Yah: Nayaona mabadiliko yajayo kwa kasi isiyotarajiwa

Kuna wakati niliwahi kuandika katika waraka wangu kwamba kuna mabadiliko makubwa yajayo ambayo nayaona njozini, nilisema nikijihami kwamba labda ipo siku yanaweza kukwama, mkwamo ambao ungesababishwa na kusita kwa baadhi ya watu katika kutekeleza azma ya pamoja kukubaliana na kaulimbiu ya hapa kazi tu.

Sasa nayaona mabadiliko yajayo kwa kasi isiyotarajiwa, kasi ambayo tunatakiwa kujipanga kuipokea kwa kuwa hayakuwa mazowea yetu kuishi kwa namna hiyo, tulizowea kuishi kwa siasa za hapa na pale ili siku iende, tulikuwa wapambe katika masuala ya siasa na kupoteza muda mwingi tukibishana mambo ya siasa na kuendesha mikutano isiyokuwa na tija kwa Taifa wala kibali cha kufanya siasa.
Nilisema siasa ni sehemu ya maisha ya Watanzania wenzangu ambao wengi wao walikuwa madalali wa vigogo wachache kunogesha siasa, tuligeuza Taifa kuwa uwanja wa matukio ya kisiasa na wapo waliosema nchi haiwezi kwenda bila siasa, nadhani hao walisahau kuwa siasa ya kazi ambayo sisi tuliizowea tangu enzi za siasa ni kilimo inaweza ikaendeshwa pasi na kukaa vijiweni kufanya siasa.
Tulizowea maisha ya dili nchi nzima, hili halina mjadala kwa wanaoelewa dili maana yake nini, ilikuwa ngumu kuamini kwamba dili zinaweza kufa kifo kibaya kama hiki, ilikuwa kawaida kumpa heshima mpiga dili badala ya kumpa heshima mchapakazi, haya yalikuwa maisha ya kawaida na kupewa hadhi ya juu katika jamii yetu ya Watanzania waliopata uhuru miaka hamsini iliyopita.

Tulizowea ukiritimba katika kila kitu ilimradi kutengeneza ajira ya mtu wa kati, mtu wa kati almaarufu kama dalali alikuwa na jeuri ya kufanya kila akitakacho ikiwamo hata kuyumbisha maisha ya watu na kuleta madhara katika jamii.
Wapo madalali waliotunywesha dawa feki na hata zilizopita wakati kwa manufaa yake yeye mwenyewe, waliomtuma na wanaosimama nyuma yake kumtetea.
Wapo waliopandisha gharama za maisha ya Mtanzania kwa udalali wao na wameweza kupata fedha za kutosha kununua baadhi ya viongozi na kuongeza ukiritimba mwingine kwa manufaa yao, kiufupi kundi hili la makiritimba limeifanya jamii ya Watanzania kuamini kuwa maisha ni magumu sana.

Kupitia kundi hili, gharama za mafuta zilikuwa zayumbishwa kila siku, gharama za maji zilikuwa afadhali kupata mafuta kuliko maji ya kuoga, gharama za vyakula zilikuwa kama vile chakula tunaagiza kutoka nje ya nchi kumbe tunalima hapahapa Kipatimo, walipandisha gharama za nishati hadi wanyama wetu waliopo mbugani.
Madalali waliingia hadi katika migodi, waliingiza ukiritimba ambao umetufikisha hapa tulipo leo, hii ndio Tanzania hasa ambayo inahitaji pasi kubwa kuinyoosha pamoja na maombi maalumu kuweza kubadilika.
Nchi hii tulizowea undugu na urafiki hata katika mambo ambayo yanafanyika kwa manufaa ya kitaifa, sasa tunaanza kuyakubali matokeo ambayo hatukuzowea, inakuwa vigumu kutembeza fedha kama mlungula, inakuwa vigumu kukweza majina yetu kwa kutumia nguvu ya fedha huku tukijua kuwa tunatumia rasilimali ya wote kujinufaisha wachache.

Nchi hii ilifika mahali pabaya kwamba mtoa rushwa anajinadi hadharani huku akitisha viongozi wa Serikali, nchi hii ilifika mahali ambapo sheria iliwahusu wananchi wa hali ya chini lakini si wenye vipato au viongozi walioko madarakani, kiufupi ilikuwa pepo ya wachache kwa niaba ya wengi.

Nchi hii ilikuwa barabara ya kupitisha kila jambo baya duniani, dawa za kulevya, madini feki, madini ya wizi, mali za wizi, wanyamapori na kadhalika. Nchi hii ilikuwa ya kutakatisha fedha haramu za mafisadi tena waliotuhujumu, sasa inaelekea kunyooka japo mkunjo ulikuwa mgumu.

Nchi hii ilikuwa ikielekea kuwa nchi ya walezi wa majambazi, majasusi, magaidi, wauza unga, majangili, maharamia, wakimbizi feki, wanasiasa uchwara, wapigadili mbovu, wala rushwa, waganga wa kienyeji feki, watu wa michongo, wezi na wabaya wote uwajuao.
Tuko kwenye mapito ya mabadiliko makubwa na mazito, wenye nacho wanatumia nguvu na akili ya pesa kunyong’onyesha jitihada kwa kuwa wengi wetu ni masikini na bendera fuata upepo wa kisiasa za udanganyifu na kuturudisha katika umaskini.
Tuunge mkono jitihada za viongozi walioamua kuongoka na kuwa na sisi, tuunge mkono bila unafiki na wakikosea tutoe ushauri bila unafiki pia, tusifanye mambo kwa woga bali tufuate sheria za nchi katika kutekeleza juhudi zetu.
Vita ni pevu inawezekana wanaamini hakuna vita ya maendeleo itakayomwacha mtu huru, mimi naamini tutashinda dhidi yao.

Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.