Mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tayari wamejitokeza watangaza nia 40 ambao wote wanawania kiti cha urais, waweze kumrithi Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu. Kila anayetangaza nia anayo maono ya nini anataka kuifanyia nchi hii kwa nia njema ya kututoa hapa tulipo tusonge mbele zaidi. Katika makala hii, Mwandishi Wetu amefanya mahojiano na mmoja wa wana-CCM walioonesha nia ya kugombea urais wa nchi hii. Huyu si mwingine bali ni Charles Makongoro Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, anayetaka kuirejesha CCM mikononi mwa wakulima na wafanyakazi. Atafanyaje? Soma mahojiano hapa chini.

JAMHURI: Mheshimiwa, nini hasa kilichokusukuma zamu hii ukasema ugombee urais?
Makongoro: Ehee, ninao uwezo, ninayo nia, ninayo sababu. Chama Cha Mapinduzi sasa hivi kimepoteza mwelekeo wake ule wa asili. Chama Cha Mapinduzi kihistoria ndiye mwakilishi halali, wa watu walio wengi, wanyonge. Ni chama cha wakulima na wafanyakazi, kisichobagua walio wachache. Walio wachache ni pamoja na matajiri wanaofuata sheria za nchi yetu, wasiokuwa wasumbufu.
Ni pamoja na, kwa mfano, walemavu, ni pamoja na watu wenye rangi ambazo ni tofauti katika miili yao. Wote wako included (pamoja) humo lakini ni pamoja na waliolengwa, ni hawa wakulima na wafanyakazi. Chama Cha Mapinduzi ni urithi wetu katika urithi halali tuliopewa na wazee wetu, waasisi wa nchi yetu. Urithi wa kwanza waliotupatia ni nchi iliyo huru. Na walitwambia kwamba tulitawaliwa kwa sababu hatukuwa wamoja, tulikuwa hatuna elimu, tulikuwa tuna njaa, tulikuwa hatuna lishe, tulikuwa hatuna tiba, na hatuna nyumba nzuri za kuishi.
Na wakatuasa kwamba tunakuachieni nchi huru, na msikubali kutawaliwa tena, na ili msitawaliwe tena ndiyo wakatuachia urithi wa pili, haki yetu. Wakatuachia Chama Cha Mapinduzi. Chama Cha Mapinduzi ni muunganiko wa vyama viwili vya ukombozi — Afro-Shirazi Party ambayo ndiyo mwakilishi wa kweli wa walio wengi Zanzibar na TANU, mwakilishi wa kweli wa walio wengi Tanzania Bara. Waasisi hao walisema palipo na umoja pana nguvu, hivyo vyama hivi vya kweli na vya asili ambavyo walituachia urithi na nchi, vikaungana kuwa Chama Cha Mapinduzi na wakaeleza tangu mwanzo kuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi.
Na walituachia chama ambacho kilikuwa ndicho kinachoongoza serikali zetu mbili. Sasa hivi kuna dalili za dhahiri kwamba chama hiki hakiongozi hizi serikali mbili. Pili kuna udhahiri kuwa chama hiki sasa kimevamiwa na wezi, wala rushwa na mafisadi. Kwa hiyo, nimeingia ulingoni kuwapa nafasi vikao vya uamuzi, kama wataamua kufanya hivyo, uhakika huo sina, lakini kama watafanya hivyo, ili nikirejeshe chama hiki mikononi mwa wale walioundiwa chama hicho. Wananchi wanyonge walio wengi. Nina maoni yangu kwamba mwaka 2015 tukifanya kosa tukakiachia Chama Cha Mapinduzi kikaenda kwa mwizi au fisadi au mla rushwa, ndiyo bye-bye (kwaheri) hatutakipata tena.

