Mafanikio katika akili yangu (20)

Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Mchungaji hawa ndio wanaua vipaji vya watu,’’ alisema Zawadi akiwa anaendelea kuchora. “Ni kweli wamempotezea muda sana Noel, hawakuwa wanamlipa na atakuja kufanya mambo makubwa, watamhitaji zaidi,’’ yalikuwa maneno ya mchungaji akimwambia Zawadi. Mama yake Noel alifika na birika lenye maji kisha akamnawisha mchungaji mikono kwa ajili ya kula chakula. Sasa endelea…

***

Noel akiwa amekaa sebuleni peke yake mara Mungu akampa wazo, akakumbuka kuitumia barua pepe yake. Akanuia kufanya jambo hilo kisha akaamua kuondoka pale mezani na kwenda moja kwa moja hadi mlangoni kwa Meninda. Akagonga mlango, Meninda akiwa chumbani kwake alikuwa bado hajalala alikuwa anasikiliza muziki wa injili katika kompyuta yake. Akasikia mlango ukiwa unagongwa, akatoka kitandani kwenda kufungua mlango. “Kumbe ni Noel,’’ alisema Meninda kwa tabasamu. “Ndiyo dada Meninda, ninataka uniazime kidogo kompyuta yako niingie kwenye barua pepe yangu.’’

Meninda akamkubalia, akarudishia mlango na kuifuata kompyuta yake kitandani, akatoka nayo kisha wakarudi mpaka mezani wote wawili. “Unataka kupitia barua pepe yako?’’ aliuliza Meninda. “Nina siku nyingi sijaitumia,’’ alisema Noel. Meninda akampatia Noel atumie kompyuta yake. Nyumba ya profesa ilikuwa imeunganishwa na mtandao, hivyo Noel akafungua mtandao na kuanza kuperuzi barua pepe yake.

Noel akafungua barua pepe yake akakuta ujumbe ule aliokuwa ameandika mhariri wa makala ambazo Noel alikuwa akiandika pindi akiwa nchini Tanzania. 

Noel akawa makini kuusoma ujumbe ule ulioandikwa: “Kijana Noel mbona hutumi kazi zako tena na simu yako haipatikani, tuma tutakuwa tunakulipa kwa sasa.’’ 

Noel akashituka huku sura yake ikionekana yenye tabasamu. Meninda akamuuliza: “Noel mbona umetabasamu hivyo? Niambie nami nitabasamu.’’ Noel akaendelea kutabasamu kisha akamjibu Meninda: “Kuna mhariri wangu nchini Tanzania anataka niendelee kumtumia makala atanilipa.” Meninda naye akafurahia. “Ni vizuri, kwani walikuwa hawakulipi?’’ aliuliza Meninda huku akishangaa. “Walikuwa hawanilipi, nilikuwa ninawaandikia bure,’’ alisema Noel. Meninda akasikitika kisha akamwambia: “Mpaka wametaja kukulipa fedha wameona thamani yako.’’ 

Noel aliujibu ujumbe huo katika barua pepe ya mhariri: “Sawa, haina shida, malipo ni shilingi ngapi kwa kuwa mimi sipo Tanzania kwa sasa, nipo Moscow nchini Urusi?” Kisha akautuma. Aliendelea kuhamasika akiamini uandishi utaanza kumletea fedha kama alivyokuwa akihitaji kutokana na matamanio yake ya muda mrefu.

Noel alianza kukumbuka siku za nyuma akiwa katika mji wa Mwanza alikutana na binti mmoja aliyekuwa hamfahamu. Walikutana tu sehemu Noel akiwa na kipaza sauti cha kurekodia matukio akimwelezea changamoto alizokuwa anakutana nazo, binti alimpa maneno yenye faraja na matumaini.

“Usijali kijana, utafanikiwa siku moja watu watakuheshimu kupitia hiki unachokifanya,’’ yalikuwa maneno ya yule binti. Siku hiyo Noel akaona kile alichokisema yule binti ni kama kinatimia katika wakati ambao hakuwa anajua wala kufikiri kama itakuwa vile.

“Kumbe Noel una barua pepe?’’ aliuliza Meninda, huku akiwa anatazama Noel alivyokuwa akibonyeza kompyuta yake kisha Noel akamjibu: “Ndiyo ninayo, mji niliokuwa naishi ulikuwa mbali na ofisi za gazeti, hivyo nililazimika kuwa na barua pepe ya kurahisisha makala kuwafikia kwa haraka na kwa wakati.’’ 

Noel alikuwa amewahi kujifunza kutumia kompyuta mapema, mambo kadha wa kadha yalikuwa hayampigi chenga katika utumiaji wa kompyuta. “Ulikuwa unajitahidi sana nguvu yako uliyoitumia Mungu atailetea mafanikio makubwa mbeleni,’’ alisema Meninda. 

Maneno ya Meninda kwa Noel mara nyingi yalikuwa ni maneno yenye faraja na hamasa kubwa kwa Noel. Yalikuwa kama dawa lakini pia ilikuwa ni mbegu ya ushindi iliyokuwa ikiendelea kupandikizwa kwa Noel.

***

Profesa alikuwa amekaa chumbani kwake akipitia tafiti za wanafunzi aliokuwa anawasimamia katika zoezi hilo. Alikuwa akiwasikia Meninda na Noel wakiongea. Profesa alifurahi, maana alihitaji Noel afanye kile alichokuwa amesikia wakiongea na Mariana kuhusu kuandika vitabu vingi, ingawa alikuwa hajasema lakini lilikuwa ndilo tamanio lake kubwa siku za baadaye kuona hilo likifanyika.

“Noel natamani ainuke na afike mbali zaidi’,’ alikuwa akiongea mwenyewe. Profesa alimkumbuka mke wake aliyekuwa nchini Marekani akifanya kazi katika Shirika la Haki za Binadamu (HUMAN RIGHTS WATCH). Profesa akaamua kumpigia simu mke wake. Simu iliita kwa muda kisha mke wa profesa akapokea.

“Mke wangu habari za huko USA?’’ Mke wake muda huo alikuwa ametoka katika kikao. “Ni nzuri, ninapambana na kazi mume wangu, Meninda na Mariana hawajambo?’’ aliuliza mke wa profesa akiwa ameikumbuka familia yake iliyokuwa katika Jiji la Moscow. “Pole, hata mimi nipo ninasoma tafiti za wanafunzi wangu,” mke wake profesa aliongea mengi ya kifamilia na hata mambo yaliyohusu kazi.

“Lakini mume wangu nina safari ya kwenda Afrika,’’ alisema mama yake Meninda. “Afrika unakwenda kufanya nini mke wangu?’’ aliuliza profesa kutaka kujua. “Ni safari ya kikazi nchini Tanzania,” alisema.