Mafanikio ya ziara ya Rais Samia aliyofanya Doha nchini Qatar na New Delhi India

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura Yunus akizungumza na kuwaelezea Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya Doha nchini Qatar na New Delhi India. Mkutano huo na Waandishi wa Habari umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Oktoba, 2023.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya New Delhi nchini India katika sekta ya Afya. Mkutano huo na Waandishi wa Habari umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Oktoba, 2023.
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akizungumza kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya New Delhi nchini India katika sekta ya Kilimo. Mkutano huo na Waandishi wa Habari umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Oktoba, 2023.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akizungumza kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya New Delhi nchini India katika sekta ya Maji. Mkutano huo na Waandishi wa Habari umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Oktoba, 2023.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye Mkutano wa kuelezea kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya Doha nchini Qatar na New Delhi India. Mkutano huo na Waandishi wa Habari umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Oktoba, 2023.
Waandishi kutoka Vyombo mbalimbali vya Habari nchini wakiwa kwenye Mkutano wa kuelezea kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya Doha nchini Qatar na New Delhi India. Mkutano huo na Waandishi wa Habari umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Oktoba, 2023.

……………………………………….

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alifanya ziara ya kitaifa nchini India kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya India, Mhe. Droupadi Murmu, kuanzia tarehe 8 – 11 Oktoba, 2023.

Lengo la ziara ilikuwa ni kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na India, hususan katika sekta za kimkakati kama afya, viwanda, biashara, ulinzi na usalama, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchumi wa buluu, maji, na kilimo.
Lengo la pili ilikuwa ni kutangaza fursa za biashara na uwekezaji za Tanzania ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka India.


MAMBO 3 MAKUBWA
Katika siku 3 za ziara hiyo, mambo makubwa 3 yamefanyika.
LA KWANZA Rais Samia kupokelewa kitaifa na kwa heshima zote Ikulu ya India na kupokelewa na Rais wa nchi hiyo Mhe. Murmu na pia Waziri Mkuu Narendra Modi.
Mazungumzo ya Rais Samia na Mhe. Modi yalilenga kupandisha hadhi ya mahusiano ya nchi hizi mbili na kuwa STRATEGIC PARTNERSHIP, au Ushirika wa Kimkakati.
Msisitizo wa ushirikiano ni katika ulinzi hasa kutoa mafunzo, nishati na madini ambapo India imeonesha nia ya kutoa mafunzo kwa wahandisi, hasa wa masuala ya madini, usalama/Ulinzi wa majini au MARITIME SECURITY, biashara na uwekezaji, kujengeana uwezo, elimu na teknolojia hasa usalama wa mitandao na namna ya kuwashirikisha vijana kwa kuwapa elimu ya teknolojia. Na pia kwa kile kinachoitwa Big Cat Alliance, yaani namna ya kulinda wanyama wa jamii ya paka kama vile chui nk. Mengine ambayo yamepewa kipaumbele ni afya kilimo, maji.
Vile vile kulitiwa saini hati za makubaliano 15 zenye nia ya kuimarisha ushirikiano zaidi na India. Viongozi wa pande mbili walibadilishana hati hizo zikishuhudiwa na Rais Samia Pamoja na Waziri Mkuu wa India Mhe. Modi. Hati 10 ni baina ya taasisi za serikali na hati 5 za sekta binafsi.
Hati hizo za makubaliano zaidi ni Wizara ya Afya na taasisi za afya za India, uimarishaji wa masuala ya kidijitali, ushirikiano wa masuala ya kiutamaduni, kongani za viwanda, Kituo Cha Uwekezaji ya Tanzania (TIC) kimetia saini kushirikiana na taasisi ya India. Pia kumetiwa saini ya kushirikiana katika ujenzi na ukarabati wa vyombo vya majini na masuala mengine.
Kwa upande wa sekta binafsi, Chemba ya Biashara ya Viwanda na Kilimo imeingia takriban makubaliano matatu na ile ya India na Chemba ya Biashara ya Zanzibar nayo imeingia makubaliano na Chemba ya chakula na Kilimo ya India.
LA PILI ni Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya India na Tanzania. Rais Samia alikuwa mgeni rasmi katika Jukwaa hilo lililohudhuriwa na wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji wa India.
India ni mdau mkubwa wa biashara na uwekezaji wa Tanzania ambapo hadi kufika sasa, Tanzania ni nchi ya nne kwa kufanya biashara na India barani Afrika. Ujazo/kiwango wa biashara kati ya Tanzania na India ni Dola za Kimarekani bilioni 3.13 mwaka 2022 ukilinganisha na Dola za Kimarekani bilioni 2.14 mwaka 2017.