JAMHURI: Ikitokea ukafanikiwa, utawashughulikiaje hawa ambao unadhani wamekipeleka chama kusiko?
Makongoro: Kwanza kabisa ni kuvunja makundi. Chama kiwe na msimamo mmoja, kwa sababu Chama Cha Mapinduzi ndiye kiongozi wa kweli wa kihistoria wa nchi yetu. Siyo wa kubambikiwa, wa urithi. Ukikigawa Chama Cha Mapinduzi, na Watanzania utawagawa. Ukikifundisha Chama Cha Mapinduzi  wizi, na Watanzania watakuwa wezi na civil service (utumishi wa umma) nao watakuwa wezi. Ukikifundisha Chama Cha Mapinduzi ufisadi, Tanzania nayo itakuwa nchi ya ufisadi, na watumishi wetu wa umma pia nao watakuwa mafisadi. Ukikifundisha Chama Cha Mapinduzi kutofuata utaratibu kiliojiwekea, na Serikali yetu nayo itakuwa haifuati utaratibu. Sasa nitakishughulikiaje, mimi na kushughulika kwanza ni kukishughulikia hiki chama. Chama ambacho kinajidai kina uzalendo, lakini hakioneshi uzalendo, wanajidai wao ndiyo wazalendo, haina maana upinzani hawapo wazalendo, akiwa upinzani anaonekana ni mwongo, akiwa kwenye Chama Cha Mapinduzi anaonekana ni mzalendo wakati mwizi, wakati ni kibaka.
Kimsingi, huwezi kutimiza ahadi zozote ulizopewa na Chama Cha Mapinduzi kama ni kiongozi mkuu wa Serikali ikiwa manufacturer (mzalishaji) wa wezi, manufacturer wa mafisadi, manufacturer wa watu wasiopenda kufuata utaratibu bado ni Chama Cha Mapinduzi, hutafanikiwa kwanza. Step one (hatua ya kwanza) ondoa makundi, halafu ondoa wale wanaoleta matatizo, wale ambao wamefanya chama hiki leo heshima yake imekuwa mbaya.

JAMHURI: Unawaondoaje sasa hawa?
Makongoro: Kwa kutumia Katiba ya Chama. Huwafukuzi, kama yupo pale unasubiri wakati wa vikao, unasema jamani huyu ndiye anayetusumbua kila siku, nidhamu yake na pale, unasema sasa huyu tusimfukuze chama. Kuwa mwanachama wa chama ni hiyari yake. Tusimfukuze chama, lakini tusimpe nafasi ya uongozi katika chama chetu. Eheee, asipewe nafasi ya uongozi. Katika chama chetu na hasa hasa katika Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Ehee maana yake, kuwa na chama kwa hiyari yake ni imani yake. Unaweza ukawa wewe unaamini Uislamu lakini hufuati misingi ya Uislamu. Sasa sisi wanadamu hatuna haki ya kukufukuza Uislamu. Unaweza kuwa sheikh, imamu wa Msikiti wetu, katika nguzo ya Uislam moja inasema lazima ni swala tano. Kila tukija msikitini hatukuoni ili uongoze ibada. Ukitafutwa unapatikana mara moja. Kwa sababu unapatikana kwenye kilabu cha pombe. Si kwamba umefiwa, unapatikana, lakini msikitini huonekani.
Sasa tunachotakiwa kufanya, waumini ambao ni serious wa ile dini na kwa mawazo ya tulio wengi hatukufukuzi dini, tunakwambia turejeshee msikiti wetu na uishie. Halafu mnatafuta mtu mwingine, mnamwambia kaa pale. Au wewe ni Mkristo, mna paroko wenu. Yule paroko wa Parokia yenu mkisikia pale pameibwa vitu, jina lake linatajwa. Mkisikia pahali kuna mtu amekamatwa ugoni, jina lake linatajwa. Mkimuuliza, anakataa. Halafu siku moja mnakuta amekimbia ugoni, karibia kama hivi hivi alivyozaliwa, uchi wa mnyama. Halafu hata na ile shuka mnakosomesheni misa, nalo limeachwa ushahidi huko alikofumamiwa, kupunguza ugomvi.
Sasa kama ninyi ni waumini serious (makini) ni kumwambia askofu au kardinali kwamba tuondolee huyu paroko hamna mwingine? Anatuharibia Parokia yetu, maana tunaonekana Parokia yote sisi wazinzi hapa. This is the only way, so what to do (hii ndiyo njia pekee, sasa nini kifanyike) nikumwambia kwamba anawaharibia sifa yenu. Na utendaji wenu ni mbaya. Mnawaambia kwamba CCM tuliwapeni nafasi hizi, mkazitumia vibaya, mkatuvunjia heshima yetu, mmevunja imani yetu kwa wananchi, sasa basi inatosha. Kwa nchi hii haina watu wengine, wapo wengine wanaoweza kufanya kazi hizi vizuri na kwa uadilifu.

