Kwanza, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wote waliokuwa nasi katika kipindi cha mpito wa magumu ya kifo cha mwenzetu, Godfrey Dilunga.

Miji na kaya zetu zimezizima kwa baridi ya simanzi kutokana na kifo chake. Hili limetokea kama ambavyo sisi wenye imani za kidini tunavyoamini lililopangwa na Muumba hakuna wa kulipinga.

Japo nipo mbali na nyumbani, lakini nimefarijika kwa idadi ya watu waliohudhuria sherehe zake za mwisho. Marehemu alikuwa mtu wa watu, na nina imani wote waliokuja walimuombea afua ya kauli thabiti na upungufu wa adhabu kama itakuwepo.

Bado tuendelee kumuombea, kwani katika kipindi cha maisha yake amefanya mambo mengi kwa jamii hata kama kuna watu wachache hawakuyaona.

Marehemu ametumia muda mwingi na kalamu nyingi katika maisha yake kutuandikia mambo ya msingi kwa hatima ya taifa letu. Yapo ambayo aliandika na baadhi ya watu wachache waliokuwa wakienda kinyume cha utaratibu wa taifa na siasa aliwakera, hiyo peke yake kama ilitokea basi ni suna kwa mwenzetu na amekamilisha kazi na safari, daima tutamkumbuka kama mwenzetu katika tasnia na mwenzetu katika vita ya bunduki aina ya kalamu.

Ukweli ni kwamba jambo hili limehuzunisha na kunifanya leo nishike kalamu na kuandika juu ya kupunguza msongo kwa kuwa maisha ni safari ndefu ambayo tunapaswa kufurahia kila siku na kushukuru kwa kila jambo wakati huohuo tukijiandaa kwa safari, kwa kuwa hapa duniani tu wapitaji tu, hatuna kitu cha kuacha kwa ajili ya wengine, kwa kuwadhulumu wengine, siku ikifika tutaondoka peke yetu na sanda zetu kama mwenzetu alivyotangulia salama.

Dunia ya Tanzania kwa siku za hivi karibuni imegubikwa na wimbi zito la fikra ambazo ni dhahiri zinaweza zikawa chanzo cha msongo wa mawazo kama hatutakuwa makini. Msongo wa mawazo unamkumba mtu yeyote ambaye amepata kitu kwa njia isiyo rasmi au amekosa kitu kwa njia isiyo rasmi, hii ni moja tu ya sababu za msongo.

Hapa kwetu kumeibuka kundi kubwa la watu, hasa huko mijini kujiingiza katika mambo ambayo hayatuhusu na hayana faida yoyote kwetu kama familia. Watu tuna haki ya kuhoji mambo ya kijamii lakini hatuna haki ya kuongeza msongo kwa kuhoji mambo binafsi ya mtu binafsi au hata yale yaliyokubaliwa na wengi, dhana ya wengi wape inapaswa kuheshimiwa.

Nimeshuhudia mambo makubwa ambayo labda hatukupaswa kuanza kufikiria na kuzusha mjadala wa kitaifa wakati ni mambo binafsi.

Mfano, suala la mnada wa viboko, sikuelewa kwanini litamalaki katika vichwa vya watu kiasi cha kuwafanya wakose usingizi. Sasa viboko labda bado hawajapigwa mnada au wameshapigwa mnada lakini uliyekuwa unawaza hujamnunua hata mmoja au hata kula nyama yake, sielewi tunanunua msongo kwa jambo kama hili kwa sababu gani.

Zinaibuliwa tetesi na wanaojiita wanasiasa wakubwa ambazo hazijathibitishwa au hazina ukweli wowote. Badala ya kupuuza na kuwaachia wenye jukumu la kufuatilia tunajigeuza kuwa vyombo vya ufuatiliaji mpaka tunafikia hitimisho, matokeo yake tunapata msongo na kuanza kulaumu hata mambo ya msingi kwa mustakabali wa taifa letu.

Huu msemo wa hii ni nchi yetu wote, lazima mtu atete jambo fulani, sioni kama una tija kwa taifa letu. Kunaibuka wanaharakati na wanasiasa waongo wanaotaka kupata umaarufu kwa kufanya hesabu za magazijuto na kututoa katika reli kama taifa la pamoja tunaopaswa kusafiri pamoja, tunawachukia wenzetu wachache bila sababu za msingi na zisizo na mashiko, zaidi ya kujenga chuki za misongo kwa yale yaliyoibuliwa.

Baada ya mwenzetu Dilunga kutangulia mbele ya haki ndipo nilipogundua kuwa maisha ni mafupi sana, sijui kama alikuwa na msongo ambao labda uliwahi kumpotezea siku moja ya kuwa na furaha katika siku zake za kuishi hapa duniani.

Hakuna mwenye hakika ya akiba ya siku zake zilizosalia katika gimba hili liitwalo duniani, tuache kupeana misongo kwa mambo ya uzushi ili siku zetu zihesabike katika fungu la furaha.

Sina hakika kama nimeeleweka, lakini cha msingi tupunguze unafiki, uzandiki na megineyo na tufanye maisha mazuri. Tupafanye duniani kuwa mahali pazuri pa kupita, hakuna atakayeishi milele na hakuna atakayeweza kufanya jambo lolote kinyume cha mapenzi ya Muumba.

Wasalamu,

Mzee Zuzu, 

Kipatimo.

By Jamhuri