Home Makala MAFANIKIO KATIKA AKILI YANGU (10)

MAFANIKIO KATIKA AKILI YANGU (10)

by Jamhuri

Na Phabian Isaya

Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Sasa wewe kazana, hakikisha unatengeneza wigo wa watu wengi wenye tija, alimsihi Noel katika hilo.
Kadiri Noel alivyokuwa akizungumza na Profesa Alison Ziki (Mzimbabwe) katika simu, ndivyo alivyozidi kupata hamasa na mwamko wa kuandika.
“Nitakuwa nikikujulia hali mara kwa mara, alisema Profesa Ziki kikisha akakata simu. Profesa huyo Mzimbabwe alikuwa yupo nchini Afrika Kusini. Alimuweka Noel katika kumbukumbu zake.
Noel naye akamuweka katika akili yake, akiamini ipo siku watakutana na kufanya mambo mazito.
Akiwa amelala kitandani, kijana Noel usingizi ulikosekana, akaamka na kuchukua daftari ambalo alinunua na kuandika wazo jipya la kitabu alichokipatia jina la Kiingereza I NEVER FORGERT MY CONTINENT. Alikuwa ameanza kuandika tangu akiwa  nchini Tanzania.
Akaamua kukaa kuendelea kuandika. Akashika kalamu yake na kuendeleza mtiririko wa mawazo yake. Pamoja na  baridi nyingi kuwapo, lakini Noel hilo hakuweza kulifikria kama kikwazo kwake. Aliamua kuvaa glovu mikononi ili kuzuia baridi kuingia kwenye mikono na kumfanya ashindwe kuandika.
Noel alipoanza kuandika mtiririko wa mawazo ulikuwa mara tatu ya yale aliyokuwa nayo mwanzoni. Picha ya kile alichokuwa akikiandika ilimjia kama uhalisia machoni pake. “Ninatamani kitabu hiki kije kusomwa na watu wengi Afrika na hata hapa nchini Urusi pia, alijisemea moyoni.
Alikuwa akiandika huku hilo ndilo likiwa kusudi lake halisi. Akiwa anaendelea kuandika, akitumia nguvu ya akili ya pili, sauti ile ile ikamjia akilini mwake: “Success is on my mind.” Sauti hiyo ilipomjia Noel alijikuta akihamasika na kuandika akiamini ipo siku mambo yatakwenda kubadilika na akazungumziwa kwa namna ya tofauti.


