Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ilemela

Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wametakiwa kutekeleza wajibu wao kwa kufanya mikutano ya hadhara, kusoma mapato na matumizi pamoja na kutatua kero za wananchi.

Rai hiyo imetolewa na mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula wakati wa kikao chake na wenyeviti wa mitaa 171 iliyopo ndani ya Wilaya ya Ilemela kilichofanyika katika ukumbi mpya wa jengo la utawala la manispaa hiyo ambapo amewataka kutimiza wjibu wao wa kuhudumia wananchi na kutatua kero zinazowakabili na zile wanazoshindwa kuzipatia ufumbuzi kuziwasilisha ngazi ya juu yao.

‘.. Kuna wenyeviti hawasomi hata taarifa za mapato na matumizi na hawafanyi mikutano ya hadhara Kwa wananchi, wengine wanakwamisha wananchi kuchangia shughuli za maendeleo hata wale wanaojitokeza kwa hiari yao wenyewe, hii si sawa ..’ amesema.

Aidha Dkt. Mabula amemshukuru Rais Mhe Dkt.Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya jimbo lake pamoja na kumuamini kuwa Waziri wa Wizara ya Ardhi kwa kipindi cha miaka nane.

Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Bahebe Mulunga mbali na kumshukuru mbunge kwa kusukuma shughuli za maendeleo amewataka wananchi kuendelea kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu Hasan na kuunga mkono shughuli za maendeleo.

Nae Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Wakili Mariam Abubakar Msengi ameahidi kuendelea kuzisimamia fedha za maendeleo zinaletwa ndani ya wilaya hiyo kwa ajili ya maendeleo sanjari na kuwapongeza Rais Dkt. Samia na mbunge Dkt. Mabula.

Hasan Milanga ni Katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela yeye ameahidi kuwalinda viongozi wa wilaya hiyo waliopo madarakani dhidi ya watia hofu na wakwamisha maendeleo wanaoanza kampeni kabla ya wakati na kuwasema vibaya viongozi waliopo madarakani wakiwemo wenyeviti wa Serikali za Mitaa, madiwani na mbunge.

Akihitimisha Mwenyekiti wa Mtaa wa Bulola A, Elias Malipesa mbali na kumshukuru Kwa kikao hicho ameiomba mamlaka ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuweka matuta katika barabara ya Mecco ili kupunguza na kuzuia ajali zinazojitokeza mara kwa mara.

By Jamhuri