Na Suzy Butondo, JamhuriMedia, Shinyanga

Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Shinyanya chini ya mwenyekiti wake Mabala Mlolwa kimemvua madaraka mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana UVCCM Wilaya ya Shinyanga mjini Jonathan Agustino Madete kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Juni 13,2024 Katibu wa Siasa Uenezi na Mafunzo Mkoa wa Shinyanga Richard Masele amesema kikao cha Hlmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Shinyanga kimemvua madaraka mwenyekiti huyo kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Jonathan Madete aliyekuwa mwenyekiti UVCCM

Masele amesema Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa imeadhimia kwamba haitamfumbia macho wala kumvumilia mtu yeyote kiongozi au mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi atakayevunja kanuni, taratibu na katiba ya chama hicho.

“Kamwe chama chetu hakitamfumbia macho wala kumvumilia mtu yeyote, kiongozi au mwanachama wa chama cha mapinduzi atakayevunja kanuni, taratibu na katiba ya chama chetu, hatua za kinidhamu zitachukuliwa mara moja, hii ni pamoja na kulinda heshima ya chama chetu na jumuiya zake na kuhakikisha misingi ya chama hiki na miongozo inaendelea kuheshimwa chini ya mwenyekiti wetu mahiri Rais Samia Suluhu Hassan ,”amesema Masele.

Masele amesema Chama cha Mapinduzi na jumuiya zake kina miongozo yake na kinahakikisha misingi ya chama hiki na miongozo inaendelea kuheshimiwa chini ya mwenyekiti mahiri, mchapa kazi na mzalendo wa kweli Rais Samia.

Katibu wa Siasa Uenezi na Mafunzo Mkoa wa Shinyanga, Richard Masele akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo Mkoa wa Shinyanga Richard Masele.