*Kauli ya Rais Magufuli yazima ‘kiburi’
chake nchini
*Sh bilioni 1.2 makontena kaa la moto,
akilipa linammaliza
*Wasema sasa ni ‘zilipendwa’
,
wakumbushia vituko vyake
*Askofu Gwajima asisitiza alikwishamfuta
katika uliwengu wa siasa

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, maji yamemfika shingoni na
kama si mwogeleaji hodari kisiasa wakati
wowote kuanzia sasa jahazi lake linaweza
kuzama, JAMHURI limebaini.
Makonda, mwanasiasa anayetajwa kuwa
“rafiki” wa karibu wa Rais John Magufuli

aliyemwamini, akampa madaraka makubwa
na kumkingia kifua dhidi ya mawimbi mengi
yaliyopita, kwa sasa inaonekana nyota yake
inaanza kuzimika mbele ya Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameonyesha hisia bila kificho
kuwa amekerwa na namna Makonda
alivyoshughulikia suala la makontena 20 ya
‘samani za walimu’

, hivyo akaamua

kumsema wazi hadharani kuwa alipe kodi.
Akiwa Chato, mkoani Geita, Rais Magufuli
hakumng’unya maneno, bali akasema
bayana kuwa viongozi wote nchini
wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia sheria na kuhakikisha
wanasimamia ipasavyo matumizi ya
rasilimali za umma kwa masilahi ya
wananchi.
“Sasa ni lazima sisi viongozi, no matter uko
kwenye position gani, tujenge mazingira ya
kuwatumikia Watanzania. Hizo ndizo
sadaka zetu. Mmesikia hili sakata la Dar es
Salaam. Eti Mkuu wa Mkoa ameleta
makontena, anaambiwa alipe kodi hataki,
kwa nini asilipe kodi?
“Kwa sababu katika sheria za nchi yetu kwa

mfano… ni mtu mmoja tu, katika nchi hii
aliyepewa dhamana kwa mujibu wa sheria.
Sheria ya Fedha, Sheria ya Madeni, Sheria
ya Dhamana na Misaada. Nafikiri kupitia
Sheria Namba 30 ya mwaka 1974 [kama
ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya
mwaka 2003] kifungu cha 3, 6, cha 13, cha
15, ndiye amepewa dhamana ya kupokea
misaada kwa ajili ya nchi, hakuna mtu
mwingine. Hayupo.
“Sasa ukichukua makontena kule,
umezungumza labda na watu wengine au
na wafanyabiashara, unasema una
makontena yako halafu ukasema ni ya
walimu, wala hata shule hazitajwi, maana
yake nini? Maana yake si unataka utumie
walimu, ulete hayo makontena, utapeleka
shule mbili – tatu ndizo zitapewa, mengine
unakwenda kuyapeleka kwenye shopping
mall. Lakini walimu walikwambia wanahitaji
makochi, sofa? Kwa hiyo wafanyakazi
wasitumike kwa masilahi ya watu fulani,

amesema Rais Magufuli.
Mwezi Agosti, 2018 umekuwa mwezi
ambao kisiasa Makonda hawezi kuusahau.

Agosti 1, mwaka huu Rais Magufuli wakati
anawaapisha wateule mbalimbali Ikulu
alitoa kauli iliyoonyesha kuwa siku za
Makonda zinahesabika.
Msimamo huu wa Rais Magufuli dhidi ya
Makonda ulianza kuonekana Agosti 1, 2018
wakati akizungumza na wateule
aliowaapisha alipoisifia Dodoma kwa
kukusanya kodi vizuri tofauti na Dar es
Salaam. Rais Magufuli alisema kati ya majiji
yote, Dodoma inaongoza kwa makusanyo
ya mapato ya Sh bilioni 24.2 ikiwa ni
asilimia 123 ya makisio yao ya Sh bilioni 19.
Alikwenda mbali zaidi akasema Jiji la Dar es
Salaam ambalo ni kongwe kuliko yote
lilikusanya Sh bilioni 15.3, Arusha Sh bilioni
10.3, Mwanza Sh bilioni 9.3, Tanga Sh
bilioni 9.1 na Mbeya Sh bilioni 4.2, suala
lisilokubalika.
Mmoja wa wanasiasa aliyepo karibu na
Ikulu ameliambia JAMHURI: “Kwa kweli
Makonda amewekewa mtego wa mwaka.
Ikitokea akailipa hiyo kodi ya Sh bilioni 1.2,
basi siku hiyo hiyo anapandishwa Kisutu.
Atakaguliwa mapato yake, vyombo vya dola