JAMHURI: Kwenye eneo la uchumi mheshimiwa, ukifanikiwa kushika nchi, Mwalimu Baba wa Taifa alijenga mashirika 450 na viwanda vikubwa. Viwanda vyote alivyovijenga karibu vyote  vimekufa kama Mwatex, Kiltex na vingine. Hata viwanda vya ngozi vimetushinda. Wewe katika eneo hili utafanya nini ili tuzalishe na kuuza ndani na nje ya nchi shilingi yetu isicheze?
Makongoro: Nitafanya vile nitakavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ambayo sasa hivi bado sijaiona. Ehee, mpaka sasa hivi siwezi kukujibu. Nikiishaiona, nitaweza kukujibu.

JAMHURI: Katika eneo hili nimesoma pahala, ukimtaja mgombea mmoja aliyeonesha nia, Wasira, kwamba yeye amekuwa anaandaa Ilani lakini amefika ni kama vile amekuja na kabrasha anaizungumzia kupitia milango ya nyuma, ambalo si fair (haki) kwa wagombea wengine.
Makongoro: Siyo utaratibu kwanza, mwenye mamlaka ya kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, kikao pekee chenye mamlaka ya kuitoa Ilani, siyo Kamati ambayo yeye ni Mwenyekiti, hiyo ni Kamati ya kuandaa rasimu. Halafu rasimu ikiishatayarishwa kikao cha kwanza kinachoipitisha hiyo rasimu ni Halmashauri Kuu ya Mkutano Mkuu. Kwa maana ikiishapitishwa itapelekwa kwenye Mkutano Mkuu ambao ndiyo wenye mamlaka ya kupitisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Mkutano Mkuu ndiyo mwenye mamlaka ukiridhika na Ilani na kuipitisha. Chama Cha Mapinduzi, kwa mujibu wa miiko tuliyoachiwa na waasisi na kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, siyo kinaongozwa na mtu mmoja mmoja. Ni chama ambacho tunakiongoza kwa pamoja kwenye vikao. Sasa wewe, ukianza kusema mtangaza nia utafanya nini, unayoyasema yakiwa tofauti na ile mwenye mamlaka atakayotoa Ilani, utajibu nini? Au kama wewe unaanza kusema kabla eti kwa sababu wewe ndiye upo kwenye Kamati ya Ilani, what do you want to prove (unataka kusema nini) wakati unadai wewe ni mwadilifu?
Una uadilifu gani wakati unajinyakulia mamlaka ya Mkutano Mkuu, unayanyakuwa. Wewe ndiye umekuwa Mkutano Mkuu? Halafu, funny enough (cha kushangaza) utaratibu wanaujua, na wote hawa niliowatolea mfano; Edward Lowassa, Mwigulu Nchemba, na Wasira utaratibu wanaujua wanatunyang’anya sisi wajumbe wa Mkutano Mkuu mamlaka yetu na mpaka sasa hivi hawajatutaka radhi. Ebu angalia walivyo na dharau, ni watu wenye dharau. Dharau imeingia kwenye Chama Cha Mapinduzi na inaoneshwa waziwazi na hawajali.
Na ndiyo matokeo yake leo, kutokana na kuzungumza za kwao binafsi unapompa mtu wa namna hiyo uongozi wa juu wa chama ana hiyari ya kufanya ya kwake binafsi na kuachana na hayo ya kwenu kwa sababu tangu mwanzo alisema atafanya ya kwake and then (kisha) akaja tatu bora, huyo aliyesema hivyo bila kuwataka radhi. Mkampa na ya kwenu. Akiishaingia kule madarakani, Kinana siyo kama Kinana lakini kama Katibu Mkuu wa chama akimfuata kumwambia jamani eheee, huku kuna kilio hiki si anamwambia, ‘ahaa usinibabaishe bwana. Wewe ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi nilipokuja sikusema nitafanya hayo. Sasa wewe mtendaji mkuu wa chama usinisumbuesumbue ndiyo maana yake kosa umelifanya tangu mwanzo.

