Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Shinyanga

Mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Nyasorod Paul, anadaiwa kumuua mtoto wake Nazaeri Kidia, mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba na kisha kumla nyama.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesema mwanamke huyo mkulima mkazi wa Shinyanga, aliondoka nyumbani Januari 4, 2024 Akiwa na mtoto wake na kuelekea kusikojulikana, ambapo alirudi Januari 8, saa 2 asubuhi akiwa peke yake.

Wanafamilia akiwemo mama yake mzazi anayeishi naue nyumbani walipomuhoji kwanini amerudi bila mtoto alijibu kuwa amemla nyama.

Baada ya kupata Taarifa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga lilianza uchunguzi wa haraka ambapo mtuhumiwa aliwaambia kuwa amemuua mwanae katika mbuga za mashamba, na ikawalazimu timu ya askari kuelekea huko ambapo walifanikiwa kukuta fuvu la binadamu ambalo walilichukua kwa ajili ya kufanya kipimo cha ‘DNA’ ili kubaini kama ndiye mtoto wa mwanamke huyo.

Ofisi ya upelelezi Wilaya ya Shinyanga imepeleka jalada kwa mwanasheria wa Serikali ambapo katika upelelezi walimpeleka mtuhumiwa hospital kupimwa afya ya akili.

Kamanda Magomi amesema kwa sasa mtuhumiwa yupo nje kwa dhamana wakisubiria majibu ya vinasaba kutoka kwa mkaguzi mkuu wa Serikali.