Padre Dk. Faustin Kamugisha

Sala na kazi ni sababu ya mafanikio. “Sali kana kwamba kila kitu kinamtegemea Mungu, na fanya kazi kana kwamba kila kitu kinakutegemea wewe,” alisema Mt. Augustino wa Hippo Afrika ya Kaskazini. Kanuni hii ya mafanikio kwa Kilatini ni: Ora et labora yaani Sali na Fanya kazi au Sala na Kazi. Kanuni hii ilisaidia kuleta maendeleo uko Ulaya katika nyanja za kilimo na utengenezaji wa nguo. Sala ilitafsiriwa katika vitendo. Methali ya Kiafrika inasema yote: “Unaposali tembeza miguu yako.” Sali na enda kufanya kazi. Ukweli huu unaweza kueleweka vizuri katika mtazamo wa Mama Teresa wa Calcutta aliyesema: “kazi haisimamishi sala na sala haisimamishi kazi.” Tatizo tunalolipata katika Afrika kwa baadhi ya watu ni kama sala zinasimamisha kazi wiki nzima kwa maana kanuni ya sala na kazi haifuatwi vizuri.

Umuhimu wa kanuni hii Sala na Kazi unaonekana pale ambapo taasisi nyingi duniani zimechukua maneno hayo kama motto au kauli mbiu. Mfano, Chuo Kikuu cha Dalhousie kilichoanzishwa mwaka 1818 kilichukua maneno hayo: Ora et Labora  kama kauli mbiu yake au motto yake mwaka 1870. Licha ya taasisi hata baadhi ya watu wamechukua maneno hayo kama taa ya kuwaongoza. Alexander Maclaren alipoulizwa juu ya siri ya mafanikio alisema: “Nimegundua kuwa faraja yangu na umahiri wangu vimekuwa katika uwiano wa moja kwa moja na wingi na kina cha mawasiliano yangu ya kila siku na Mungu. Siri ya mafanikio katika jambo lolote ni kumtumainia Mungu na kufanya kazi kwa bidii.” Ni kama Bwana Alexander Maclaren alikuwa akisema kuwa hakuna mafanikio ya kweli nje ya Mungu. Ni sala na kazi.

Mwaka 1994 Gazeti liitwalo The Dallas Morning News lilifanya utafiti kwa kuhoji watu wazima 1,011  kazkazini mwa Texas juu ya imani yao. Asilimia themanini na saba (87%) ya waliojibu maswali walisema wanaamini sala inazaa matokeo. Wanawake asilimia tisini na tatu (93%) waliamini katika sala. Wakilinganishwa na wanaume asilimia  themanini (80%) ambao huamini katika sala.

Wanyankole wa Uganda wana msemo husemao: ukishinda kwenye mambo ya Mungu Mungu anashinda kwenye mambo yako. Msemo huu hauna maana ya Mungu kukufanyia kila kitu, wewe ukishinda umepiga magoti. Katika familia moja kuna mama aliyemwombea jirani yake Mungu amsaidie walau apate hela ya kidogo ya chakula. Alipomaliza kusali, mtoto wake alichukua pochi ya mama yake na kutoa elfu hamsini na kusema: “Mama mambo madogo madogo usimsumbue Mungu, mimi nampelekea pesa hii yako.” Sala itafsiriwe katika matendo.

Kusali na kufanya kazi ni kushinda kwenye mambo ya Mungu. Kufanya kazi ni kufanya kazi ya Bwana, kusali ni kuzungumza na Bwana wa kazi. Mungu anahitaji usaidizi. Tuchukulie mfano wa kuumbwa kwa mwanamke kuwa msaidizi. Haina maana mwanaume afanyiwe kila kitu kwa vile mwenzi wake ni msaidizi. Usaidizi huu una barabara mbili kwa wote: barabara ya kwenda na kurudi, barabara ya kutoa na kupokea, kupoteza na kupata. Inasemwa Mungu anawalisha ndege wa angani lakini hawawekei chakula kwenye kiota wanatafuta. Mungu anatupa nazi lakini hatukunii, inabidi unjikunie. Mt. Augustino wa Hippo alisema: “Uwe tayari japo Mungu ni mtoaji kwa wote; anatoa kwa Yule aombaye, ili asije akampa mtu asiyeweza kupokea.”

Kabla ya kufanya kazi ya Bwana, kaa na Bwana wa kazi. Kabla ya kukutana na watu, kutana na Mungu. Kabla ya kuzungumza na watu, zungumza na Mungu. Kabla ya kutumia watu ujumbe, mtumie Mungu ujumbe. “Sala ni kujiweka katika mikono ya Mungu” (Mama Tereza wa Calcutta). “Sala ni kutojiweza kunajitupa kwenye Mamlaka, ni ulemavu unaogemea  Nguvu, ukosefu unaofikia Huruma, ni mfungwa anayetafuta Uhuru (Askofu Fulton Sheen).

Please follow and like us:
Pin Share