vitamhoji amezitoa wapi.
“Mwanzo alifikiri ni mchezo TRA
walipotangaza akasema hana uhusiano na
makontena hayo, mara akasema
atamwambia rais, wote tukawa na wasiwasi
kuwa huenda ni makontena ya rais pengine
ndiyo maana anataka kumwambia, kumbe
sivyo.
“Kwa kawaida kila rais anakuwa na mtu
anayempenda na anayemwamini, aliye
tayari kumlinda. Lakini hata kama ukilindwa,
ni vema ukafahamu kuwa katika siasa
hauwezi kuwa na ulinzi wa kudumu.
“Kutokana na ukweli huo, Makonda
alipaswa kujua kuwa rais anatumia nguvu
kubwa kumlinda, hivyo naye alipaswa
kuilinda heshima hii anayopewa. Ni bahati
mbaya kwamba alifikiri yeye ni mbia wa
rais, hivyo akadhani anaweza kufanya kila
atendalo.
“Nilipoona habari hii imeandikwa kwenye
Gazeti la Uhuru, ambalo ni Gazeti la CCM,
nikajua nyota ya Makonda imeanza
kuzimika. Naifahamu CCM nimekuwa
mwanachama kwa miaka 38 sasa. CCM ina

masilahi ya kudumu ya nchi, lakini si mtu.
“Makonda angeachwa anakuwa sawa na
mtoboa jahazi. Rais anapambana
kukusanya kodi kujenga reli ya standard
gauge, barabara, maji, dawa hospitalini,
halafu unaletewa taarifa kuwa mmoja wa
makamanda wako uliyetarajia akusaidie
kukusanya kodi anashirikiana na wakwepa
kodi kwa miradi ya kisanii, ni lazima hili
limemuumiza sana Rais Magufuli. Ilibidi
atoke hadharani na kusema na
nampongeza rais kwa alichofanya.
“Bado kidogo ule wimbo wa Diamond wa
‘Zilipendwa’ utaanza kuimbiwa mtaani sasa,
utasikia watu wanasema: ‘Gwajima na
Bashite, zilipendwa, zilipendwa… Makonda
na Magufuli, zilipendwa, zilipendwa…’ Kwa
kila hali, Makonda sasa hivi amefikia saa 12
kasoro robo jioni. Hakuna namna, atapata
tabu sana.”
Hata hivyo, Makonda bado ana nguvu,
kwani JAMHURI karibu viongozi wote
liliozungumza nao wanasita kutajwa majina
yao gazetini, ila wako tayari kunukuliwa
kama vyanzo vya kuaminika.

“Mhe. Rais ana urafiki wa karibu na
Makonda. Sote tunakumbuka alichomfanya
Nape Nnauye, aliyejaribu kumgusa
Makonda aliyejitangaza mara kadhaa kuwa
waziri yeyote hana mamlaka mbele ya
mkuu wa mkoa. Sasa unaposema unataka
kuweka jina langu, hunitakii mema.
“Ndugu wakigombana, shika jembe ukalime,
maana si muda watapatana, kisha
wataungana kukushughulikia. Bado nina
watoto wanataka kwenda shule, hivyo kama
unakubali ujumbe, ndiyo huo uufikishe, ila si
jina langu,

” amesema Mjumbe wa Mkutano

Mkuu wa Taifa wa CCM, aliyeomba
ahifadhiwe jina.
Mwingine akasema: “Makonda anafahamu
dhambi zake. Aliwambia watu Roma
Mkatoliki alipotekwa angepatikana ndani ya
siku mbili na akapatikana kweli. Kwa hiyo
anafahamu nani walikuwa wamemteka na
huenda anashiriki mchezo huo.
“Makonda huyu huyu amekingiwa kifua
wakati wa vyeti feki, lakini yeye akawa
anatukana watu wenye vyeti vyao. Ninyi
JAMHURI mlikwenda hadi nyumbani kwao

kwa mzee Kamese Mwanza, mkabaini kuwa
ni kweli anaitwa Daudi Albert Bashite kama
alivyosema mara kadhaa Askofu Josephat
Gwajima, bado rais akamlinda.
“Makonda huyu huyu anayetukana kila mtu
kwa kiburi cha kulindwa na rais, sasa
ameingiza askari wa JKT mtaani bila
utaratibu na wanachafua Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT) kwa sababu hata vibaka
wanaingia kwenye makazi ya watu wakidai
wametumwa na Makonda na wanapiga na
kuumiza watu, huku wengine wakiiba.
“Huyu bwana hana chembe ya utawala wa
sheria. Mhe. Rais haya aliyoona ni
machache. Akiendelea kumlea siku akija
kufahamu anayoyafanya Makonda nyuma
ya pazia, serikali yake itakuwa imechafuka
mno. Rais asikubali serikali yake
kuchukuliwa kuwa inafanya biashara Ikulu
kutokana na makosa ya Makonda.
“Makonda ana gharama kubwa kwa Rais
Magufuli… lakini Rais [Jakaya] Kikwete
alitwambia: ‘Akili ya kuambiwa, changanya
na ya kwako’. Rais amshukuru Mungu
amepata fursa ya kuanza kumfahamu

Makonda. Asipojiongeza, historia
itamhukumu.”
JAMHURI limemtafuta Askofu Josephat
Gwajima kupata maoni yake juu ya
uhusiano wa Rais Magufuli na Makonda
kuonekana kuyumba, aliyesema:
“Nilishamfuta Makonda hadharani katika
ulimwengu wa siasa… suala hili limo
mikononi mwa rais, na Mungu anaendelea
kutenda kwa kadiri ya maombi ya wenye
haki.” Hakutaka kuendelea zaidi.

