Akisoma Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Bungeni-Dodoma, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa Kilovoti 400 na kituo kipya cha kupoza umeme cha Chalinze cha Kilovoti 400/220/132 na kimeanza kutumika kuingiza umeme katika Gridi ya Taifa.

Aidha, amesema Serikali imekamilisha Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa Kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 414 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Babati na Arusha ambapo gharama za mradi huo ni dola za Marekani milioni 258.82 na umeme tayarin unasafirishwa kutoka Singida hadi Arusha.

Ameeleza kuwa mradi huo utawezesha kuiunganisha Gridi ya Taifa na Nchi za Afrika Mashariki (Eastern Africa Power Pool – EAPP).

Kwa upande wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Iringa kupitia Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga pamoja na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Kisada (Iringa), Iganjo (Mbeya), Tunduma na Sumbawanga amesema umefikia asilimia 27 ya utekelezaji ambapo gharama za mradi huu ni dola za Marekani milioni 615.

Ameeleza kuwa, mradi huo unalenga kuunganisha Gridi ya Taifa na nchi za Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool – SAPP).

Kwa upande mwingine, ameeleza kuwa Serikali imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 132 kutoka Malagarasi hadi Kidahwe mkoani Kigoma. Kazi hii inaenda sambamba na kazi ya 16 ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 49.5 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Malagarasi.