JAMHURI: Kuna sehemu nimesoma kwamba unawataja hawa watatu kwa sababu unawaogopa. Kwamba unawaona wao ndiyo tishio kwenye mpango wako huu.
Makongoro: Wale siwaogopi isipokuwa timetoa mfano kama kigezo cha kufundishia (teaching aid). Ina maana unapotoa teaching aid unamwambia mwanafunzi huyu unamuona huyu, huyu ana kifaduro, huyu ana tumbo la kuhara, sasa na yule mwanafunzi anaelewa. Siwaogopi, mimi niwaogope watu ambao si waadilifu? Hawa ndiyo nataka nipate nafasi niwanyooshe wawe waadilifu. Waache tabia mbaya, wale nimewatumia kama teaching aid, wamo wengi humu ndani na ninawafahamu wote kwa sura na majina, ehee ila nilitumia wachache ili nisiwadanganye wanafunzi wangu.

JAMHURI: Kwenye eneo la uongozi na uzoefu, wapo wanaosema huna uzoefu wa kutosha maana ulipata kuwa Mbunge wa Arusha kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, baadaye ukarejea CCM. Rais Benjamin Mkapa akakuteua kuwa mbunge na kuna taarifa kuwa alitaka kukupa unaibu waziri ukakata, akataka kukupa ubalozi wa Zimbabwe ukakataa pia. Unalizungumziaje?
Makongoro: Katika uzoefu wamesahau kuwa nimewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara kwa miaka mitano, hilo ninalo, uzoefu ninao bwana. Ehee, uzoefu gani tena, wanataka uzoefu wa wizi, kuiba sijazoea, ufisadi zijauzoea na ninauchukia. Na kutofuata utaratibu, hiyo sina uzoefu huo sina, nina uzoefu wa kufuata utaratibu. La msingi hapa ni kwamba mimi ni mwadilifu bwana, sina uzoefu wa wizi.
Sina uzoefu wa kusoma vibaya Ilani ya Uchaguzi. Ilani ya Uchaguzi, kwa mfano, inasema kwamba tukienda huko vijana wa vyuo vikuu tuwalipe hela waweze kusoma halafu haijaandikwa kwamba tuwapige mabomu ya machozi, because you are doing otherwise (unafanya kinyume).

JAMHURI: Lakini pia wanasema mwaka 2004 Rais Mkapa alipokuwa amekuteua, alikupa fursa ya kuwa Naibu Waziri au Balozi wa Zimbabwe ukakataa, sasa haiwezekani Watanzania wakakupa urais ukakataa pia?
Makongoro: Wakinipa urais Watanzania, kwanza Watanzania kunipa urais itakuwa napitia CCM inabidi kwanza wanipe CCM. Watanzania hawawezi kunipa urais, kama CCM hawajanipa. Kwa sababu CCM wakiishanipa, mimi nitakuwa mgombea wa CCM, sasa kama nitakuwa tayari niko CCM, Watanzania wakanipa urais, itakuwa imekataa CCM. Wewe CCM wanakataaga urais?

JAMHURI: Kuna taarifa kuwa uliporejea CCM kutoka NCCR-Mageuzi, kurejea kwako kulichangia ushindi wa Rais Mkapa.
Makongoro: Kilichotokea tulikuwa wamoja ndani ya CCM. Hii mana yake ni nini, ni kwamba kama mkiwa wamoja mtashinda udiwani, mtashinda ubunge na mtashinda urais. Mkiwa hamna umoja, na hili nalijua mtashindwa kila kitu. Kwa hiyo, mimi CCM ndiyo inayonibeba, kwa hiyo mimi ninachofanya ni kutangaza sera ya hicho chama. Kwa hiyo, Mkapa aliposhinda au mimi nitakaposhinda, ni chama ndicho kilichonibeba siyo mimi niliyekibeba chama. Au siyo mmoja mmoja kati yetu, mmoja mmoja ndiye anayekibeba chama.
Ukiishaanza kufanya hivyo unaanza kuona walionipa urais si Watanzania, nitaanza kuwaogopa hao badala ya kuiogopa CCM. Hiyo ni sehemu ya maradhi ya CCM ya sasa.

