Hussein Amar KasuMbunge wa Jimbo la Nyang’hwale, mkoani Geita, Hussein Amar Kasu, amejikuta akipigwa na butwaa baada ya mtu aliyemwandaa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, John Isack John, kushindwa.

John, Diwani wa Kata ya Kafita, aliandaliwa mazingira ya ushindi ambapo madiwani 14 kati ya 21 wa halmashauri hiyo wanaelezwa kuwa walipewa fedha Sh Sh milioni moja kila mmoja ili kuwahadaa wampitishe mtu wake huyo.

Tukio hilo lilitokea Desemba 3, 2015 mchana katika Ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, muda mfupi baada ya mkutano wa uchaguzi wa kumpata mwenyekiti na makamu wa halmashauri hiyo kumalizika.

Katika uchaguzi huo, Loyce Mussa alitangazwa huku mbunge huyo akiamua kudai hadharani pesa aliyowapa madiwani hao aliowaita wasaliti.

Kwenye kinyang’anyiro hicho, wagombea walioteuliwa na chama hicho walikuwa wawili – Musa kutoka Kata ya Kaboha na John aliyeanguka.

Taarifa ya kile kilichofanyika zilifichwa, lakini sasa zimefumuka zikisema kwamba hali ya usalama mara baada ya matokeo ilikuwa mbaya.

Mtoa taarifa wa gazeti hili aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, aliliambia gazeti hili kwamba mbali ya Louce na Mussa pia alikuwako mgombea mwingine wa tatu ambaye ni Yavin Petro Noah.

Noah alikuwa akitetea nafasi yake, lakini jina lake lilikatwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Geita kutokana na sababu ambazo gazeti hili halikuweza kuzipata.

“Aah! unataka kujua kilichojiri. Of course tulikuwa kwenye mchakato wa kumpata mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale. Katika mchakato huo uliomalizika Desemba 3, mwaka huu mchana, wagombea kwa upande wa mwenyekiti walikuwa watatu – Yavin Petro Noah (Bukwimba), Loyce Mussa na John Isack John,” anasema mtoa taarifa.

“Hata hivyo, jina la Noah lilikatwa dakika za majeruhi na Kamati ya Siasa ya Mkoa mwishoni mwa mwezi Novemba na kubakizwa majina ya madiwani wawili.

“Musa na Isack John ambaye yuko kambi ya mbunge wa jimbo hilo Husein Amar Kasu,” anasema mtoa taarifa na kuongeza:

“Kati ya majina hayo mawili yaliyobaki, mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, John, alikuwa ni chaguo la mbunge huyo ambapo siku moja kabla ya uchaguzi huo (Desemba 2, 2015), mbunge huyo aliwaita nyumbani kwake baadhi ya wajumbe (madiwani) ili kukubaliana namna wanavyoweza kumpatia kura mtu wake huyo,” alieleza mtoa taarifa.

Imeelezwa kuwa madiwani waliokwenda nyumbani kwa mbunge huyo eneo la Ibalanguru katika Kata ya Izunya, wilayani humo, ni 14 kati ya 21 wanaounda halmashauri ya wilaya hiyo.

“Sasa bwana, mbunge alitualika nyumbani kwake siku ya Desemba 2, mwaka huu na tulipofika tuliongea mambo mengi, lakini mwisho wa siku alitupatia kila mmoja kiasi cha shilingi milioni moja na akasema ni pesa ya maji… ila katika mazungumzo yake alisisitiza tumchague John na sisi tulimkubalia kwa shingo upande kwani chaguo letu lilikuwa Loyce Musa na ndiye tuliyempa kura… sasa tunashangaa kuanza kudai pesa yake kwani tulimchukulia mfukoni?” anahoji mmoja wa madiwani waliochukua mgawo huo.

Habari zinasema katika kikao hicho cha siri kati ya mbunge na madiwani hao, ilimlazimu mbunge huyo kuwapa madiwani hao fedha aliyoiita ya maji kiasi cha Sh milioni moja kila mmoja, lakini kwa mashariti ya kuhakikisha wanampigia kura za John na kuhakikisha anashinda nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo. Anasema walimkubalia.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, pamoja na kupewa kiasi hicho cha maji kutoka kwa mbunge huyo, siku iliyofuata madiwani hao walimtosa John, diwani aliyeungwa mkono na mbunge.

