Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Dkt. Angeline Mabula amewataka wanawake kujiamini na kutumia fursa mbalimbali zinazowazunguka ili kujiimarisha kiuchumi badala ya kuendelea kulalamika kukwamishwa na mfumo dume.

Waziri Dkt. Mabula ameyasema hayo Oktoba 16, 2022 jijini Mwanza wakati akifungua kongamano la Jukwaa la Wanawake Viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kuongeza kuwa suala la mfumo dume nchini si changamoto kwani tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameliondoa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Dkt. Angeline Mabula akizungumza kwenye kongamano hilo. Waliokaa kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Antony Mavunde, Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SCCULT) Dkt. Cuthbert Msuya.

“Hamtakiwi kuwa wanyonge tena, mjiamini kwani hakuna mfumo dume kwa sasa, wanawake tunaweza na hilo limedhihirishwa na Rais wetu Mhe. Rais Samia, ndiyo maana baada ya kuingia madarakani amepata tuzo mbalimbali kutokana na uchapaji kazi wake” amesisitiza Waziri Dkt. Mabula.

Aidha alisema Rais Samia ameendelea kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, akitolea mfano jijini Mwanza ambapo alisema soko kuu la Mwanza na Kirumba yatachochea fursa za kiuchumi kwa wananchi hususani wanawake ambao ni wengi masokoni.

Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akitoa salamu kwenye kongamano hilo.

Pia Dkt. Mabula amewahimiza wanawake hao viongozi kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo za uzalishaji mali na kimafunzo na kisha kuwashirikisha wanawake wenzao kupitia vyama vya ushirika ili kusonga mbele kwa pamoja huku akiwahimiza kuwa tayari kuipokea sheria mpya ya bima ya afya kwa wote itakayorahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya.

“Mkawe mabalozi wazuri wa kuelimisha wenzenu kuhusu bima ya afya kwa wote kwani kama huna uhakika wa afya yako, hutaweza kunufaika na fursa mbalimbali za uzalishaji mali. Kumbuka mlio hapa ni viongozi, mmeaminiwa na waliowachagua hivyo usifurahie tu kuwa kiongozi, bali kipindi chako kikiisha uwe umeacha alama” alidokeza Waziri Dkt. Mabula.

Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Antony Mavunde ametumia kongamano hilo kuwahimiza wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali akisema kwa sasa mpango uliopo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 nchi ijitosheleze kwa uzalishaji wa sukari na mafuta ya kula hivyo angetamani kuona wanawake wanachangamka kwa kuanzisha viwanda vidogo.

Naye Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege alisema changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakumba wanawake ni mitaji ya uhakika kwa ajili ya kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na hivyo kuwahimiza kutumia kongamano hilo kuweka mikakati ya pamoja ya kusonga mbele na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo iko tayari kuwasimamia.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Viongozi wa SACCOS, Monica Komba alisema awali wanawake waliathiriwa na kutojiamini kutokana na mfumo dume uliokuwa ukiwanyima fursa mbalimbali za kiuchumi lakini kupitia jukwaa hilo kumekuwa na mabadiliko makubwa ambapo kwa sasa wanashiriki shughuli mbalimbali na hivyo kuondokana na utegemezi.

Kongamano hilo limeambatana na kauli mbiu ya siku ya kimataifa ya ushirika inayoadhimishwa Oktoba 17, 2022 isemayo “Imarisha uwezo wako wa kifedha kwa siku zijazo kupitia ushirika wa akiba na mikopo”.