Bunge la Burundi limepitisha sheria itakayoidhinisha malipo kwa Rais Pierre Nkurunziza ya dola za Marekani 530,000 (Sh bilioni 1.22) na kumjengea kasri atakapostaafu, pamoja na posho anayopata mbunge.

Wapo watakaoshangaa ukubwa wa mafao hayo, lakini wapo wanaoona kuwa malipo hayo yanaweza kuwa suluhisho la mlolongo wa mivutano ya muda mrefu ya kisiasa nchini Burundi.
Kwamba, kama sheria hiyo inampa rais mstaafu nyenzo za kuishi vizuri nje ya serikali, basi ni mzigo halali kabisa ambao taifa la Burundi linapaswa kuubeba.
Burundi ilibadilisha katiba mwaka 2018 kumruhusu Rais Nkurunziza kugombea, na anaweza kubaki madarakani hadi mwaka 2034. Kupitishwa kwa sheria hii ni ishara kuwa Rais Nkurunziza ameamua kung’atuka na hana nia ya kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Mei mwaka huu.
Ya Burundi hutayashangaa kama umesikia ya Angola. Isabel dos Santos, binti wa rais mstaafu wa Angola, Jose Eduardo dos Santos, anakabiliwa na tuhuma za ufisadi wa thamani ya mamilioni ya dola za Marekani, ambayo ni pamoja na utakatishaji pesa, kutumia vibaya wadhifa wake, kughushi nyaraka na tuhuma nyingine kadhaa za fedha.
Isabel anakadiriwa kuwa na utajiri wa thamani ya dola bilioni mbili za Marekani, utajiri ambao inadaiwa umetokana na ushawishi wa familia yake, kinga na upendeleo aliopewa na serikali ya baba yake. Rais dos Santos aliongoza Angola kwa miaka 38. Isabel anakanusha tuhuma zote na anadai kuwa anaandamwa kisiasa.
Rais Joao Lourenco wa Angola anaendesha kampeni dhidi ya ufisadi ambayo inamhusisha rais mstaafu Dos Santos na watu waliokuwa karibu naye. Inakadiriwa zaidi ya dola bilioni 30 za Marekani zimeporwa kutoka Angola wakati wa utawala wa Dos Santos.
Kwa kuwa bado ni tuhuma, hatuwezi kukurupuka na kuanza kutoa hukumu, lakini ni muhimu kusema kuwa ni shutuma ambazo zimeibuliwa na waandishi wa habari mahiri wanaoaminika kuheshimu kanuni za utafiti na utoaji wa taarifa. Hawa si kanjanja, ni watu wanaofuata misingi ya taaluma yao.
Lakini si vibaya kutoa maoni ambayo ningeyatoa kama Isabel atakutwa na hatia.
Naanza na historia. Waafrika wote ambao nchi zao zilikuwa huru siku viongozi wa nchi walipokutana Addis Ababa kuunda Umoja wa Nchi Huru za Afrika Mei 25, 1963 ni wadau wakuu wa ustawi wa Afrika, na wanayo haki ya kudai kuwa rasilimali za nchi zote za Afrika zilizokombolewa baada ya tarehe hiyo zitumike kwa manufaa ya raia wa nchi hizo na si kunufaisha kundi dogo la watu ambao inaelekea wanasahau kilichoamuliwa Addis Ababa.
Umoja wa Nchi Huru za Afrika ulipitisha uamuzi sahihi kabisa wa kuunga mkono mapambano ya kukomboa Waafrika waliobaki kwenye utawala wa wakoloni wa Ureno na maeneo ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini.
Kuna Watanzania wengi katika mikoa ya kusini ambao walikufa kwa sababu ya mashambulizi ya majeshi ya Ureno wakati wa mapambano yale. Ni maelfu kwa maelfu waliokufa wakipigania Uhuru wa Angola. Tuhuma za Angola zikithibitishwa kitakuwa ni kitendo cha usaliti mkubwa kwa Waafrika wote.

Nimesimuliwa na Mama Maria Nyerere ni jinsi gani siku moja, katika miaka ya sitini, ambapo alishuhudia Mwalimu Nyerere akikesha usiku akisumbuliwa na jambo fulani.
Siku kadhaa baadaye walifika wageni wanne nyumbani Msasani akawatambulisha kwake. Mmoja alikuwa Samora Machel, mmoja wa waasisi wa mapambano dhidi ya utawala wa Ureno nchini Msumbiji. Hawakumbuki wengine lakini anahisi mmoja wao alitokea Angola. Wote walifika Tanzania kujiunga na mapambano ya ukombozi wa nchi zao.
Kilichomkosesha usingizi Mwalimu ni kupokea taarifa ya kukamatwa kwao kwenye mpaka wa nchi moja ya Afrika, na wangerudishwa kwenye nchi walizokimbia kama Serikali ya Tanganyika isingetuma ujumbe kusema waachiliwe, ni “watu wetu.”
Waafrika wote wana haki ya kuona kuwa nchi walizosaidia kukomboa zinaongozwa kwa misingi imara ya utawala bora. Sina hakika angepatikana hata Mwafrika mmoja kuunga mkono ukombozi kama matokeo yake yangejulikana kuwa ni uporaji wa rasilimali za nchi zilizokombolewa, na kuacha umati wa raia wa nchi hizo wakitapatapa kwenye umaskini.
Kila mwaka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) hukutana kuweka mikakati na miradi ya maendeleo kwa nchi zao. Angola nayo ni mwanachama wa SADC.
SADC inayo itifaki nzuri ya mikakati ya kuzuia, kubaini, kuadhibu na kufuta rushwa na ufisadi kwenye sekta ya umma na sekta binafsi. Sina hakika itifaki hiyo ina nguvu kiasi gani inapojitokeza kuwa viongozi wanaopaswa kusimamia utekelezwaji wake ndio wao wanaotuhumiwa kuwa vinara wa rushwa na ufisadi.

Itakuwa ajabu kama raia wa nchi wanachama tunahimizwa kuunga mkono utangamano wa nchi wanachama za SADC wakati hakuna taratibu madhubuti za kuwawajibisha viongozi ambao tumewapa imani kutuongoza.

Utajiri si dhambi. Tatizo ni jinsi gani viongozi wetu wanatajirika. Kwa yanayotokea Angola, ya Burundi ni sawa kabisa.

Hatimaye, Waafrika wanalazimika kuzinduka na kutambua kuwa ulinzi wa masilahi yao utatokana na wao wenyewe.

barua pepe: barua.muhunda@gmail.com

405 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!