Familia ni miongoni mwa maneno ambayo hakuna muafaka wa fasili yake. Kiujumla, familia ni kundi la watu wanaokaa pamoja kama baba, mama na watoto. 

Kikundi hiki mara nyingi ni sehemu ya kundi kubwa zaidi la ukoo unaounganisha watu wenye asili katika uzazi wa pamoja. Familia zinatofautiana duniani kutokana na utamaduni na hali ya jamii. Katika nchi nyingi za Afrika; familia ndogo ya baba, mama na watoto (Nuclear Family),   kwa kawaida ni sehemu tu ya familia kubwa zaidi (Extended Family) pamoja na ndugu wa baba na mama, akina babu na bibi na kadhalika. 

Lakini hata Afrika kuna taratibu tofautitofauti kama ni ndugu wa baba au ndugu wa mama wanaotazamiwa kuwa karibu zaidi kwa watoto wa familia ndogo. Vilevile kuna tofauti kama muundo wa kawaida ni mume mmoja na wake wengi na kila mmoja akiwa na watoto wake. Hata hivyo, kwa muktadha wa makala hii, familia ni wale wenye uhusiano wa karibu zaidi na wewe kuliko wengine miongoni mwa wanafamilia na ambao wewe ni mkata shauri juu ya mambo yao.

Anuani ya makala yetu inamtaka Muislamu, baada ya kujitathmini yeye mwenyewe ni kwa kiwango gani yeye ni Muislamu, aitupie jicho familia yake na kuitathmini ni kwa kiwango gani imekuwa ni familia ya Kiislamu yenye kutekeleza kwa kauli na vitendo yale yanayoamrishwa na Uislamu na kuyaacha yale yanayokatazwa na Uislamu. Anapaswa afanye hivyo kwa sababu yeye ni mchungaji atakayeulizwa na Mola wake Siku ya Kiyama juu ya wale aliopewa dhamana ya kuwachunga.

Tunasoma katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Umar’ (Allaah Amridhie) kwamba Mtume Muhammad (Allah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Nyote ni wachunga na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga. Kiongozi ni mchunga, na mume ni mchunga juu ya mkewe na mke ni mchunga juu ya nyumba ya mumewe na watoto wake. Kwa hivyo, nyote ni wachunga na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga.” (Hadithi hii inapatikana katika Vitabu vya Hadithi za Mtume, Sahih Al-Bukhary na Sahih Muslim).

Katika kusisitiza juu ya utekelezaji wa jukumu hili adhimu tunasoma katika Qur’aan Aya mbili; moja ikisisitiza umuhimu wa mtu kuinusuru familia yake na adhabu ya moto aliouandaa Mwenyezi Mungu kwa watu waovu, na nyingine ikionyesha umuhimu wa kuiongoza familia kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu ili ipate radhi zake na Siku ya Kiyama inusurike na moto na izawadiwe pepo.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 66 (Surat At-Tahriim) Aya ya 6 kuwa: “Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali (familia) zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa.”

Tunaona hapa jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anajilinda yeye mwenyewe na kuilinda familia yake na adhabu ya moto wa Mwenyezi Mungu.

Tunasoma pia katika Qur’aan Tukufu Sura ya 20 (Surat Twaa-Haa) Aya ya 132 kuwa: “Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mcha-Mungu.”

Hapa tunaona msisitizo kwa familia kutekeleza Ibada ya Swala ambayo ni ibada kubwa sana ambayo hakuna udhuru wa kutoitekeleza isipokuwa kwa kupitiwa na usingizi au kusahau, kwa maana ya kusahau, na si kujisahaulisha au kupuuza utekelezaji wake ndani ya wakati. 

Ni ibada yenye nyakati maalumu ambayo hata mgonjwa hana udhuru wa kuiacha muda wa kuwa ana akili timamu; anatakiwa aitekeleze kwa hali yoyote awezavyo; kwa kusimama, kukaa, kulala kwa ubavu wa kulia; kwa kuleta nguzo za Swala kwa vitendo au hata kuvileta kwa kuashiria au kuvileta mawazoni, ili mradi hakuna sababu yoyote ya kutotekeleza Ibada ya Swala kwa Muislamu mwenye akili timamu na msafi (Hili la usafi hapa ni maalumu kwa wanawake na wanalijua vizuri maana yake).

Swali la kujiuliza: Wanaotangaza kuwa wao ni Waislamu wanatekeleza Ibada ya Swala? Ni dhahiri na kwa utafiti wa wazi kuwa asilimia chache sana ya wanaotangaza kuwa wao ni Waislamu wanatekeleza Ibada ya Swala. Huamini? Jiulize, katika familia yako wangapi wanatekeleza Ibada ya Swala? Unapotoka alfajiri kwenda msikitini ni wangapi unawaacha wakiasi kuswali?

Siku moja nilimstaajabu mtu anayeshangaa kuwa katika nchi moja huko ughaibuni Waislamu imewalazimu kukaa foleni kusubiri zamu yao ya kuswali baada ya msikiti kujaa pomoni. Nilimwambia mtu yule kuwa katika mji ule Waislamu ni wachache sana lakini wengi wao wanatekeleza Ibada ya Swala na wana msikiti mmoja mdogo usiowatosha na ndiyo sababu wanaswali kwa zamu. 

