Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Watu wawili wamefariki dunia na wengine watano wamejeruhiwa ,katika ajali iliyohusisha magari matatu likiweno bus kampuni la abiria New Force,Sauli na lori la mafuta kuteketea kwa moto alfajir ya Machi 28 eneo la Ruvu, Mlandizi ,mkoani Pwani.

Kati ya watano waliojeruhiwa ni pamoja na askari wawili wa Jeshi la Zimamoto ambao wamejeruhiwa wakati wakiwa watatekeleza majukumu yao ya uokoaji.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Ameeleza ,katika barabara ya Morogoro Dar es Salaam gari namba T 668 DTF aina ya scania kampuni ya Sauli ikiendeshwa na Iddi Aloyce (35) mkazi wa Mafinga likitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya liligonga ubavuni lori la mafuta ya petrol lenye namba za usajili RAF672N na tela lenye namba RL2594 aina ya Howo lililokuwa linatoka Dar kwenda Rwanda likiendeshwa a Mushimana Musiyimana lililokuwa limesimama kupisha gari lililokuwa linakuja mbele yake .

Aidha basi hilo lilikuwa limeongozana na basi la Golden Deer Kampuni ya New Force lenye namba za usajili T175 DZU likiendeshwa na Burton Jacob (33), mkazi wa Mbeya ambapo nalo liligonga kwa nyuma bus la Saul lililokuwa mbele na kusababisha vifo.

Lutumo alisema, watu waliofariki bado hawajafahamika majina yao na waliojeruhiwa watatu ni Salim Daud (50) mkazi wa Mbozi,Farida Idrisa (26) mkazi wa Tabata na Kiambile Geoffrey mkazi WA Uyole Mbeya .

“Baada ya ajali hiyo Jeshi la Polisi wakiwa na jeshi la zimamoto na uokoaji wakiwa katika harakati za kuwatoa marehemu waliokuwa wamenasia kwenye gari ghafla magari yaliwaka moto uliotokana na petrol iliyokuwa inavuja toka kwenye tenki la mafuta.”

“Jeshi la zimamoto na uokoaji lilifanikiwa kudhibiti moto huo na kuwatoa marehemu ambao nao walikuwa wameteketea kwa moto kwa mara nyingine moto ulilipuka tena toka kwenye moja ya chumba cha tenki la mafuta “

“Mlipuko huo ulisababisha majeraha kwa askari wawili wa Jeshi la zimamoto na uokoaji ambao ni Koplo Hamis Kungwi na Koplo Elias Bwire ambao walikimbizwa hospital ya Mloganzila kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri “alieleza Lutumo.

Lutumo alieleza, chanzo cha ajali ni uzembe wa madereva wa mabasi yote mawili kushindwa kuchukua tahadhari kwa kuyapita magari mengine lakini pia kushindwa kutunza umbali kati ya gari moja na lingine yakiwa yanafuatana.

Alisema, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya injini ya basi la Saul iliyokuwa imekita chini baada ya kugonga gari lingine na kulipua petrol wakati wa uokoaji.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani,alhaj Abubakar Kunenge alitoa wito kwa madereva kutiii sheria za usalama wa barabarani na ambae atakiuka mkoa hautosita kuyazuia magari hayo yasipite barabara za mkoa huo.

Aliwaasa wananchi waache tabia za kuhatarisha maisha yao wakati ajali zinazohusisha milipuko ya mafuta kukimbilia kwani ni hatari kwao.

Kunenge aliwataka pia watumiaji wa barabara wazingatie sheria za usalama wa barabarani.

Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi Jennifer Shirima alisema wakifika kwa wakati katika ajali hiyo na kufanikiwa kudhibiti moto na kuokoa .

Shirima alieleza askari wawili wa Jeshi la zimamoto walipata majeraha wakati wakitekeleza majukumu yao ya uokoaji mchana ambapo ulitokea mlipuko wa pili.

Alifafanua kwamba , askari hao wanapatiwa matibabu hospital Mloganzila -Muhas na wanaendelea vizuri.