‘Unga’ wasambaratisha polisi

3-Waziri-wa-Ujenzi-John-Magufuli-kush-akitoa-taarifa-kwa-waandishi-wa-habari-hwapo-pichani-leoKamanda-MpingaWiki moja tu baada ya JAMHURI kuchapisha orodha ya wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefanya uhamisho kwa askari wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni na Mkoa wa Tanga.

Habari za uhakika zilizolifikia JAMHURI zimebainisha kuwa uhamisho huo wa haraka umefanyika kuvunja mtandao wa uhalifu, hususani wauza dawa za kulevya ndani ya jeshi hilo.

Asilimia kubwa ya ‘mapapa’ wa biashara hiyo haramu wapo jijini Dar es Salaam, hasa maeneo ya Kinondoni, Magomeni na Mbezi Beach yakiongoza kwa kutoa idadi kubwa.

Katika kuhakikisha mtandao huo sugu unavunjwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alianza operesheni kwa kumulika Jeshi la Polisi nchini ambako alikabidhiwa orodha ya askari polisi  wanaojihusisha na biashara hiyo.

Taarifa zinasema baada ya kukabidhiwa orodha hiyo, naye aliipeleka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu ambaye ameanza kuifanyia kazi.

“Kuna mtu alionana na Waziri, akamkabidhi orodha ya askari polisi ambao wanafanya biashara kwa kushirikiana na wauza unga, naye alikwenda moja kwa moja kwa IGP na kumkabidhi majina hayo, wengi wapo kituo cha Oysterbay,” anasema mtoa taarifa.

Anasema kitendo cha askari polisi kushirikiana na wahalifu kilimuudhi waziri na kutaka hatua za haraka kuondokana na fedheha hiyo.

Kadhalika inaelezwa kuwa baada ya IGP Mangu kukabidhiwa majina hayo, waliwataka askari wa kituo cha Oysterbay kumkabidhi orodha ya majina ya wauza unga haraka.

Baada ya amri hiyo, kituoni hapo kulikuwa na tetesi za kuondolewa kwa baadhi ya askari kitendo kilichozua tafrani huku baadhi yao wakihaha na kuanza kuwasiliana na watu wao wa karibu kwa lolote linaloweza kutokea.

Desemba 23, 2015 JAMHURI lilifika Oysterbay Polisi ambako lilishuhudia baadhi ya askari katika kituo hicho wakihaha kutokana na kuwepo na taarifa za kuondolewa.

“Hivi unavyotuona hatujui bwana mkubwa anawaza nini. Tumepata taarifa kuwa kuna uhamisho mkubwa unakuja kutokana na masuala ya wauza unga. Kila mmoja anafanya awezalo kuona inakuwaje. Asikudanganye mtu, hapa matumbo joto,” anasema mmoja wa askari hao.

Desemba 24, 2015 Gazeti hili la JAMHURI lilipata taarifa kuwa tayari jeshi la polisi limewahamisha askari zaidi ya 10 katika kituo cha Oysterbay na maofisa wawili kutoka mkoa wa Tanga.

Maofisa waliohamishwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, RPC Zuberi Mwombeki amehamishiwa Ruvuma, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tanga RCO Aziz Kimati.

RPC Kinondoni Camillius Wambura, RCO Kinondoni

Mkuu wa Utawala Kinondoni, pamoja na baadhi ya askari wa kitengo cha upelelezi (6), na wengine kutoka idara tofauti tofauti, nao wamehamishwa.

Uhamiasho huo umegusa pia kitendo cha kikosi kazi cha taifa chenye ofisi zake Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza na JAMHURI baadhi ya askari katika kituo cha Oysterbay wanasema uhamisho huo ni pigo kwa baadhi yao ambao walikuwa hawaamini kama wanaweza kuondolewa kituoni hapo.

Wanasema pamoja na uhamisho huo kugusa baadhi yao, lakini wanaamini unaweza kuwa na mwendelezo hivyo kila mmoja wao yuko tayari tayari kwa lolote linaloweza kujitokeza maana hata mikoa ambayo wenzao wamepelekwa ni mikoa ambayo ni kama wametupwa.

Akizungumza katika mahojiano na JAMHURI, Kitwanga amesema suala la uhamisho si jambo geni katika utendaji wa Serikali, hivyo uhamisho huo umefanywa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.

Alipoulizwa uhamisho huo kuhusishwa na mtandao wa dawa za kulevya nchini hakuwa tayari kujibu swali hilo huku akidai kuwa ameshalijibu.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na kumpatia IGP Mangu majina ya askari wanaojihusisha na dawa za kulevya amekiri kukabidhiwa orodha hiyo na kwamba tayari alikwisha mkabidhi Mangu kwa utekelezaji.

Kitwanga anasema amejipanga kuhakikisha anavunja mtandao wa wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya na tayari amepata taarifa nyingi nyeti kuhusiana na wafanyabiashara hao hivyo mkakati wa kuwakabiri tayari umeshaanza.