Nikamwambia na huu ni ushahidi tosha kuwa wanaotangaza kuwa Waislamu nchini Tanzania asilimia kubwa hawatekelezi Ibada ya Swala na lau wangetekeleza kwa wingi wao na ufinyu wa nafasi katika misikiti yetu, basi jamaa za kusubiriana zingeunganisha Swala moja na nyingine, ukiiondoa Swala ya Ishaa na Swala ya Asubuhi.

Ni wazi kuwa wakuu wa familia za Kiislamu hawaitekelezi amri ya Mwenyezi Mungu inayowataka kuziamrisha familia zao, na si kuziomba na kuzibembeleza, kutekeleza Ibada ya Swala.

Katika mafundisho ya Mtume Muhammad anamtaka mzazi kumuamrisha mtoto kutekeleza Ibada ya Swala pale anapofika umri wa miaka saba na ampige (kipigo cha kumuadabisha ili atii bila shuruti, si cha kuua nyoka) kwa kuacha Swala afikapo umri wa miaka kumi.

Tunasoma katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa ‘Amri bin Shuayb (Allaah Amridhie) naye akiipokea kutoka kwa baba yake, naye akiipokea kutoka kwa babu yake (‘Amri) kwamba Mtume Muhammad amesema: “Waamrisheni watoto wenu kuswali wakifikisha miaka saba na waadhibuni (wapigeni) kwa kuiacha hiyo swala wakifikisha miaka kumi na watenganisheni katika vitanda (katika kulala).” (Hadithi hii inapatikana katika Vitabu vya Hadithi za Mtume, Sunanu Abi Dauud na Musnad Ahmad).

Unaweza kujiuliza kwa nini mtoto huyu aanze kuamrishwa kuswali afikapo umri wa miaka saba? Kwa nini aadhibiwe kwa kupigwa afikapo miaka kumi? Kuna nini katika namba saba na kumi? Bila ya kuvutwa na Mwanazuoni wa Kiswisi katika Bailojia na Saikolojia, Jean Piaget (1896 – 1980), juu ya hatua nne za makuzi ya akili, tunaona dhahiri kuwa Uislamu umetangulia kuonyesha hatua ya ukuzi wa akili ya mtoto kufikia kufikiri mawazo ya kufikirika (abstract thinking) na hapo ibada ya msingi ya kuzoeshwa nayo ili imuingie na iwe vigumu kwake kuiacha hapo baadaye ni Ibada ya Swala.

Kwa nini Swala? Swala ni Ibada yenye athari chanya ya kumzuia mwenye kuitekeleza kwa dhati kufanya maovu na machafu. Yaani, kipimo cha Muislamu kujipima kama Ibada ya Swala anayoitekeleza ina athari chanya kwake ni kujiangalia ni kwa namna gani amekuwa mbali na maovu na machafu. Vinginevyo, Ibada ya Swala kwake ni sawa na mazoezi ya viungo.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 29 (Surat Al-Ankaboot) Aya ya 45 kuwa: “Soma uliyofunuliwa katika Kitabu, na ushike Swala. Hakika Swala inazuia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyatenda.”

Makala yetu letu imeiangazia familia ya wanaotangaza kuwa Waislamu kwa kipengele kimoja tu cha kutekeleza Ibada ya Swala na bila shaka sote tunakubaliana kuwa asilimia kubwa ya wanaotangaza kuwa wao ni Waislamu hawatekelezi Ibada ya Swala na kwamba familia nyingi zinazotambulika kuwa za Kiislamu hazitambuliki hivyo kwa kigezo cha kuishi Kiislamu au kutekeleza Ibada ya Swala ambayo ndiyo alama nyepesi kabisa ya kumtambua Muislamu anayefanya juhudi ya kuishi Kiislamu.

Kwani ni Swala ambayo itamzuia kufanya maovu na machafu ikiwemo kutumia ulevi, kuzini, kucheza kamari, wizi na ufisadi, kutoa na kupokea rushwa, kuishi vibaya na majirani na kuamiliana vibaya na viumbe wengine wakiwemo binadamu, wanyama, ndege na mazingira yote kwa ujumla.

Swala ikitekelezwa inavyopaswa itamuhakikishia mwenye kuswali kufaulu kesho Siku ya Kiyama kama tunavyojifunza kutoka katika mafundisho ya Mtume Muhammad kuwa Swala ndiyo ya kwanza kuhesabiwa Siku ya Kiyama katika matendo ya mja, ikitengemaa yatatengemaa mengine na isipotengemaa hayatatengemaa mengine.

Nirudie kukumbusha kuwa Uislamu wa mtu yeyote hauangaliwi kwa kuwa na jina la Kiarabu wala kuvaa kanzu na baraghashia kwani hayo yote hayana nafasi katika Uislamu na imani ya mtu, hata nasaba yako kwa wazazi Waislamu wacha-Mungu haina nafasi ya kukuokoa, ukizingatia kuangamia kwa mtoto wa Nabii Nuhu pamoja na baba yake kumbembeleza kuingia kwenye safina.

Uislamu wako ni namna wewe unavyojenga uhusiano mwema na Mola wako kwa kufanya uliyoamrishwa kuyafanya na kuacha uliyokatazwa, huku ukijenga uhusiano mwema na viumbe wenzako wakiwemo wanadamu, wanyama na mazingira kwa ujumla ili usiingizwe katika orodha ya watakaotangazwa kufilisiwa Siku ya Kiyama kwa kutojipamba na tabia njema.

Shime, tujiokoe na tuziokoe familia zetu na adhabu ya moto na tuhimizane Swala!

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata). 

Simu: 0713603050/0754603050

By Jamhuri