Na Michael Mbughi, JamhuriMedia, Mbeya

Mgogoro wa maeneo yanayodaiwa kuwa vyanzo vya mapato ya Serikali ya Kijiji cha Ipinda, wilayani Kyela mkoani Mbeya, umeibua maswali kuhusu umiliki wa ardhi na matumizi ya mali zinazotajwa kuwa chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baadhi ya viongozi na wakazi wa kijiji hicho wanadai kuwa maeneo yaliyokuwa yakitumika kwa shughuli za biashara na ukusanyaji wa mapato sasa yanatambulika kuwa mali za CCM, hali wanayosema imeathiri uwezo wa serikali ya kijiji kupata mapato na eneo la kujenga ofisi.

Malalamiko hayo yameibua mjadala kuhusu historia ya umiliki wa maeneo husika, huku viongozi wa kijiji wakitaka kupatikana kwa ufumbuzi utakaowezesha wananchi kupata huduma za serikali bila kuathiriwa na mgogoro huo.

Viongozi wa kijiji wanena

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ipinda, Erick Komba, ameliambia JAMHURI kuwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakitumika kwa shughuli za kiuchumi yalikuwa yakichangia mapato ya kijiji.

Amesema maeneo hayo yalihusisha vilabu vya pombe za kienyeji na biashara nyingine ambazo serikali ya kijiji ilikuwa ikizitegemea katika kukusanya mapato kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

“Changamoto kubwa inayotukabili kwa sasa ni kupata eneo la kujenga ofisi ya serikali ya kijiji. Sehemu iliyopendekezwa na CCM ina mgogoro,” amesema.

Komba ameshauri chama hicho na viongozi wa serikali ya kijiji kushirikiana kutafuta ufumbuzi utakaowezesha kupatikana kwa eneo lisilo na mgogoro.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kafundo, Gabriel Mwamundeka, amesema kuendelea kutegemea CCM kutoa eneo kutachelewesha ujenzi wa ofisi hiyo.

Kikao cha viongozi kilichofanyika mwishoni mwa wiki kilijadili umuhimu wa chama hicho kushirikiana na serikali ya kijiji kutafuta suluhisho.

Mwamundeka ameonya kuwa kuendelea kwa mvutano huo kunaathiri uhusiano kati ya wananchi na viongozi wao.

Amesema hata eneo ambalo chama kimependekeza kutoa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi linadaiwa kuwa na mgogoro unaohusisha familia moja.

“Viongozi wanafikiria kuwashirikisha wananchi katika kuchagua eneo jingine linalofaa, huku mazungumzo kati ya viongozi wa CCM na serikali ya kijiji yakitarajiwa kufanyika,” amesema.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA JAMHURI LA OKTOBA 27- NOVEMBA 2, 2026