Congolese workers search for rough diamonds Kangambala mine in Lunged, in the south west region of Kasai in the Democratic Republic of Congo, the heart of the diamond mining area in the DRC, August 9, 2015. Diamond buyers and manufacturers in the west are trying to find a way to make the diamond industry cleaner and more responsibly-sourced, in order to combat human rights abuses, child labor, the degradation of the environment, and unfair trade practices. (Credit: Lynsey Addario/ Getty Images Reportage for Time Magazine)
Congolese workers search for rough diamonds Kangambala mine in Lunged, in the south west region of Kasai in the Democratic Republic of Congo, the heart of the diamond mining area in the DRC, August 9, 2015. Diamond buyers and manufacturers in the west are trying to find a way to make the diamond industry cleaner and more responsibly-sourced, in order to combat human rights abuses, child labor, the degradation of the environment, and unfair trade practices. (Credit: Lynsey Addario/ Getty Images Reportage for Time Magazine)

Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Kila siku Noel alikuwa anaitwa ofisini kwa mhasibu, kusoma kwake kulikuwa kwa shaka, hakuwa na furaha. Aliishi kwa wasiwasi muda wote alipokuwa shuleni. ‘Nitafanyaje, nitafanyaje?’ ndilo lilikuwa swali lake kila mara kijana Noel. Alipokuwa akitembea kuelekea shuleni alifika sehemu yenye uwazi ambapo walionekana walimu wake wakamuita kwa sauti: ‘Noeli?’”  Sasa endelea…

“Naam! Mwalimu,” aliitikia kwa upole. Akiwa anageuza shingo yake, alikuta ni wale walimu wake ambao kila siku walikuwa wanamsumbua shuleni kutokana na madeni aliyokuwa nayo. “Aiseee ninarudi nyumbani,’’ ndilo wazo aliloliwaza kwa haraka wakati huo Noel.

Licha ya kupitia mambo yote hayo, lakini bado Noel aliamini kuwa ipo siku matatizo yatakwisha. “Wewe fedha tunayokudai umelipa?’’ aliulizwa na mhasibu wa shule.

“Hapana’’, alijibu kijana Noel. Mwalimu Mkuu aliamua kutoa agizo kuwa Noel afukuzwe shule. “Mwalimu, huyu aende nyumbani tu,’’  alizungumza akiwa ameshikilia begi la Noel.

Noel anafukuzwa kurudi tena nyumbani kwao. Kufukuzwa kwa Noel ilikuwa imekwisha kuwa kawaida. Wanafunzi wenzake ilifikia hatua waliona ni jambo la kawaida kwa Noel kurudishwa nyumbani kutokana na madeni aliyokuwa akidaiwa.

Noel akiwa njiani aliawaza: “Nirudi tena nyumbani?’’ Alijiuliza swali hilo kichwani mwake kwa dakika kadhaa, mara akapata ufahamu wa haraka. “Ngoja niende mtaani,’’ aliwaza hivyo. Hatimaye aliamua kwenda mjini.

Rafiki yake alikuwa darasani akimsubiri: “leo Noeli yuko wapi?’’ alijiuliza mwenyewe tu akilini huku akiwa anajinyoosha.

Rafiki yake Noel alionekana kutokufurahia somo la mwalimu aliyekuwemo darasani wakati huo kwa maana mawazo yake yalikuwa juu ya rafiki yake.

Noel baada ya kufika mjini alianza kujifikiria tena akilini mwake: “Nifanye nini?’’ Akili ikamjia aende kuvua nguo za shule  kisha aende kufanya vibarua atakavyokuwa akikutana navyo mitaani.

Aliingia katika uchochoro na kubadili nguo zake kwa haraka.  Alitumia kama dakika tano kuweza kubadili nguo zake na kuvaa nguo za nyumbani. Noel akiwa anatembea na kuangaza huku na kule akakutana na watu wakichimba barabara.

Wakati amesimama na kuwashaagaa wale wachimba barabara, mara mmoja wa wale wachimba barabara alimuita Noel: “Dogo vipi?’’ Alisogea karibu na Noel kisha akamwambia: “Mbona unashangaa hapa, kwanini?’’ Noel alisimama kisha akamjibu: “Mimi pia ninataka kazi,’’ alizungumza Noel kwa kujiamini.

“Wewe utaweza kweli kazi yetu?’’ aliongea huku akimtazama usoni kwa huruma kijana Noel. “Ninawaombeni hata nibebe kifusi cha mchanga.” Noel alionekana mwenye shauku ya kutaka kufanya kazi na baadaye aweze kulipwa ujira wake.

“Kama utaweza nifuate.’’ Walitembea kwa kufuatana kama kumbikumbi wakielekea Noel ambako alikuwa hapajui. Walipofika sehemu moja walikutana na bwana mmoja, akamuuliza yule mwenyeji wake Noel: “Unasemaje?’’

“Nimekutana na huyu bwana mdogo.” Yule bwana alimuangalia sana Noel kisha akamuuliza tena: “Ana shida gani?’’ ingawa hakutaja ana shida gani, mwenyeji wake Noel alimuelewa kisha akamwambia yule bwana: “Ninakuomba umsikilize.’’ Yule bwana alikubali kisha mwenyeji wake Noel aliondoka na kuwaacha wawili hao.