Nchi hizo mbili pia zilibadilishana tena hati za makubaliano 4 na nyingine 7 kupitia sekta binafsi. Baadhi ya hati hizo ni kwenye sekta za afya, uwekezaji na kilimo.

Kama nilivyosema awali, kuna sekta nyingi zimefanya mazungumzo ila nitataja chache tu.

AFYA
Tukizungumzia afya, tayari India imeshirikiana sana na Tanzania kwa kutupa utaalamu wa huduma za ubingwa bobezi, ikiwemo kupandikiza figo (KIDNEY TRANSPLANT) Pamoja na upandikizaji wa uloto (bone marrow) lakini kumekuwa na majadiliano ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Tanzania kuweza kufanya upandikizaji wa ini.
Jambo jingine kubwa kwenye sekta ya afya linaihusu hospitali ya Apollo ya India. Apollo ina mtandao wa hospitali 73 nchini India na imekubali ombi la serikali ya Tanzania kufungua tawi la Appollo nchini ili kusogeza huduma zao karibu na Watanzania wengi zaidi.


Kipaumbele kikubwa cha Tanzania katika ziara hii ilikuwa ni dawa, ambapo kuna uhitaji mkubwa nchini. Kiwango cha dawa kinachozalishwa Tanzania ni kidogo ukilinganisha na mahitaji, kwani asilimoa 80 ya dawa hununuliwa nje ya nchi ambapo asilimka 60 hutoka India.

Hivyo katika mazungumzo na wenzetu wa India, Tanzania imesisitiza umuhimu wa Wafamasia wa India kuzalisha humu humu nchini. Na hilo likifanikiwa ina maana hatua hiyo italinufaisha soko la Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Kusini mwa Afrika (SADC).
Aidha, India na Tanzania zimekubaliana kuanzisha kituo cha tiba asilia nchini.

KILIMO
Kama tunavyojua, Rais Samia ameongeza bajeti mara dufu katika sekta ya kilimo na pia jitihada nyingi zinaendelea kufanyika kushawishi hususan vijana kuingia kwenye kilimo kwa mfano mradi wa BBT. Kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa teknolojia kwenye kilimo, uzalishaji wa soko la uhakika, mitaji na uwekezaji kwenye miundombinu ya umwagiliaji.

Katika ziara hii, Tanzania imefanikiwa kupata uhakika wa soko la mbaazi na Rais Samia ameomba kupata allocation yaani kupatiwa soko la mgawo wa uhakika wa tani laki mbili kwa kuwa India ni mtumiaji mkubwa wa mbaazi duniani.
Nchi ambazo zimepata fursa ya mgao kama huo ni Malawi na Msumbiji kutoka India, hivyo sisi ni wa 3 kutoka Afrika.


Serikali ya Tanzania imewasilisha mahitaji kwenye serikali ya India, kupitia Exim Bank ya India kwa ajili ya mradi mkubwa wa umwagiliaji kutoka Ziwa Victoria. Mahitaji hayo ni takriban dola Bilioni moja ambao mradi huo utatekelezwa mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida, Dodoma, Kagera na Mara.

Pia Serikali ya Tanzania ina mpango wa kununua jumla ya trekta elfu 10 na kujenga vituo maalum vya vifaa vya kilimo (mechanization). Serikali imekubaliana na makampuni makubwa 2 duniani ya matrekta, Mahindra na John Deer kuweka katika kipindi cha miezi 12 viwanda vya kuunganisha matrekta na kutengeneza vipuri ndani ya Tanzania.