Wakati Noel akiendelea kuandika, alikuwa akikumbuka vitu vingi sana, zikiwemo ahadi alizokuwa akipewa na watu mbalimbali. Akamkumbuka mama mmoja aliyekuwa akimkwepa sana baada ya kumpa ahadi ya kuchapisha kitabu.
Noel akiwa anaandika alikuwa akiingiwa na kumbukumbu ya matukio ya nyuma. 
“Mungu endelea kunipa watu sahihi,” alisema Noel huku akiacha kuandika kwa muda wa dakika kadhaa na kufikiria zaidi jinsi ya kuandika kitabu chake kwa ufasaha.
Mariana alikuwa chumbani kwake naye alikuwa bado angali hajalala, alikuwa akiangalia sinema katika tanakilishi mpakato yake. Ghafla akapigiwa simu na mfanyakazi mwenzake. Mariana akaitazama kisha akaipokea.
“Vipi Mariana? Mariana akaitikia kwa shauku: “Safi, upo nyumbani? aliuliza Mariana. “Ndiyo nasikia tumepewa muda wa majuma ili tuweze kukamilisha kuandika vitabu, alisema.
Dah! Inakuwa taarifa nzito kwa Mariana, maana chuo kilikuwa kina gharamika kununua vitabu na ukaanzishwa utaratibu wa kuwafanya wahadhiri kuaanda wenyewe vitabu vya kufundishia. Huu ulikuwa utaratibu wa chuo chao Mariana alichokuwa akifundisha.
Dah! Hii shughuli sasa, ila haina shida, alisema Mariana akishusha pumzi yake. “Mimi ndiyo sijui nitaanzia wapi uwezo wa kuandika vitabu sina, sijui nitampata wapi mtu mwenye uwezo huo,” alisema Mariana. 
Mariana akafikria kwa muda wa sekunde chache na kugundua kuwa Noel hiyo kazi inaweza kuwa moja ya fursa kwake kutengeneza jina na kujipatia fedha. Akaamua kumshauri huyo mhadhiri mwenzake.
 “Nina kijana hapa nyumbani kutoka Afrika anaweza kuandika vitabu, tunaweza kumtumia yeye na kumlipa, alisema Mariana. “Sawa, tena huyo hata kesho nikutanishe naye, alisema kwa shauku mhadhiri mwenzake Mariana.
“Sawa, kwa sasa amepumzika ila asubuhi nitaongea naye tuone, wakaelewana kisha Mariana akakata simu huku mawazo yakienda mbalia sana.
“Mungu amefanya njia kwa huyu kijana, naamini anaweza, anakatisha sinema aliyokuwa akiangalia na kufunga tanakilishi mpakato yake.
Mariana akaendelea kufikiria zaidi: “Hivi si nimtafutie pointi yeye aanze kuandika? Alikuwa akiwaza namna ya kumrahisishia mambo Noel ili amsaidie kuandika kitabu.
Mariana akatoka chumbani na kwenda kukaa sebuleni akiwa ameshikilia kalamu na karatasi. Alitaka kutengeneza uwanda wa vitu ambavyo ataanza kuandika ili kusababisha muundo wa kile kitu alichokuwa anakihitaji.
Chuo kiliamua kufanya hivyo kutokana tu na kutumia pesa nyingi katika machapisho ya vitabu kuwalipa waandishi ambao walitoka nje ya chuo. Ulikuwa ni mpango wa kupunguza gharama katika uchapishaji wa vitabu.
Mariana akaumiza kichwa, baba yake ambaye ni profesa akatoka chumbani kwenda kuchukua kitabu katika kabati akamkuta Mariana akiwa anaandika huku mawazo yake yakiwa mbali sana kwa muonekano wake. “Mariana si utachelewa kulala? alihoji baba yake.
Mariana akamjibu baba yake: “Hapana baba, kuna suala hapa nimepigiwa simu linahitajika kufanyiwa ufumbuzi wa haraka. Alisema Mariana akiwa anaendelea kuandika katika karatasi nyeupe.  “Haya, lakini angalia usichelewe kazini asubuhi,” alimtahadharisha.
Noel akiwa chumbani akiendelea kuandika kitabu chake katika daftari, akasikia sauti ya profesa na binti yake Mariana. “Duh! Hawa watu hawalali? alijiuliza. Noel alikuwa akiandika kwa lugha ya Kiingereza. Alipanga mara atakapokimaliza atampatia Mariana kitabu chake aweze kukichapa kupitia tanakilishi yake mpakato.
“Nina imani hataweza kukataa Mariana, aliwaza Noel kijana aliyekuwa na ndoto kubwa za uandishi tangu utotoni. Noel alikumbuka kipindi alipokuwa akisoma Shule ya Msingi Bugando, mjini Mwanza mwalimu alipozunguka darasani kuuliza watu wanataka kusoma ili kuwa kina nani baadaye. Akakumbuka namna alivyoulizwa na mwalimu na kumjibu.
“Unataka kuwa nani wewe? Noel pasipo kuyumbisha macho yake akajibu: “Ninataka kuwa mwandishi.” Jibu hilo lilimfanya mwalimu wake amuulize mara mbili mbili kwa nini alijibu vile, jibu lililokuwa tofauti na wenzake.


