Nimeandika mara kadhaa na kusisitiza kuwa Katibu wa Baraza la Ardhi la kata si mjumbe wa baraza hilo. Kwa sababu si mjumbe, hivyo ni kosa kubwa kumhesabu kama mjumbe. Kwa wasiojua lolote kuhusu Baraza la Ardhi la Kata ninaongelea chombo kilichoundwa kisheria ambacho kipo kila kata na kazi yake kubwa ikiwa ni kupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu migogoro midogo ya ardhi iliyo katika ngazi ya kata. Ni kama mahakama ya mwanzo katika migogoro ya ardhi.

Wajumbe tunaozungumzia hapa ni wale wanaokaa kusikiliza na kutolea uamuzi kuhusu migogoro hiyo ya ardhi. Hawa ni kama mahakimu. Kwa hiyo, kumjumuisha katibu kama mjumbe ni sawa na kumjumuisha miongoni mwa mahakimu. Ninaposema kuwa ni kosa kumhesabu katibu kama mjumbe ninamaanisha kuwa ni kosa kumhesabu katibu kama sehemu ya mahakimu.

Tukirudi kwenye mada, Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata, Sura ya 206 kinasema kuwa kila Baraza litaundwa na wajumbe wasiopungua wanne na wasiozidi wanane, ambao watachaguliwa na kamati ya kata kutoka katika orodha ya wakazi wa kata husika.

Maana yake ni kuwa kila baraza linapokaa kusikiliza mgogoro ni lazima wajumbe (mahakimu) wanaokaa kusikiliza wawe si chini ya wanne, ila wasizidi wanane. Ikiwa ni hivyo, maana yake akidi imetimia na usikilizwaji wa shauri hilo umefanyika kihalali. Akidi hii ikiwa pungufu au ikizidi, basi usikilizwaji wa shauri ni batili.

Tatizo linalokuja na linalotokea mara kwa mara ni kitendo cha wajumbe hawa kumhesabu na katibu kuwa sehemu ya akidi yao. Kwa maana kuwa unakuta wajumbe ni watatu halafu na katibu wanamhesabu wa nne, na kwa kufanya hivyo wanadhani akidi imetimia, wanaendelea kusikiliza shauri.

Ni hivi; shauri lolote la ardhi ngazi ya kata ambalo katibu atahesabika kama mjumbe na likasikilizwa, shauri hilo ni batili. Na ndiyo maana hapo juu kwenye kichwa, nikaandika mabaraza yaache kuharibu kesi za watu. Hii ni kwa kuwa kesi ikiamuliwa kwa akidi hiyo ni lazima ikienda rufaa katika Baraza la Ardhi la Wilaya, Mahakama Kuu, au Mahakama ya Rufaa, itafutwa tu. Mnakuwa mmepoteza muda mwingi wa watu na gharama zao.

Kwa msingi huu, tuelimishane tena kuwa Katibu wa Baraza la Ardhi la Kata asihesabike kabisa kama mjumbe anayepaswa kusikiliza shauri (kesi). Katibu yeye ni katibu na mjumbe ni mjumbe. Kifungu cha 4 (2) cha Sheria hiyo ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata kinamtaja Katibu kuwa mtu anayeteuliwa na mamlaka za Serikali za Mitaa baada ya kuwasiliana na Kamati ya Kata.

Tofauti za wazi kati ya katibu na wajumbe ni kuwa, katibu kazi yake ni kuchukua kumbukumbu wakati shauri linapokuwa linasikilizwa, yaani kuandika kila kinachosemwa. Wakati wajumbe ni kusikiliza shauri na kutoa uamuzi.  Tofauti nyingine, mjumbe lazima awe mkazi wa kata husika, wakati si lazima kwa katibu kuwa mkazi wa kata husika.

Katika kesi ya ADELINA KOKU ANIFA na JOANITHA SIKUZANI ANIFA vs BYARUGABA ALEX, kesi namba 46/2019 Mahakama ya Rufaa chini ya majaji watatu walifuta shauri  kwa sababu wajumbe waliosikiliza shauri walikuwa watatu na walimhesabu katibu kuwa mjumbe wa nne, hivyo kumwingiza kwenye akidi.

Rai yangu kwa wajumbe, hasa wenyeviti wa haya mabaraza, ni lazima wazingatie jambo hili ili kuepuka kuwapotezea muda wananchi. Mashauri yenu mengi mnayoamua yanafutwa na kubatilishwa kwenye rufaa kwa sababu hii. Chonde msipoteze muda wa watu.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea  SHERIA  YAKUB BLOG.

By Jamhuri