Maafisa ugani watakiwa kuwasaidia wafugaji kufuga kibiashara
 

Na Edward Kondela,JamhuriMedia

Maafisa ugani kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Mashariki wametakiwa kuhakikisha wanawasaidia wafugaji kufuga kibiashara na kuachana na ufugaji usio na tija.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Aswege Kaminyonge amebainisha hayo jana Mjini Maswa, wakati akifungua rasmi mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera na kuwataka maafisa hao kuwasaidia wafugaji kwa kuwapatia elimu ya ufugaji na kuipatia mifugo yao chanjo ili kufuga kwa tija.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe. Aswege Kaminyonge akizungumza leo (12.12.2022) Mjini Maswa, wakati akifungua rasmi mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera na kuwataka maafisa hao kuwasaidia wafugaji kwa kuwapatia elimu ya ufugaji na kuipatia mifugo yao chanjo ili kufuga kwa tija. (Picha zote na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Kaminyonge ameongeza kuwa endapo wafugaji wakielimishwa na kuhamasishwa hawana shida katika kufanya mabadiliko kwenye ufugaji bora na kibiashara kwa kuzingatia pia uogeshaji wa mifugo na kilimo cha malisho ya mifugo katika maeneo yao.

“Naona jinsi ilivyo rahisi kutoa elimu kwa wafugaji hususan kwa wafugaji ambao wanafuga kiholela bila kuzingatia matumizi bora ya ardhi, inatakiwa kila mfugaji kuwa na eneo la kufuga na kuligawa kwa malisho na mifugo yake” amesema Kaminyonge.

Aidha, amesema mifugo mingi imekuwa ikila mchanga badala ya malisho bora ambayo yanaweza kuleta tija kwa kutoa mazao bora yanayotokana na mifugo hiyo kama maziwa na nyama na kukosa ubora unaotakiwa.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi akifafanua juu ya mwendelezo wa jitihada za wizara kuwaongezea uwezo maafisa ugani ili kuwasaidia wafugaji katika kutatua changamoto zinazowakabili, ambapo amesema katika mwaka huu wa fedha wizara imepanga kuwafikia maafisa ugani 800 kote nchini. Bw. Mdachi amebainisha hayo leo (12.12.2022) katika Mji wa Maswa, Mkoani Simiyu wakati wa ufunguzi wa mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera.

Akizungumza kando ya kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi amesema mafunzo hayo yanafanyika katika kanda tano nchini ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za wizara kuwaongezea uwezo maafisa ugani ili kuwasaidia wafugaji katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Mdachi amesema mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwa awamu ya pili sasa ikiwa ni moja ya mikakati ya kuleta mabadiliko katika Sekta ya Mifugo nchini ambapo eneo linalowekewa mkazo ni kuimarisha huduma za ugani ambapo wizara kwa mwaka huu wa fedha imepanga kuwafikia maafisa ugani 800 kote nchini.

Nao baadhi ya maafisa ugani wanaoshiriki mafunzo hayo wamesema, ni wakati sasa kwa wao kuwasaidia zaidi wafugaji namna ya kufuga kibiashara pia namna ya kutokomeza magonjwa ya mifugo ambayo yamekuwa yakiathiri shughuli zao.

Wamebainisha kuwa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi yatakuwa na tija kwao kwa kuwa watajifunza mambo mengi kulingana na mabadiliko ya tabia ya nchi hali ambayo pia inaweza kuwasaidia wafugaji.

Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Danietha Tindamanyere akizungumzia mpango wa mabadiliko ya Sekta ya Mifugo na maboresho ya Sera ya Mifugo wakati wa siku ya kwanza ya mafunzo rejea kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka Kanda ya Ziwa Mashariki inayohusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera. Mafunzo haya ya siku mbili yanafanyika katika Mji wa Maswa, Mkoani Simiyu.
Afisa Mifugo Msaidizi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Sebastian Shilangalila akifafanua kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka Kanda ya Ziwa Mashariki inayohusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, juu ya matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ugani kwa maana ya M-Kilimo na Ugani Kiganjani. Mafunzo haya ya siku mbili yanafanyika katika Mji wa Maswa, Mkoani Simiyu.
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe. Aswege Kaminyonge baada ya kufungua mafunzo rejea ya siku mbili kwa maafisa ugani kutoka Kanda ya Ziwa Mashariki inayohusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, mafunzo haya yameandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo yanafanyika katika awamu ya pili kwenye kanda tano nchini. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)