Na Mwandishi Wetu, JamburiMedia, Pwani

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewasisitiza Wakuu wa Mikoa nchini kuendelea kuishikilia Ajenda ya kupambana na mmomonyoko wa maadili, vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na uwezeshaji wanawake kiuchumi katika maeneo yao.

Mhe. Dkt. Gwajima amesisitiza hayo Agosti 26, 2023 kwenye mkutano wa mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa yanayaoendelea wilayani Kibaha, mkoa wa Pwani ambapo amewasilisha afua mbalimbali zinazoratibiwa na Wizara na kutekelezwa na Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Amezieleza afua hizo kuwa ni Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, Ulinzi wa Watoto na Haki za Watoto, Uwezeshaji Wanawake na Makundi Maalum Kiuchumi ikiwemo kundi la Machinga na Mpango wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto. Nyingine ni Mpango wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi (Bottom Up) wa Mwaka 2022/23 hadi 2025/26 na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Kuhusu elimu ya Malezi na Makuzi ya Watoto wa miaka ya awali kabla ya kuanza shule ya msingi Dkt Gwajima amesisitiza Wakuu wa Mikoa kuzungumza na Wadau wa Maendeleo kwenye maeneo yao ili washirikiane kwa kasi zaidi kwenye kuanzisha huduma hiyo kwani vituo 30 vilivyojengwa na jamii na kuhudumia watoto katika mikoa ya Dar es salaam (20) na Dodoma (10) vimeonesha mafanikio makubwa.

Akifafanua changamoto ya watoto kukimbilia kuishi na kufanya kazi mitaani, kwenye majiji na miji mikubwa, Waziri Dkt. Gwajima amewaomba Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii na kuweka mifumo ambayo watoto wenye changamoto kwenye familia watachagua kukimbilia kwenye huduma za ustawi wa jamii na kupelekwa Makao ya Watoto kwa uangalizi na ufumbuzi wa changamoto zao badala ya kukimbilia mitaani ambako ni hatarishi.

Aidha, wazazi na walezi wa mtoto aliyetoweka nyumbani wakumbushwe na watakiwe kutoa taarifa Polisi kwani kukaa kimya ni kosa la utelekezaji na kumhatarisha mtoto kinyume na sheria ya mtoto.

Kuhusu uendeshaji wa Makao ya Watoto Dkt Gwajima amehimiza ufanyike ufuatiliaji wa kina kwani wako baadhi ambao wanakiuka mwongozo wa usajili na uendeshaji na kusababisha changamoto kwa watoto walio kwenye vituo hivyo.

Vilevile, Dkt.Gwajima amewasisitiza Wakuu wa Mikoa kuimarisha uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kubaini mafanikio na changamoto zao na kudhibiti yale wanaoenda kinyume na sheria ya usajili.

Akimalizia wasilisho lake, Dk. Gwajima amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuwawezesha maafisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kwani wao ndiyo timu ya ufundi katika kuleta mabadiliko ya fikra za jamii ili iweze kupokea na kutekeleza kwa tija sera na mikakati ya sekta zote.

Waziri Dkt. Gwajima ametumia nafasi hiyo kumpongeza Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki kwa kuratibu vema mkutano huo na kutoa nafasi kwa Wizara za kisekta kufanya mawasilisho ya kuelimisha na kukumbusha mamlaka za mikoa juu ya ajenda za kipaumbele

Waziri Dkt. Gwajima ametumia nafasi hiyo kumpongeza Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki kwa kuratibu vema mkutano huo na kutoa nafasi kwa Wizara za kisekta kufanya mawasilisho ya kuelimisha na kukumbusha mamlaka za mikoa juu ya ajenda za kipaumbele.

By Jamhuri