JAMHURI: Suala la mgombea mwenza kwamba una mpango wa kumchukua kijana kutoka Zanzibar awe makamu wako, na baada ya miaka 10 umkabidhi madaraka rais atoke Zanzibar. Hili unalizungumziaje?
Makongoro: Mimi mpango wa mgombea mwenza sina. Isipokuwa ninazo taarifa ambazo naamini ni za uhakika. Kwamba aliyeshawishi mgombea mwenza rais akitoka upande mmoja wa Muungano, mgombea mwenza atoke upande mwingine na akakubaliwa kwa hoja, alikuwa ni Baba wa Taifa na nia yake ilikuwa ni kusaidia Zanzibar. Haikuwa kusaidia mgombea mwenza, nor kusaidia Zanzibar kama nchi. Kwamba lingeachwa wazi, mgombea angeweza kutoka upande mmoja, upande mwingine ukakosa mgombea mwenza kwa sababu ya mapenzi yake. Kwa hiyo likaingizwa hilo kwenye Katiba ya nchi. Sasa mimi ninavyofahamu, ingawa hakusema hivyo, ninavyofahamu na ninavyoamini nia yake ilikuwa ni kwamba huu upande mwingine, ndiyo upendekeze, kwamba sisi tunadhani, mgombea mwenza chama mmempa huyo, tunadhani chama sasa huku awe fulani. Na wakifanya hivyo wala wasiniambie mimi, waiambie Kamati Kuu, Kamati Kuu itaniambia, basi mimi nitasema sawa bwana. Nitapiga saluti na, naondoka naye.

JAMHURI: Kuna hili linasemwa kuwa wewe umeingia kwenye kinyang’anyiro si kwa sababu nyingine bali kumsafishia njia Mheshimiwa [Bernard] Membe, na kwamba hapo baadaye wewe utamwachia na umuunge mkono. Wewe hilo unalizungumziaje?
Makongoro: Mimi hilo sijaliona, lakini nikuamini wewe na nikujibu kama ulivyosema. Mimi sijaingia humu kumsafishia njia mtu. Na hata kama siku nikitaka kumsafishia njia mtu, sitamsafishia Membe… kwa nini nimsafishie? Kwa sababu sasa hivi kuna makundi, katika Chama Cha Mapinduzi, na mimi makundi siyapendi. Kwa sababu makundi ndiyo yanayodhoofisha Chama Cha Mapinduzi, na ndiyo maana nimeingia humu kivyangu, na nikosa nikose kivyangu. Lakini nikipata nisipate kwa sababu kuna mtu fulani amenisaidia.
Mimi nataka nifuate taratibu zilizowekwa ili kwamba nikipitishwa, nijue kwamba kura nilizozipata siyo kura za makundi, ni kura za Chama Cha Mapinduzi na ni kura za kazi. Mimi nataka kuomba kura za kazi. Siyo kura za Membe sijui, Mwandosya, sijui Lowassa, kwani wao nani? Wao wana kura moja kama mimi. Mimi nipeni kura za kazi, za kutosha kutoka Mkutano Mkuu, nataka bosi wangu kuanzia siku ya kwanza awe Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, full stop. Hawa watu mmoja mmoja ndiyo wametufikisha tulipo sasa hivi sitaki kabisa.

JAMHURI: Lakini pia kuna jingine, hili hutakuwa umelisikia kwa mara ya kwanza kutoka kwangu, kwamba kinywaji unakipiga kidogo. Kwamba unaweza kwenda Ikulu ukawa unashinda umeutwika, halafu nchi ikajiendesha. Wewe unalizungumziaje?
Makongoro: Na mimi pia nimelisikia hili suala, lakini pia Ikulu napafahamu, hakuna baa pale. Pale kuna ofisi tu na kazi, baa ziko huku kwingine. Asante sana kwa kuuliza.

JAMHURI: Na nikuulize na jingine wanasema mabinti unawapenda kidogo. Hata siku unatangaza nia uliwatajataja.
Makongoro: Niliwataja mimi mabinti nawapenda sana na bahati nzuri wao wenyewe wananipenda sana na tunapendana. Siyo mabinti ni wanawake. Tunapendana sana.