Mazungumzo yalianza kati ya yule bwana na kijana Noel: “Bwana mdogo ulikuwa unasemaje?’’ alimuuliza Noel, kisha Noel alimjibu: “Mimi natafuta kazi.’’ Alijibu kwa kujiamini.

Noel alikuwa kijana ambaye anajiamini sana. Yule bwana akamwambia: “Kibarua au?’’ Ilikuwa ni kama bahati, lakini ilikuwa kama mpango asilia kutoka kwa Mungu. “Ndiyo, mimi vyovyote vile’’ alisema Noel.

Basi, yule mtu ambaye alikuwa mkubwa pale aliamua kumpeleka sehemu ili aweze kumpa kibarua cha kubeba mchanga wa moramu na kuwapelekea mafundi.

Kazi ile haikuwa nyepesi, ilikuwa ngumu, isivyo kawaida. “Fanya kwa leo nitakulipa Sh elfu 35,’’ alisema yule bosi wa pale, kisha akaondoka na kumuacha. Noel baada ya kusikia atapewa donge nono kama hilo alijituma kwa bidii sana katika kazi yake, huku akiwa na matumaini mengi moyoni mwake: “Kumbe ngoja nijitume,” alijisemea peke  yake.

Mama yake muda huo alikuwa akiuza pombe kilabuni, suala la shule kwa mwanae alikuwa halifuatilii. Noel alijikita katika kufanya kazi yake jua lote likimuishia mwilini. Jasho lilikuwa likimtoka mwilini kwa wingi. Alijitahidi kubeba mifuko mikubwa ya mchanga wa moramu lakini imani yake katika mafanikio ilimfanya kujituma bila kuchoka.

Huku akiamini ipo siku atakwenda kuuacha umaskini, Noel hakuwahi kujiwazia mabaya hata siku moja, kila gumu alilokuwa akipitia aliliona kama changamoto na kuona sehemu ya kujifunza zaidi.

Mama Noel alikuwa akifuata maji huku akiuza pombe, alifanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Wateja wake wa pombe walikuwa ni makuli pamoja na makondakta waliokuwa wakitokea maeneo mbalimbali ya mji wa Mwanza.

Mama Noel alikuwa mwanamke ambaye ni mchakalikaji katika kazi. “Mama Noel habari?’’ alimsemesha mmoja wa wateja wake. Mama Noel akamjibu: “Salama.’’ Alikuwa na ukaribu na wateja wake. “Niachie pomnbe ya leo,’’ walizungumza walipokutana njiani Mama Noel akiwa amebeba ndoo ya maji kichwani.

Kutokana na biashara hiyo, Mama Noel alikuwa mtu maarufu mtaani, hakuna aliyekuwa hamjui. Pesa aliyokuwa akiipata katika biashara yake ilikuwa ni sawa anagawana na askari. Alikuwa na siku nyingi sana hajawapelekea pesa ya hongo polisi kutokana na biashara yake kuwa ngumu.

Akiwa njiani kurudi nyumbani, askari nao walikuwa wameshafika nyumbani kwake, tena wakiwa  wenye hasira isiyokuwa na kifani. “Weka ndoo chini tuondoke,’’ walisema askari hao wakiwa wamemsubiri kwa muda mrefu.

Mama Noel kabla ya kuweka ndoo ya maji chini, ilibidi aanze kujitetea: “Biashara ni ngumu,” alijitahidi kujitetea lakini hakuna aliyemsikiliza, hoja zake waliona kama hazina nguvu ya ushawishi.

Askari wale walichokuwa wakikifanya kilikuwa ni kitu haramu, ingawa pia biashara ya Mama Noel ilikuwa ni haramu vilevile. Mama Noel kwa kutokufahamu haki zake aliona kama ni sawa. “Naomba mnipatie muda kidogo,” alisema Mama Noel.

Askari wakajibu: “Haiwezekani, unatuchezea wewe mama!’’ walisema wale askari, wote kwa pamoja wakiwa na msimamo sawa. “Leo ni lazima twende wote kituoni, haiwezekani,” alisema mmoja wa askari hao.

Mama Noel baada ya kusikia hivyo alizidi kuchanganyikiwa, askari walimuangalia kwa sura za kikatili, huruma kuhusu yeye ilikuwa haipo.

Mama Noel akaamua kutua ndoo ya maji chini kisha akafungua kitenge chake na kutoa pesa zake zote za mauzo madogo ya siku hiyo aliyokuwa ameyapata na kuwapa wale askari.

“Kumbe unatuchezea akili zetu?’’ walimuuliza huku wakimpa vitisho. “Hapana jamani, pesa hakuna,’’ alisema huku akiwa anajuta kutoa pesa yote ya mauzo yake ya siku hiyo.

“Sasa tukiwa tunakuijia utatu…’’ walisema wale askari huku wakigawana na kuweka mifukoni mwao pesa ambayo walikuwa wamepewa na Mama Noel.

Baada ya kumaliza walichokuwa wanakitaka waliamua kuondoka, walimuacha Mama Noel akiwa anawaza mikono yake ameiweka kichwani.

“Dah! Biashara hii sasa mbona inaendelea kufilisika,’’ aliwaza kichwa kikawa na msongo wa mawazo. Siku hiyo ilikuwa ngumu kwa Mama Noel kutengeneza pombe nyingine, kwa kuwa hakuwa na pesa hata senti moja. Wateja wake walianza kuja mmoja baada ya mwingine, alihisi Mwenyezi Mungu hathamini uwepo wake katika dunia hii.

By Jamhuri