Anasema katika kipindi kifupi ambacho ameingia wizarani hapo amepata taarifa nyingi kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ambazo zimemuwezesha kuanza mapambano hayo makubwa.

“Natambua ya kuwa kuna watu waliamini kuwa hawawezi kuguswa, nitawagusa na kupambana kuondokana na biashara hii haramu. Ni lazima kutimiza ahadi ya Rais, nami nipo hapa kumsaidia Rais, pamoja na kuwa wapo wanaoamini kuwa haiwezekani. Subiri uone hakuna sehemu ambayo hatutofika,” anasema Kitwanga.

Baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Kitwanga aliwataka polisi wamweleze mikakati waliyonayo ya kupambana na wauzaji wa dawa za kulevya kabla ya wiki iliyopita.

Habari za uhakika zilizolifikia JAMHURI zinasema Rais John Pombe Magufuli tayari amekabidhiwa majina ya wauzaji, wasafirishaji na waagizaji wa dawa za kulevya nchini.

Wiki iliyopita, JAMHURI lilichapisha orodha ya watu 560 ambao wanaotajwa kuwa vigogo wa usafirishaji wa biashara dawa za kulevya.

Katika orodha hiyo, wamo wachungaji, waimba taarab maarufu na wafanyabiashara wenye ukwasi wa ghafla unaotisha wengi. Wapo ambao gazeti hili limefanikiwa kupata makazi yao, lakini wengi wameorodheshwa na vyombo vya dola vinaendelea kukusanya taarifa zao.

Baadhi ya mapapa hao ni raia wa kigeni na wengine wako rumande wakishikiliwa na vyombo vya dola, na huku wengine wakiwa wamefikishwa mahakamani na ama kuachiwa huru, au kutumikia kifungo cha nje.

Zaidi ya asilimia 90 ya ‘mapapa’ hao wapo jijini Dar es Salaam, huki maeneo ya Kinondoni, Magomeni na Mbezi yakiongoza kwa kutoa idadi kubwa. Kilo moja ya cocaine inatajwa kuuzwa hadi Sh milioni 50.

Kwenye orodha hii, wamo Watanzania na raia wa mataifa mbalimbali walionaswa kwa nyakati tofauti, wengine wakiwa wamejichimbia kwenye mahekalu katika maeneo ya Mbezi, Oysterbay na Masaki.

Miongoni mwa ‘mapapa’ hao ni Fredy William Chonde (mkazi wa Magomeni), Kambi Zuberi (Temeke), Abdul Ghan na Shahbaz Maliki (Pakistani) ambao wamekamatwa wakiwa na kilo 175 za heroin.

Mapapa wawili -Shahbaz na Maliki ambao ni raia wa Pakistani, wametoroka nchini baada ya kupewa dhamana katika mazingira tata. Jaji aliyetoa dhamana hiyo kinyume na kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya, kwa sasa anasikiliza kesi nyingine ya dawa za kulevya na tayari ametajwa kuwa na mizengwe ya hapa na pale.

Papa mwingine, Ally Mirzai Pirbakhish ambaye ni Mpakistani, alikamatwa akiwa na waimba taarabu maarufu ambao wote ni wakazi wa Kinondoni.

Waimbaji hao ni Aziz Juma Kizingiti, Said Mashaka Mrisho, Abdulahman Mtumwa, na Hamidu Kitwana Karimu. Nao hawa majina yao yametua kwa Rais Magufuli.

Pia kuna watuhumiwa Ismail Shebe Ismail, Rashid Salim na Majed Gholamghader (wote wakazi wa Kinondoni, Dar es Salaam) ambao wamekamatwa wakiwa na kilo 50 za heroin. Kesi yao inaendelea Tanga.

Raia wa Afrika Kusini, Jack Vuyo na Anastazia Elizabeth Cloete, wako mbaroni kwa kukutwa na kilo 42 za heroin. Mnigeria aliyetambuliwa kwa jina la Kwako Sarfo amekamatwa akiwa na kilo 11.951 za cocaine.

Mapapa wengine ni wakazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Aziz Juma Kizingiti, Said Mashaka Mrisho, Abdulahman Mtumwa, Hamidu Kitwana Karimu na Mpakistani Ally Mirzai Pirbakhish ambao wamekamatwa wakiwa na kilo 97 za cocaine.

Kwenye orodha hiyo wamo Mwanaidi Ramadhan Mfundo ambaye ameolewa na raia wa Kenya, lakini nyumbani kwa wazazi wake ni Mbezi Beach, Dar es Salaam. Huyu amelipa sifa ya pekee Jeshi la Polisi Tanzania kwa kumkamata kwani anatafutwa na Marekani, Uingereza, Ujerumani na nchini nyingine ambako kote huko alishindikana kukamatwa, lakini polisi wa Tanzania wakamkata akiwa Mbezi, Dar es Salaam.