Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni miongoni mwa injini za maendeleo katika taifa letu. Dhima kuu ni kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelevu, lakini wenye tija kuanzia ngazi ya chini kabisa ya jamii hadi taifa zima.

Kwa kulitambua na kulizingatia hilo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikitekeleza miradi mingi ya uhifadhi na jamii ndani na nje ya hifadhi. Miradi hiyo imegawanyika katika maeneo makuu manne; Usalama wa chakula kwa wenyeji waishio ndani ya hifadhi; Uboreshaji na tiba ya mifugo kwa wenyeji; Utekelezaji wa miradi ya huduma za jamii; na Utekelezaji wa miradi kwa ajili ya uhifadhi.

Katika mwaka wa fedha 2017/2018 pekee, Mamlaka imetekeleza miradi mingi; yote ikilenga kuboresha maisha ya Watanzania wanaoishi ndani na nje ya hifadhi.

Kwa kutambua kuwa wenyeji hawana ruhusa ya kuendesha shughuli za uzalishaji kupitia kilimo ndani ya hifadhi, usalama wa chakula kwa wenyeji waishio ndani ya hifadhi ni jambo la msingi sana. Mwaka 2017/2018 Sh bilioni 2.3 zilitumika kununua mahindi kutoka Ghala la Taifa la Hifadhi ya Chakula (NFRA) na kusambazwa katika vijiji vya NCA.

Sh milioni 100 zilitumika kutekeleza programu ya lishe katika shule za msingi 24 ndani ya hifadhi ili kuwawezesha watoto kupata elimu wakiwa na shibe njema, hivyo kusaidia kuongeza ufaulu wao katika masomo. Sambamba na hilo, Sh milioni 27 zilitumika kutekeleza miradi ya lishe kwa watoto wenye utapiamlo katika Hospitali ya Endulen.

Kazi kuu ya asili ya kiuchumi ya wananchi ndani ya NCA ni ufugaji. Kisayansi yamekuwapo matokeo ya utafiti yasiyo na shaka kuwa mwingiliano wa wanyamapori na mifugo kunaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa, ama ya kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa mifugo, au kutoka kwa mifugo kwenda kwa wanyamapori.

Kwa kulitambua hilo, NCAA imekuwa ikifanya kila linalowezekana kusaidia kwenye uboreshaji na tiba ya mifugo ya wenyeji. Mwaka 2017/2018 kazi hiyo imefanywa kwa mafanikio makubwa kwa kutenda haya:

Mosi, Sh milioni 371 zilitumika kununulia chanjo ya mifugo na dawa. Pili, Sh milioni 279 zilitumika kwa ajili ya sensa ya watu na mifugo pamoja na kuweka alama za mifugo.

Tatu, kwa kutambua kuwa ufugaji wa kisasa una tija zaidi, NCAA ilitumia Sh milioni 108 kundaa mkakati wa kuboresha mifugo ya wenyeji.

Ili uhifadhi uwe endelevu, NCAA inatambua na kuthamini upelekaji wa huduma na miradi mbalimbali kwa jamii. Katika mwaka 2017/2018 Sh bilioni 2.5 zilipelekwa kugharimia shughuli za Baraza la Wafugaji ambalo lipo kisheria.

Sh milioni 50 zilitumilka kuchangia umaliziaji wa ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Msingi Endulen; Sh milioni 120 zilitumika kutekeleza miradi ya huduma za jamii kwa vijiji vinavyoizunguka Hifadhi ya Ngorongoro na Sh milioni 550 zilitumika kupeleka maji katika makazi mapya Jema Oldonyosambu.

Kiasi kingine cha fedha kimetumika katika kipindi hicho kusaidia vikundi vya kina mama, pia kuanzisha vyama vya ushirika 12 ndani ya Tarafa ya Ngorongoro.

Kuna miradi mingine mingi yenye tija iliyogharimiwa na NCAA ili kulifanya eneo la hifadhi kuwa salama zaidi.

Baadhi ya miradi hiyo ni ya kuboresha usalama wa eneo ambapo Sh milioni 95 zilitumika kununua na kufunga mfumo wa CCTV camera; na Sh milioni 527 zilitumika katika mradi wa ununuzi wa mawasiliano ya ulinzi wa pori na vifaa vya usalama wa eneo la hifadhi.

Kwa muda mrefu lango la Nasera Rock lilikuwa upenyo wa wageni, hivyo kuikosesha NCAA mapato mengi. Kwa sababu hiyo, Sh milioni 293 hivi zmetumika katika ujenzi wa lango jipya la eneo hilo, zikiwa ni jitihada za kudhibiti uingiaji usio rasmi wa wageni ndani ya eneo la hifadhi. Sh milioni 493 zilitumika kwenye ujenzi wa nyumba za askari katika kituo cha Lemala ili kuwawezesha kupata sehemu nzuri ya kuishi, hivyo kuwafanya waweze kutekeleza majukumu yao kwa uzuri zaidi.

Magari ni vitendea kazi muhimu katika suala zima la uhifadhi. Katika kuimarisha usalama wa eneo, ufuatiliaji wa miradi na usimamizi wa eneo kwa ujumla, Mamlaka ilitekeleza mradi huu kwa ununuzi wa magari mbalimbali yenye thamani ya Sh bilioni 1.974.

Mradi  mwingine uliotekelezwa ni wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mali za shirika, ambapo Sh milioni 106 zilitumika.

Jengo la Kitega Uchumi la Ngorongoro Tourism Centre linatajwa kuwa jengo bora katika Jiji na Mkoa wa Arusha. Ni mradi uliobuniwa ili kusaidia kukuza sekta ya utalii kwa kuwaweka pamoja wadau wote wa sekta hii. Kwa kulitambua hilo, mwaka 2017/2018 Sh bilioni 2.107 zilitumika kutekeleza huo ujenzi ambao kwa sasa umekamilika.

Aidha, kiasi kingine cha Sh milioni 968 kilitumika katika mradi wa ukarabati wa kawaida wa barabara ya Loduare hadi Golini; na kiasi kingine cha Sh bilioni 1.025 kilielekezwa kwenye ujenzi wa eneo la mapokezi la Laitole. Hapo ndipo kwenye nyayo za binadamu wa kale. Eneo hilo pamoja na Olduvai Gorge limekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato ya NCAA.

Please follow and like us:
Pin Share