WAZIRI mkuu wa Tanzania,Kasimu Majaliwa amewataka  Watumishi wa serikali kuacha urasimu pindi wanapohudumia wananchi badala yake wahudumie wananchi na kutatua kero zao kwa wakati. 

Ameyasema hayo leo mkoani Arusha wakati akifungua mkutano mkuu wa 14  wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za MitaaTanzania (TOA) unaofanyika kwa muda wa siku tatu mkoani Arusha .

Majaliwa amesema kuwa, kumekuwepo na urasimu mkubwa sana ambao umekuwa ukifanywa na viongozi hao kwa wananchi pindi wanapofika maofisini  kuleta kero zao na badala yake kupigwa kalenda  kwa lengo la kutengeneza mazingira ya rushwa. 

“Nawaombeni sana muondoe  urasimu muache  tabia  ya kuomba rushwa kwa wananchi wanaohitaji haki zao ,kwani kumekuwepo na miongoni mwenu badala ya kuyashughulikia  matatizo ya wananchi kwa wakati mnawapa maneno magumu kama ” bado  tunafanya tathimini “,mchakato bado,tunafanya upembuzi yakinifu waache kutosha wananchi kwa kuwapa maneno magumu kama hayo ambayo yanawakatisha tamaa na kutengeneza mazingira ya rushwa “amesema Majaliwa. 

Aidha amewataka watumishi hao kuacha kukaa maofisini kuanzia jumatatu hadi ijumaa na kusubiri wananchi kuleta kero zao bali watenge  siku ndani ya wiki na kufuata wananchi  katika maeneo yao ya vijijini kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuweza kuzifanyia  kazi kwa wakati .

Aidha Majaliwa amesisitiza kwa Watendaji hao kuhakikisha wanadhibiti  kikamilifu upotevu  wa mapato na wizi kwenye halmashauri na kupitia mkutano huo wajadili  na kuweka mikakati namna ya kwenda kudhibiti mapato kwenye halmashauri zote nchini.

Ambapo amewataka kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma huku wakifanya kazi kwa bidii na kutanguliza weledi na kizalendo mbele kwani ndio majukumu yao  makuu. 

“Nawaombeni pia mhakikishe mnakuwa na majibu  ya staa pindi mnapowajibu wananchi na muepuke kuwajibu  vibaya kwani kwa kufanya hivyo mnakiuka  Sheria na kanuni za maadili ya umma.

Naibu waziri wa Tamisemi Dk .Festo Ndungange amewataka kutumia mfumo huo wa uwazi ili kuondoa malalamiko kwa wananchi na kuweza kutengeneza miradi yao ya maendeleo .

Amesema kuwa, endapo watatuma mfumo huo utasaidia sana katika kuboresha utendaji kazi kwenye mambo ya serikali za mitaa .

Mwenyekiti wa TOA  Taifa ,Albert  Msovela amesema kuwa TOA ipo kisheria ikiwa na lengo la kuchangia na kuongeza ushiriki wa wananchi wote katika masuala ya utawala ambapo imekuwa imekuwa ikileta pamoja wananchi katika kusimamia masuala ya ungatuzi wa madaraka katika serikali za mitaa.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “kuboresha nguvukazi katika mamlaka za serikali za mitaa,kurahisisha utoaji wa huduma bora.”