Sylvester AmbokileIdara ya uhamiaji inafukuta, baada ya uwepo wa taarifa za ununuzi wa kiwanja cha ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya askari wa taasisi hiyo kilichonunuliwa mkoani Mbeya hivi karibuni.

Vyanzo vya habari kutoka katika jeshi hilo vimedokeza kuwa viongozi wa idara hiyo wamenunua kiwanja hicho kwa kiasi cha Sh milioni 400 katika eneo lisilo na sifa za kujengwa kwa chuo.

Inaelezwa kuwa kiwanja hicho, chenye ukubwa wa ekari 25 kimenunuliwa wilayani Ileje, Mbeya na kwamba kipo katika mteremko jambo linalozua maswali mengi kwa baadhi ya maofisa wa idara hiyo.

Hata hivyo, wakati Uhamiaji wakinunua kiwanja hicho, kati ya mwaka 2007 na 2009, Serikali ya Mkoa wa Tanga iliwahi kutoa kiwanja katika Wilaya Mpya ya Mkinga. Kiwanja hicho kina zaidi ya ekari 300.

Taarifa za uhakika zinasema kwamba Serikali ya Mkoa wa Tanga ilitoa kiwanja hicho kikubwa kwa lengo la ujenzi wa chuo cha mafunzo ya uhamiaji nchini ili kutimiza ndoto zao za kuwatoa wanafunzi wake Chuo cha Polisi (CCP), Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kiwanja hicho kilichopo ufukweni mwa bahari katika vijiji vya Manza na Vuo, awali kilikuwa ni shamba la mkonge huku baadhi ya maeneo yakiwa mashamba ya wanakijiji wa vijiji hivyo.

Wanakijiji hao walilipwa fidia na Serikali ili kupisha ujenzi wa chuo hicho, lakini habari kutoka ndani ya Maofisa wa Uhamiaji ni kwamba wamekikacha kiwanja hicho na kuhamia Ileje mkoani Mbeya.

Hata hivyo, pamoja na kutengwa kwa shamba hilo kubwa kwa ajili ya ujenzi huo, viongozi wa Uhamiaji Makao Makuu waliamua kununua eneo jingine jambo ambalo limesababisha mtafaruku ndani ya idara hiyo.

Aidha kumekuwepo na madai ya kuwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile kujimilikisha shamba hilo lililostawi mkonge kinyume cha taratibu.

“Mara kwa mara amekuwa akionekana shambani kule Tanga, wapo wanaomuona na kusema, ‘Shamba limestawi sana mkonge’, naye anaona ni vigumu kuachia fedha hiyo ndio maana ameweza kufanya awezalo kununua eneo jingine mkoani Mbeya ili kujenga chuo ili hapa pamuingizie fedha,” anasema mtoa taarifa.

Mtoa taarifa huyo anaeleza kuwa katika upatikanaji wa shamba hilo, Kamishna wa Mipaka na Operesheni, Abdullah Abdullah ndiye aliyefanikisha upatikanaji wake wakati akiwa katika chuo mkoani Kilimanjaro.

JAMHURI limefanya mahojiano na Abdullah kuhusiana na shamba hilo ambako anakiri kuhusika kutafuta eneo hilo baada ya aliyekuwa Kamishna wakati huo, Kinemo D. Kihomano (1997 hadi 2010), kutoridhishwa na mafunzo wanayopata mkoani Kilimanjaro.

“Kamishna alitaka tuweze kuwa na chuo chetu wenyewe, kitakachokuwa kikitoa mafunzo ya uhamiaji tu, sio kama ilivyo sasa. Chuo hiki kitaweza kuwapika ipasavyo maafisa wetu katika utekelezaji wa majukumu yao, akaniagiza kutafuta eneo, nikapata mkoani Tanga. Lakini kwa sasa sijui nini kinaendelea na mimi si msemaji wake,” anasema Abdallah.

Inaelezwa kuwa chuo hicho kilikuwa mahususi kwa ajili ya mafunzo yote ya kijeshi yanayohusiana na ulinzi na usalama wa nchi.

Pia inaelezwa kuwa aliyekuwa Rais wa Libya Muammar Gaddafi katika utawala wake aliwahi kutaka kusaidia ujenzi wa chuo hicho.

Kadhalika akizungumza na JAMHURI, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Ambokile anasema kuwa idara hiyo haina eneo lolote mkoani Mbeya na kuwa bado wanatafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha mafunzo.

“Hatujaamua kujenga chuo Mbeya, tunatafuta bado eneo, nia yetu ni kuwa na chuo chetu wenyewe, ila Tanga tunalo eneo, lakini sio lazima lijengwe chuo,” anasema Ambokile.

Alipoulizwa kuhusiana na  kuwepo kwa eneo lililotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa chuo mkoani Tanga anasema kuwa hana kumbukumbu kama lililotewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa chuo.

Hata hivyo, alipoulizwa kuwepo kwa taarifa za yeye binafsi kujimilikisha eneo hilo, akasema kuwa eneo hilo lilitafutwa na watangulizi wake, “kwanini nilichukue wakati sina mpango wa kuwa mkulima?”

Akaongeza: “Kwanza sina interest (sivutiki) shamba, kwani sina uwezo wa kutafuta eneo langu binafsi?, kwanini (mwandishi wa habari) ufuatilie mambo ya kufikirika?” anahoji Ambokile.

Hata hivyo alipoulizwa ni kwanini idara hiyo ihangaike kutafuta eneo jingine la kujenga chuo wakati eneo hilo lipo, anasema: “Sio lazima chuo kijengwe mkoani Tanga na kuwa idara inatakiwa kuwa na maeneo zaidi ya moja.”

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alimwagiza Katibu Mkuu  wa Mambo ya Ndani kupeleka wakaguzi katika Idara ya Uhamiaji ili kuweza kuondoa utata na kujua malipo yanayofanyika kwa njia ya benki.

Waziri Kitwanga ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji na kujadiliana mambo mbalimbali na wakuu wa idara ili kuboresha utendaji kazi.

Wakati Waziri Kitwanga akitoa agizo hilo, kumekuwepo na taarifa za matumizi mabaya ya fedha ikiwa ni pamoja na ununuzi wa kiwanja cha mkoani Mbeya pamoja na fedha kwa ajili ya kufanyika operesheni.

JAMHURI lilizungumza na Waziri Kitwanga kuhusu ununuzi wa kiwanja hicho, akasema: “Ni kweli nilifanya ziara makao makuu ya uhamiaji Kuranisi Jijini Dar es Salaam.”

Alipoulizwa iwapo ana taarifa za kuwepo na shamba kubwa mkoani Tanga, Kitwanga anasema kuwa hana taarifa hizo na wala hakupatiwa taarifa hizo wakati wa ziara hiyo.

“Sijaambiwa lolote, labda nifuatilie sasa maana mimi ni mgeni katika wizara hii, lakini kwa vile nimeagiza ukaguzi wa haraka yapo nitakayoyabaini tupeane muda,” anasema Waziri Kitwanga.

Aidha JAMHURI limedokezwa kuwa tayari ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kufuatilia ununuzi wa eneo hilo unaoelezwa kuwa na utata huku ukiomba kupatiwa taarifa za kina.

2261 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!