“Ndiyo hapo valangati lilipoanzia kwa mbunge huyo kuomba arudishiwe pesa zake kwa madai kuwa wamemsaliti…hadi sasa madiwani waliochukua pesa ya maji ya mbunge wamegawanyika katika makundi mawili, kuna baadhi yao wameapa kutorudisha kiasi hicho cha pesa na wengine wanajishauri warudishe au la kwani hakukuwapo mkataba wowote walioandikiana na mbunge huyo bali aliwapa kwa kutaka yeye,” anasema.

Mmoja wa madiwani aliyenufaika na mgawo huo alipoulizwa iwapo madai hayo yana ukweli wowote, mbali na kukiri aliapa kutorudisha kiasi hicho cha pesa kwa vile hakumlazimisha kumpatia.

“Sisi haturudishi hiyo pesa kwani hatukuchukua kwa ajili ya kumchagua mtu… sisi alitupa pesa ya maji na yule mtu wake tukampiga chini na hatuwezi kuchaguliwa mtu legelege… tunataka mtu wa kasi inayoendana na Rais wetu, John Pombe Magufuli, ili tuwaletee wananchi wetu maendeleo stahiki,” anasema.

Katika uchaguzi huo, Mussa alipata kura 16, huku John Isack ambaye ni mtu wa mbunge akiambulia kura 7 kati ya kura 23 zilizopigwa.

Msimamizi wa uchaguzi huo aliyefahamika kwa jina moja tu la Makoye, ni Katibu wa CCM Wilaya hiyo. Makoye ndiye aliyemtangaza Musa kuwa mwenyekiti mteule wa halmashauri hiyo.

Baada ya uchaguzi huo, ulihudhuriwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Geita, Josephine Chagula, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya hiyo, Adam Mtore, Katibu Mwenezi wilayani, Said Madoshi na mbunge Amari.

Kadhalika, katika uchaguzi huo pia ulifanyika uchaguzi wa makamu mwenyelkiti wa halmashauri hiyo na aliyeshinda ni Faida Nyanda, Diwani wa Kata ya Kakola kwa kupata kura 12, dhidi ya mpinzani wake Manuel Ndozi, Diwani wa Nyugwa, aliyepata kura 10 kati ya kura 20 zilizopigwa baada ya kura moja kuharibika.

Katibu Mwenezi wa CCM Geita, Madoshi, alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na tuhuma hizo hakukiri wala kukana badala yake alidai kuwa masuala hayo yanawahusu waliopeana pesa na si vinginevyo na kwamba.

“Iwapo yangekuwa  yanahusu mambo ya chama chetu ningeweza kuyazungumzia kwa vile ndiye msemaji wa chama hicho,” anasema Modishi.

Baada ya uchaguzi huo, mbunge huyo alisimama na kueleza: “Bwana leo kuna unafiki umetendeka… mmekula hela na hamjampa kura John Isack… huo ni unafiki na wale mliochukua pesa hiyo naomba mbaki hapa ukumbini ili tujadiliane,” alinukuliwa.

Kutokana na hali hiyo, baada ya mkutano huo wa uchaguzi kumalizika, madiwani wote waliokula kiasi hicho cha pesa ya mbunge walilazimika kubaki ukumbini kama walivyotakiwa na mbunge huyo na katika mazungumzo yao walitakiwa kurejesha pesa hizo.  

Ili kumridhisha mbunge huyo, walidai kwa wakati huo hawakuwa na pesa hiyo waliiacha nyumbani na kuahidi kuirejesha siku iliyofuata.

Hata hivyo, baada ya kutoka ukumbini hapo madiwani hao walisikika wakiapa kutofanya hivyo kwa madai kuwa hakuna aliyemlazimisha kuwapatia kiasi hicho cha pesa na kwamba wako tayari kwa lolote.

Naye mbunge huyo alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alidai: “Aliyekupa taarifa ndiye anayejua ukweli zaidi. Mimi nikieleza wala haitasaidia. Wewe andika ulichoelezwa, sina zaidi,” anasema mbunge.

By Jamhuri