Asubuhi yenye kupendeza na yenye faraja kwa Noel

Noel alishituka kutoka usingizini akaweka shuka pembeni kisha akainuka na kwenda kunawa uso. Chumba kilikuwa na dawa za meno, sabuni ya kuogea, taulo na vitu vyote vilivyomwezesha kuwa nadhifu wakati huo wa asubuhi. Bomba lilikuwa kwenye sinki la kunawia uso. “Dah! Baridi sana, Noel alikuwa akiongea mwenyewe.
Lakini uso ulikuwa ni wenye furaha isiyokuwa na kifani, sebuleni Mariana na Meninda walikuwa wameshaamka. Profesa naye alikuwa ameamka, alikuwa akijiandaa kuondoka na Noel aende naye kuulizia namna utaratibu ulivyokuwa ukiendelea.
“Mariana za kuamka? aliuliza Meninda kwa furaha akiwa ameshikilia begi lake lililokuwa na tanakilishi ndani. “Unaondoka muda huu kwenda kazini? aliuliza Mariana, akimuuliza dada yake.
“Ndiyo, leo nina mambo mengi ya kufanya ofisini, alisema Meninda akionekana kuwa na haraka. “Sawa, mimi bado nipo ila baadaye nitaondoka kwenda chuoni, alisema.
Mariana alikuwa akiongea huku akiweka tanakilishi yake mezani. “Utamsalimia mwandishi, aliongea Meninda huku akiondoka, mkononi akiwa ameshika funguo za gari.
Noel alikuwa chumbani akinawa uso mbele ya sinki la kunawia ambako kulikuwa na dirisha, hivyo kilichokuwa kikifanyika nje alikuwa akikiona. Akamuona Meninda akiwa anaingia katika gari lake, Noel akashangaa: “Kumbe Meninda ana gari!
Kilikuwa ni kitu cha kushangaza kwa Noel. Meninda akafungua mlango wa gari lake, alipokuwa akifungua Noel akaona Haiwezekani, ni lazima asalimiane na Meninda, akamuita akiwa kichwa amekielekeza dirishani.
“Dada Meninda? aliita kwa sauti kisha Meninda akageuka: “Abee, Noel za kuamka? alisimama Meninda akiwa anaangalia dirishani ambapo sauti ya Noel ilikuwa ikitoka.
“Nzuri, ndiyo unakwenda kazini?” Noel alimuuliza. “Ndiyo, lakini baadaye jioni nitarudi, uwe na siku njema Noel, aliongea Meninda akiwa anaingia katika gari lake na kuondoka.
Sebuleni Mariana alikuwa amesikia sauti ya Noel, alijua wazi atakuwa ameamka kutoka usingizini. “Dah! Afadhali kama Noel ameamka ninataka anisaidie kitu hapa, alisema Mariana huku akiwa ameketi mezani akionekana mtu mwenye kufikiria kwa marefu na mapana. 
“Noel ulitaka akusaidie nini? aliuliza profesa. “Ninataka niende naye sehemu lakini pia kuna kitabu ninahitaji anisaidie kuandika, alisema.
Profesa alikuwa akimsikiliza binti yake Mariana kwa umakini. “Mimi pia ninataka kuondoka naye twende wote chuoni, alisema profesa huku akishikilia begi lake lililokuwa na tanakilishi pamoja na nyaraka mbalimbali ndani.
“Mmmh! Sasa itakuwaje baba? aliuliza Mariana. Profesa akafikiria kwa muda kisha akamwambia Mariana: “Kesho utakwenda naye, ila leo acha kwanza twende wote chuoni ili kujua utaratibu utakuwaje. Mariana akamkubalia baba yake. Profesa alikuwa na maelewano mazuri na watoto wake.
Wakiwa wanaongea, mara Noel akawa ametoka nje akiwa amejawa tabasamu usoni, mkononi akiwa ameshikilia lile daftari lake alilokuwa akiandikia wazo la kitabu chake.
Mariana alipomuona Noel alifurahi zaidi. “Noel ndiyo unaamka? aliuliza. Noel akamjibu Mariana kwa furaha: “Ndiyo, vipi za toka usiku? Mariana akamjibu kuwa yuko vizuri.
Profesa yeye alikuwa amesimama akiangalia kitu kwenye tanakilishi yake. Punde dada wa kazi akatoka na chupa ya chai akiwa ndiyo anafanya maandalizi ya meza kwa ajili ya chai.
“Noel, ujiandae, maana tutaondoka wote, alisema profesa. Noel alikuwa yuko tayari, alivaa sweta lake zito. “Mimi niko tayari, alisema Noel kisha wakasalimiana na profesa. Maisha ya Moscow Noel alianza kuona kuwa ni mazuri, ambayo yangeweza kumfaa katika uandishi wake.

Itaendelea wiki ijayo…

You may also like