Rafiki wa Makonda anena

Rafiki wa karibu wa Paul Makonda, ambaye
hakutaka kutajwa jina lake gazetini,
ameliambia JAMHURI kuwa Makonda,
amefedheheshwa na tuhuma zilizoelekezwa
kwake, huku sehemu ya tuhuma hizo zikiwa
hazina ukweli wowote.
“Unajua Makonda kwa kiasi kikubwa
amekuwa anapambana kuhakikisha
anatatua kero za wananchi wa Jiji la Dar es
Salaam… katika harakati hizo sidhani kama
wote wanafurahi. Amepambana na masuala

kadhaa bila kurudi nyuma na amefanikiwa.
“Makonda amepambana kuongeza mapato
kutoka Sh milioni 86 za maegesho ya
magari jijini Dar es Salaam hadi kufikia Sh
bilioni 1.5 kwa mwezi, mambo ya dawa za
kulevya, uvutaji wa shisha, amehangaika
kutengeneza magari mabovu ya polisi
pamoja na ofisini kwake, yeye amekuwa
mkuu wa mkoa anayeshughulika na
suluhisho kwa mkoa wake.
“Inashangaza kuona kuna watu wanakuwa
na ujasiri wa kumwambia Rais Magufuli
kwamba kwenye yale makontena kuna
makochi…” kimesema chanzo chetu.
JAMHURI limemtafuta Makonda, ambaye
amesema kwa ufupi: “Sina la kusema.”
Wakati huohuo, wiki iliyopita Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kupitia Kampuni ya
udalali ya Yono Auction Mart imeshindwa
kuyauza makontena 20 yaliyoagizwa na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda.
Katika mnada uliofanyika Jumamosi,
kuanzia saa 03:00 asubuhi, kwenye ghala la
Bandari Kavu Dar es Salaam (DICD),

makontena 10 yalifunguliwa wateja
waangalie bidhaa zilizomo, lakini mengine
10 hayakufunguliwa.
Akifungua mnada huo, Mkurugenzi Mtendaji
wa Yono Auction Mart, Scholastica Kevela,
aliwaita waandishi wa habari na kuwaonya
kutopiga picha bidhaa zilizomo kwenye
makontena hayo wakati wateja wakikagua,
jambo lililozidisha utata.
Alitaja masharti mengine kuwa ni wanunuzi
kuwa na vitambulisho, leseni za gari na pasi
ya kusafiria. Hata hivyo, alisema bado
wateja wengi hawajafikia bei zinazotakiwa.
Bei zinazotajwa ni kati ya Sh milioni 6 hadi
Sh milioni 16.
Akizungumzia mwenendo wa mnada huo,
katika ghala la Kurasini Inland Container
(KICD), Kevela amesema wamefanikiwa
kuuza vifaa 10 katika maghala hayo mawili,
lakini wameshindwa kuuza makontena 20
ya Makonda.
“Makontena yalikuwa 20 bei imefika hapo
ilipofika na tunaendelea na uuzaji. Kama
ilivyosema serikali, huu siyo mwisho,
nimeeleza tangu mwanzo kila Jumamosi

tunafanya mnada, kwa hiyo tutaendelea
mpaka makontena yote yapate wateja,

amesema Kevela.
Wakati huo huo, Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu katika waraka wake
kwa Rais John Magufuli, anasema Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam ni kielelezo cha
wazi cha viongozi wasiozingatia na
wanaopuuza utawala wa sheria.
Lissu anasema Rais Magufuli alinukuliwa
akisema kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam anadaiwa kodi kutokana na
yaliyomo kwenye makontena.
Mbunge huyo ambaye yumo nchini Ubelgiji
akipatiwa matibabu, anasema Rais Magufuli
ameibua maswali kadhaa. “Je, kilichomo
ndani ya makontena yale ni madawati ya
shule tu au kuna masofa ya kupelekwa
kwenye shopping malls?” amehoji Lissu.
“Je, kama ni zawadi kwa mkuu wa mkoa,
kiongozi wa serikali, kwa nini zawadi hizo
kwa serikali hazijapelekwa kwa Waziri wa
Fedha ambaye umetuelimisha, ndiye
mwenye mamlaka kisheria ya kupokea
zawadi zote za serikali kwa mujibu wa

Sheria ya Misaada, Mikopo na Dhamana za
Serikali ya mwaka 1974?” amehoji Lissu
katika waraka wake uliochapishwa wote
gazetini leo.
Lissu anasema Makonda hajawataja hao
marafiki au wafanyabiashara anaodai
wamempa zawadi ya makontena hayo, na
hilo ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya
TAKUKURU na Sheria ya Mapato ya
Udhalimu (Proceeds of Crime Act).
“Kwa makosa yote haya, haitoshelezi na
haitatosheleza kwa Mkuu wa Mkoa
Makonda kuambiwa alipe kodi anayodaiwa
tu halafu yaishe,

” amesema Lissu.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share