangu, wanasiasa wenye maelfu ya mifugo ndio wanaong’ang’ana kila siku serikali iruhusu mifugo ichungwe ndani ya maeneo ya hifadhi kama vile Serengeti! 

Hao viongozi kadhaa wa vyombo vya dola na umma, na wafanyabiashara ndio wenye mifugo mingi. Hao wanaodai kuwatetea ni wachungaji wao tu. Wanajulikana. 

Wanataka ng’ombe wanenepeshwe kisha wauzwe. Sehemu ya kunenepeshea waliyochagua ni hifadhini! Wamejaa tamaa na ubinafsi. Tusikubali.

Mara zote wamewashughulikia mawaziri na watendaji walioonekana kusimama imara kutetea uhifadhi. Walimwandama Waziri Hamis Kagasheki akiwa Maliasili na Utalii wakafanikiwa kumwondoa. 

Sasa wameanza kumwandama na kumtisha Waziri Dk. Ndumbaro ambaye hakuna shaka kuwa hadi sasa yumo kwenye kundi la mawaziri bora kabisa kuwahi kuongoza Maliasili na Utalii. 

Awe makini asibadilishwe tabia. Rais ana kila sababu ya kuwalinda watu wa aina hii ambao ni nadra kuwapata katika ulimwengu huu wa husuda na ghiliba.

Ndugu zangu, matumizi ya mkaa nchini ni janga kubwa mno. Ukataji miti hauendani na uhifadhi wake. Mkaa ni biashara haramu kama zilivyo biashara haramu nyingine. Uharamu wake unatokana na hasara zake ambazo ni nyingi kuliko faida.

Tumeanzisha maduka ya kuuza nyamapori sambamba na uanzishwaji wa mashamba ya wanyama. 

Kama imewezekana kwa wanyamapori kufugwa, kwanini kusiwepo mpango wa lazima wa kuhakikisha wenye mashamba ya miti ndio wenye kupata vibali vya kuuza mkaa? 

Kwanini miti ya umma ikatwe na kuchomwa mkaa kana kwamba ni mali ya watu binafsi? Kwanini faida ya mkaa wafaidi wachache, lakini athari za mazingira tuumie sote?

Hivi ni Tanzania pekee ambako mkaa ndiyo nishati ya kupikia? Mbona Zambia hakuna haya mambo? Mbona Zimbabwe hawaujui mkaa? Wanapikia nini? 

Tanzania tumefika mahali hatutaki kula wali uliopikwa kwa kutumia gesi. Tunataka unaopikwa kwa mkaa, ukaokwa na kutoa ukoko! Hatutaki kula mishikaki iliyochomwa kwenye majiko ya umeme au gesi, maana hainukii kama iliyopitishwa kwenye mkaa!

Kwanini kusiwepo kampeni ya kuhakikisha bei za gesi na vifaa vyake zinapungua ili kila kaya iwe na jiko au majiko ya gesi? Tunasubiri nchi iangamie kwa kukosa miti ndipo tuzinduke?

Kwanini tumeruhusu pikipiki zitumike kusafirisha mkaa na kuteketeza maelfu kwa maelfu ya hekta za miti? Tumeridhia kweli mkaa uwe ajira kwa kila anayetaka? 

Wakubwa hawayaoni haya mambo ya hatari? Kwanini hakuna anayejali? Kwanini tumechagua kujikomoa sisi na kukomoa kizazi kijacho?

Ushauri wangu, kulinda mazingira si kazi ya serikali pekee. Ni kazi ya kila Mtanzania anayejitambua. Muhimu katika hili ni wanasiasa kushiriki kulinda, na si kuvuruga mazingira yetu. 

Maeneo ya hifadhi yalindwe kwa mujibu wa sheria. Tusiruhusu watu waharibu mazingira na rutuba kwenye maeneo yao halafu walilie kuachiwa waingie hifadhini.

Biashara ya mkaa tuitafakari upya kwa kuja na njia mbadala, ikiwamo ya kutoa ruzuku kwenye gesi na vifaa vyake kama majiko. Kama ilivyo kwamba kila kaya iwe na choo, basi tuhakikishe kila kaya inakuwa na jiko au majiko ya gesi. Mighahawa na hoteli iwe marufuku kutumia mkaa, isipokuwa kama umezalishwa kwa sheria zitakazotambua hilo.

Taasisi kama Magereza na vyuo vikuu ambako kuna watu wengi zitumie nishati inayotokana na kinyesi cha binadamu na wanyama. 

Tukiamua, haya yanawezekana kabisa. Tusitumie umaskini au unyonge kuhalalisha matumizi ya mkaa au kuharibu mazingira. 

Hapa hapa nchini mikoa kama Iringa, Njombe na Mbeya matumizi ya mkaa ni madogo sana. Wamewezaje? Tujifunze kwao.

Maeneo ya kimila yaendelee kulindwa kwa sheria zinazotambulika. Kila Mtanzania awe mlinzi wa mazingira mahali alipo. 

Tupaze sauti kulinda hazina hii ya miti ambayo ndiyo chanzo cha maji, chakula, hewa safi na kwa jumla – uhai wa viumbe hao wote. Tukiamua tunaweza. Tuanze sasa.