MAJI
India ni wadau wetu muhimu katika sekta ya maji kwa kushirikiana na serikali walishatoa mkopo nafuu wa Dola Milioni 500 za Kimarekani zinazotumika kutekeleza miradi ya maji katika miji 24 nchini. Utakapokamilika utanufaisha takriban Watanzania milioni 6 kupata maji safi na salama.
Hata hivyo Rais Samia ameonyesha nia ya kutaka kuyatoa maji Ziwa Victoria kupeleka Singida mpaka Dodoma na ndio yaliojadiliwa katika ziara hii.

ULINZI
Tukizungumzia sekta ya ulinzi, nchi hizi mbili zinatambua umuhimu wa kushirikiana kwenye teknolojia (technology transfer), kujengeana uwezo, mafunzo ya jeshi kwa pamoja na kubadilishana utaalamu na uzoefu.

Tanzania na India pia zimeamua kuendelea kushirikiana kwenye usalama wa majini, biashara za majini na kukuza uchumi wa buluu.
Kwa upande wa usalama wa majini, India na Tanzania zimekuwa zikishirikiana kwenye kupiga doria, kujengeana uwezo na kubadilishana taarifa katika kupambana na vitisho kama uharamia, uvuvi haramu na usafirishaji wa dawa za kulevya. Yote haya yanafanyika kulinda usalama wa eneo la Bahari ya Hindi.

UCHUMI WA BULUU
Uchumi wa buluu nao ni kipaumbele kwa Tanzania ambapo inahusu kutumia rasilimali zilizomo majini kwa ajili ya kukuza uchumi, kuongeza ajira na pia kutunza mazingira. Miongoni mwa Hati za Makubaliano zilizosainiwa nayo ipo ya kushirikiana katika masuala ya White Shipping, yaani kubadilishana taarifa kuhusu meli, kuhakikisha kuna usalama majini na utulivu katika eneo.
Mbali na hayo baadhi ya wawekezaji na wafanyabiashara wameonesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye sekta ya madini, ikiwemo chuma na makaa ya mawe. Lakini pia nchi hizi mbili zimekubali kushirikiana kwenye kutoa mafunzo hasa uhandisi wa madini, masuala ya fedha, kuongeza thamani kwenye bidhaa mbalimbali ikiwemo pamba, ubanguaji wa korosho, kujenga kiwanda cha sukari, kuwekeza kwenye eneo la mafunzo na utafiti, vilevile uzalishaji wa mbegu bora kwa kushirikiana na taasisi ya hapa Tanzania, TARI. Baadhi ya wawekezaji wa India pia wameonyesha nia ya kujenga Vyuo vya ufundi na Uanzishwaji wa mabenki kwa kuanzia takriban matawi Matano hadi baadae kufikia 25.


YALIYOFANYIKA KABLA ZIARA
CHUO CHA IIT

Jambo zito kwenye suala la Eeimu ambalo India imefanya ni kuanzisha kampasi yenye hadhi ya juu ya Chuo cha Teknolojia (IIT) Madras, Zanzibar inayotarajiwa kuanza mwezi huu Oktoba. Ni Kampasi ya kwanza ya Chuo hicho nje ya India. Chuo hichi ni maarufu sana na imetoa wataalamu wanaofanya kazi kwenye sekta hiyo ya Teknolojia maeneo mbalimbali duniani.

USAFIRI WA ANGA
Safari za ndege kutoka jijini Dar es Salaam hadi Mumbai, India hadi sasa ni mara nne kwa wiki. Hivi karibuni shirika la ndege la Tanzania litaanza safari mpya kati ya New Delhi na Dar es Salaam na hivyo kufanya jumla ya safari nchini India kuwa 5.

SHAHADA YA HESHIMA
Rais Samia Suluhu Hassan alipewa hadhi ya juu kwani kama mlivyoona alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru.
Rais Samia amekuwa ni mwanamke wa kwanza kupewa Shahada hiyo kutoka chuo hicho na ni kiongozi wa tatu kupewa heshima hiyo. Kiongozi wa kwanza kupewa shahada hiyo ni Rais Vladimir Putin wa Urusi na wa pili ni Waziri Mkuu wa Japan, Hayati Shinzo Abe.