Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani imetenga sh. milioni 420 kutoka mapato yake ya ndani kwa ajili ya kufungua na kutengeneza barabara za mitaa katika kata 14 , ikiwa ni hatua ya kupunguza kero za miundombinu ya barabara zinazokwamisha huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amesema fedha hizo zimeshaanza kusambazwa, ambapo kila kata imepokea sh. milioni 30 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya uboreshaji wa barabara katika maeneo yao.

“Kupitia mapato yetu ya ndani, tumeamua kuwekeza moja kwa moja kwenye barabara za mitaa kwa kuwa zinagusa maisha ya kila siku ya wananchi ,tutasimamia kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa ufanisi,” alieleza Dkt. Shemwelekwa.
Katika Kata ya Sofu, wananchi wamepokea hatua hiyo kwa furaha, wakieleza kuwa ni faraja kuona kodi zao zikifanya kazi kwa manufaa ya jamii.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Twendepamoja, Idd Alfan, alisema wananchi wamehamasika zaidi kulipa kodi kwa hiari kutokana na kuona matokeo ya moja kwa moja.
“Mradi huu umewapa wananchi motisha ya kulipa kodi, Wanaona matokeo na sasa wanathamini ushiriki wao katika maendeleo,” alisema Alfan.

Mkazi wa kata hiyo, Deborah Mkoma, alieleza barabara hizo ni muhimu kwa huduma za afya, usafiri wa bodaboda na usalama wa wakazi.
“Awali magari hayakuweza kufika, hata bodaboda walikuwa wanatoza bei kubwa. Sasa hali imebadilika tunafika hospitali na sokoni bila shida,” alisema Mkoma.