JAMHURI: Kwamba wewe ni Mkatoliki, hatutajikuta unafunga ndoa nyingine ukiwa Ikulu?
Makongoro: Ndoa nyingine hapana, kumpenda mtu mpaka umuoe bwana? (kicheko)

JAMHURI: Sasa hautaishia pale ambapo Mwalimu alikuwa anasema kwamba ‘waziri anapitapita na nanihii huko mitaani’, sasa rais akipitapita si itakuwa shida?
Makongoro: Rais akipitapita itakuwa shida, lakini sasa hatapitapita. Rais hatapitapita, rais kazi yake ni kuongoza nchi, siyo kupitapita. Waziri anaweza akapitapita akasahau wizara yake, akapitapita, lakini kazi ya rais ni kuongoza nchi, siyo kupitapita.

JAMHURI: Wapo watu wanaodhani Takukuru imeshindwa kazi. Ingawa wewe hutaki kuzungumza mambo yaliyopo kwenye Ilani, lakini unalizungumziaje hili suala, ukipata mamlaka Takukuru itaendelea hivi ilivyo au iwe na meno ya kuprosecute (kuendesha mashitaka) badala ya kupeleka kwa DPP halafu kesi zikawa zinafika mezani?
Makongoro: Wewe inaonekana hujanielewa vizuri, lakini swali lako litasaidia kunielewa vizuri. Takukuru haiwezi kufanya kazi, ikiwa yule manufacturer (mtengenezaji) wa matatizo bado yuko kama alivyo. Polisi hawawezi kukamata watu, wezi ikiwa manufacturer wa wezi ni chama tawala. Unanielewa vizuri, utasingiziaje Takukuru makosa ya Chama Cha Mapinduzi au unalisingiziaje Jeshi la Polisi makosa ya Chama Cha Mapinduzi? Na hata wewe rais usipolijua hilo, huwezi kutekeleza sera ya Chama Cha Mapinduzi ikiwa chama chenyewe kimekaa vibaka madarakani.
Ikiwa chama chenyewe kimekaa mafisadi madarakani. Eheee, ikiwa chama chenyewe kimekaa wala rushwa madarakani, huwezi kufanya kitu. Utakaa pale Ikulu miaka mitano huwezi kufanya kazi. Odoa kwanza wale vibaka wakae pembeni, halafu utaona Takukuru wanafanya kazi, utaona TRA wanakusanya kodi, ehee manake unamsingizia mkubwa wa TRA kuwa mbona kodi haikusanywi. Unamsingizia wapi, kwenye vyombo vya habari. Lakini kwenye Chama Cha Mapinduzi wasiotaka kulipa kodi wote ndiyo rafiki zako, na wakienda kule wakisema tu kwamba wewe unanidai kodi unanijua mimi ndiye rafiki yake fulani, unajua unaweza kuhamishwa hapa? Yule anakuwa mkali, lakini anapokuja kuhamishwa, atakuja mwingine. Anafanyaje?

JAMHURI: Sasa kuna dhana hii ya kuondoa wafanyabiashara kwenye siasa na mwanzo wakati tunaanza mazungumzo ulisema tuwe nao na urafiki wenye tija. CCM ina wafanyabiashara wengi na wameshika nyadhifa za uamuzi. Je, wewe ukiingia utawaondoa wafanyabiashara au utaendelea nao kidogokidogo?
Makongoro: Sikiliza nikwambie. Chama Cha Mapinduzi tunafanya uamuzi wa pamoja. Siku moja nikiwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, meza kuu ndiyo walioleta hoja hiyo, kwamba tuwaondoe wafanyabiashara, ahaa, mimi sikuona umuhimu wake, maana unambagua mtu kwa sababu ni mfanyabiashara? Sisi tunambagua mtu kwa vitendo vyake. Kwani kuwa mfanyabiashara ndo uwe mwizi? Unamfukuza mfanyabiashara ambaye siyo mwizi halafu unabaki na mwizi? Hiyo siyo diagnosis (uchambuzi) nzuri. Ondoa vibaka, ni maamuzi yanahitajika.

