Nimepata kumsikia kiongozi mmoja wa siasa nchini akisema kuwa yanayotekelezwa na Rais John Pombe Magufuli kuhusu kudhibiti wizi na utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi, ni msimamo wake na ni ajenda ya chama chake cha siasa, ingawa chama chake hakiko madarakani.

Kauli hiyo ina utasi kwa Mtanzania aliye makini na aliyefuatilia kindakindaki kwa kusoma na kusikiliza ILANI za vyama vya siasa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, uliyofanyika hapa nchini. Naamini atakuwa na jibu sahihi katika kauli hiyo.
Binafsi, natambua kila chama kilikuwa na Ilani yake na mgombea wake wa urais ambaye alilazimika kunadi na kushawishi wananchi wachague sera za chama chake na kuweka ahadi pindi akichaguliwa kuwa rais wa nchi, atatekeleza sera za chama hicho.
Vyama vya siasa; kila kimoja kilitoa mgombea wa urais, na wote walizunguka nchi nzima kujinadi na kumwaga sera kwa wananchi. Watu waliwasikiliza kwa utuvu na kuwapima katika mizani yao na mwisho walimchagua Dk. John Pombe Magufuli kuwa rais wao kutoka Chama Cha Mapinduzi.

Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 imeweka mkazo kwa serikali zake mbili; kwanza kuondoa umaskini; pili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana; tatu kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; na nne kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama wa maisha ya wananchi na mali zao.
Kuhusu mkazo wa tatu wa kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; katika kipindi cha miaka mitano (2015-2020) Serikali imeelekezwa kutekeleza mambo (mambo 13) ambayo yataendeleza kukuza Sekta ya Madini na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa.

Baadhi ya mambo hayo ni; (a) kuweka na kusimamia mfumo thabiti wa kukagua shughuli za migodi, kukusanya takwimu za madini na kufuatilia maduhuli yatokanayo na madini kwa malengo mapana ya kuongeza mapato ya Serikali.
(b) kuweka na kutekeleza mikakati madhubuti ya kuvutia mitaji ya uwekezaji katika Sekta ya Madini, hususani kwenye madini adimu (Rare  Earth Elements-REE)
(e) Kuboresha mfumo wa utoaji na usamamizi wa leseni za madini, na upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wadau kuhusu Sekta ya Madini.
(f)  Kuimarisha udhibiti na usimamizi wa upatikanaji, utunzaji, usafirishaji na matumizi ya baruti katika shughuli za migodi.
(k) kubuni na kutekeleza mikakati mahsusi itakayowezesha kupunguza au kukomesha kabisa vitendo vya utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na biashara haramu ya madini nchini.
Mambo hayo na mengine ndiyo ambayo Rais Magufuli amesimama imara kutekeleza. Anapotokea kiongozi nje ya CCM kudai hadharani anayotekeleza Rais Magufuli ni mawazo na mpango huo ni wake na ni ajenda ya chama chake ilhali wakati wa kampeni hakusikika kusema hivyo, ni wazi pana ngoa.

Si kanuni wala lazima unapocheza ngoma kumpa chambi mkweo au mchezaji mwenzako ili nawe uonekane unacheza ngoma lau kama huna mdadi wa kucheza; sembuse kujipa chambi mwenyewe. Subiri upewe.
Ni utu na busara kwa baadhi ya viongozi wetu wa siasa kuwa wastaarabu na wakweli. Wasiwe na hiyana wanapoona mwanasiasa mwenzao kung’ara katika kutekeleza ahadi alizoweka kwa mujibu wa ILANI ya chama chake. Wampongeze na kumpa kongole za dhati; huo ndiyo uungwana; siyo kunena.

Narudia kusema Watanzania hasa wananchi wenzangu ngoma ndiyo hiyo inakesha; isizimwe kwa sababu mlio wa ngoma umesikika hadi ng’ambo na kuwaleta wale wapiga ngezi na nderemo. Manju hao wamekiri kufanya dhambi na kukubali kutunga mashairi, midundo na mitindo mipya ya haki na utu ili ngoma ichezwe na kukesha.
Ni imani yangu kuona viongozi wa siasa nchini wanasema kweli. Si vyema kusifu chanda chako kuvaa pete wakati hakijawahi kuvishwa hata siku.

By Jamhuri