JAMHURI: Mheshimiwa, mara kwa mara unazungumzia vibaka. Wako kama wangapi CCM?
Makongoro: Hawafiki hata 20 lakini wanasumbua kweli. Hawa ndiyo wameiparamia CCM kama punda-kiongwe ambaye hana hata haki ya kula nyasi wala kunywa maji. Sasa mimi najua, ilipitishwa mimi nilikuwapo, katika uongozi wa pamoja mimi nakumbuka. Kwa mfano, katika kikao kimoja mimi nilishauri kwamba yule mtu mnayemtaka ninyi kugombea Musoma Mjini pale, msimpe. Mkimpa yule tutapoteza jimbo pamoja na council, wakanibishia na mimi nilikuwa humo, basi tukaenda. Sasa hilo pia liliwahi kuletwa, ehee, kwamba hawa wafanyabiashara tuwafukuze na mimi nilikuwa mle, nakumbuka kuhoji kwamba hiyo mantiki ya kuwafukuza wafanyabiashara kwenye uongozi wa CCM ina nini? Ahaa lakini sasa ilionekana ni jambo la kisiasa, linaleta shamrashamra, sasa haya.
Mpaka leo ni kama lile la gamba. Walizungumza gamba mimi nikawapa ushauri mzuri nalo pia halikutekelezwa. Kwa hiyo kuna mambo ndani ya CCM ambayo yamebaki yanazungumzwa mpaka leo hayajatekelezwa. Kwa mfano, la gamba walileta wenyewe meza kuu, mpaka leo gamba halijatoka, sasa mimi sijui gamba ni nini, ila ninachojua ni kwamba kura zangu hazikutosha mpaka. Kwa hiyo, kuna mambo ndani ya CCM yanazungumzwa. Kuna watu wanasumbua kuliko CCM na wanafanya CCM ionekane ndiyo wao. Sababu mojawapo ya mimi kuvuta fomu, ni utaratibu wetu kwamba huyo ambaye atakuwa rais katika muda mchache na kwa mapema iwezekanavyo huyo ndiye atakayekuwa mwenyekiti. Ili hawa watu ambao mdomoni wanasema chama kwanza mtu baadaye, na kwa matendo yao 100 kwa 100 ni mimi kwanza, ili walete maneno baadaye, tafadhalini kuweni na adabu.
Chama hiki siyo mnakiparamia wakati mnataka kwenda kutupora nchi yetu, kutupora chama, mtafute vyama vingine ambavyo yaani traditionally (kwa asili), siyo kwa ajili ya wanyonge. Katafuteni vyama vingine huko.

JAMHURI: Ingawa umesema hutaki kuzungumzia Ilani, lakini kuna kundi la vijana ambao ni wengi. Je, ukifanikiwa kushinda, utafanya nini juu ya vijana hawa?
Makongoro:Makongoro: Nitakayofanya yapo kwenye Ilani, wala usiwe na wasiwasi yapo. Siku zote tatizo la CCM hawayafanyi, ndiyo yapo. Hawayafanyi. Shida ya CCM, wanaiandika Ilani nzuri, halafu wanajifanya ndiyo namna ya kuwadanganya Watanzania wawachague, halafu hawafanyi. Hii ndiyo shida yangu. Lakini hata hivyo, sijui kama watanipa, mimi waninipa, mambo ya vijana, mambo ya uvuvi, mambo ya sera ya nje, yote yamo humo ndani. Kinachotakiwa ni kuyafanya. Acha kazi zako binafsi maliza zile ulizokabidhiwa kufanya. Ukianza na zako binafsi ndiyo mtaanza kwenda mambo ya Richmond, mara Escrow, hayakuandikwa haya [kwenye Ilani] mnayafanya ya nini?

JAMHURI: Na eneo la michezo pia nalo utaniambia kwenye Ilani?
Makongoro: Hata michezo ipo kwenye Ilani, hata wasanii wapo kwenye Ilani, mimi nina hakika wapo. Kinachotakiwa ni kutekeleza kwa pamoja. Manake mimi siyo Mkutano Mkuu, wewe hapo Balile ukianza kuniuliza wewe Makongoro nani, wewe ndiye Mkutano Mkuu? Nitakwambia ahaa samahani niwie radhi.

JAMHURI: Una neno lipi la kuhitimisha mahojiano yetu kwa Watanzania mheshimiwa?
Makongoro: Kwa Watanzania, mimi nasema Watanzania watuombee Watanzania wenzao, wa vikao vya uamuzi tuliopo ndani ya Chama Cha Mapinduzi, ili mwaka huu tusikosee tukampa mtu asiyestahili.

 
3810 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!