Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Elifas Bisanda, amezungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu historia, mafanikio, changamoto na hatima ya chuo hicho. Sehemu iliyopita alieleza namna OUT ilivyosambaa nchini kote. Sehemu hii anaelezea kuhusu mtandao huo na hatari inayokikabili chuo kutokana na mfumo wa usaili anaosema unaua maana halisi ya ‘Chuo Kikuu Huria’. Mwandishi MANYERERE JACKTON, aliyezungumza naye, analeta mwendelezo wa mahojiano hayo. Endelea…

Zanzibar tulipewa jengo la Chuo cha Ualimu cha Lumumba, lile jengo sasa liko chini ya mamlaka ya State University of Zanzibar (SUZA). Tukalikarabati, tukaweka maabara za kompyuta, madarasa na ofisi za walimu. Tulipewa kwa matumizi ya muda mrefu. Tuna eneo jingine tumenunua kule Zanzibar, lakini tunataka watu wenyewe wa Zanzibar wachange pesa tujenge kwa sababu kile chuo ni cha wananchi.

Manyara is very interesting. Mkuu wa Mkoa aliyekuwapo wakati ule – Mheshimiwa Shekifu [Henry Shekifu], alitukabidhi eneo kwenye jengo la mkoa. Jengo lilikuwa na eneo la maktaba, akatukabidhi lote na tukajenga maabara mle ndani. Mpaka sasa tuko kwenye jengo la mkoa. Tunachangia kidogo. Tuna kiwanja Manyara tunataka kufanya harambee tujenge jengo letu wenyewe.

Arusha tunatumia jengo la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Tunakodi ingawa wanafunzi wamejenga jengo nje kama turubai kwa ajili ya mitihani. Kilimanjaro tulinunua eneo la Kampuni iliyoitwa PECO. Walituuzia yadi yenye ekari 7 kwa hiyo tumefanya ukarabati tukapata madarasa na kuna eneo jingine kuna nyumba. Kuna mgongano nao, tutaongea na watu wa TBA kuona namna gani tutamaliza.

Pemba tunakodisha. Maeneo mengine tunayokodisha ni Tabora, Kigoma, Lindi, Songwe, Geita, Simiyu. Simiyu walitupatia jengo la halmashauri, lakini tunalikodisha kwa muda mfupi. Baada ya muda tunatakiwa tujenge jengo letu. Tumekwisha kupewa ekari 2. Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Anthony Mtaka, ametuambia tupeleke Sh milioni 50 yeye atafanya harambee. Tunazitafuta, tukishakusanya ada tutapeleka milioni 50.

Kwa Dar es Salaam, hapo Kinondoni tunakodi. Ndiyo the most expensive. Hii shule ilikuwa ya Biafra, mwenye shule alivyofunga ndiyo akatukodisha. Tunalipa Sh milioni 126 kwa mwaka. Ada inapanda kwa asilimia 5 kila baada ya miaka mitano. Kwa hiyo ndiyo sehemu kubwa inatuumiza kichwa kwa sababu Sh milioni 126 kwa mwaka si hela ndogo, ingawa Mwanza tulikuwa tunalipa Sh milioni 200. Katika mbinu zetu za kujikwamua ni kupata majengo yetu wenyewe.

Idadi ya wanafunzi

Mapato yetu yameshuka. Idadi ya wanafunzi imeteremka. Imeteremka kwa sababu, kwanza ushindani upo mkubwa. Wakati Chuo Kikuu Huria kinaanzishwa kulikuwa na vyuo vikuu viwili tu. Kulikuwa na SUA na UDSM, ndiyo ikaanzishwa Open University. Sasa hivi vyuo vipo 54, kwa hiyo kuna ushindani mkubwa sana katika soko la vyuo.

Pili, sifa za kuingia zimebana. Zamani kozi ya Foundation ilikuwa inaingiza wanafunzi wengi. Ilikuwa inatoa watu wenye vyeti. Sasa hivi lazima uwe na Form IV na diploma au Form IV na Form VI.  Kwa hiyo wigo wa cachment umeshuka hivyo inabidi au tupanue programu za diploma ziwe nyingi ili tuwapate watu wenye diploma ndiyo baadaye waje kwenye digrii.

Katika vyuo vingine huria duniani, kwa mfano Uingereza huwa hakuna usaili. It is open. Yaani wewe hata ukitoka sokoni unasema unataka kusoma digrii, unaingia. Ukifeli unaacha. Ulisoma HGL, sasa unataka kusoma udaktari unaingia tu. Wewe mwenyewe baada ya semester moja utaamua kama unaendelea au unaacha.  Hiyo ndiyo maana halisi ya ‘open’.  Sisi tuko regulated na TCU na wanataka tuendane na vigezo kama vya vyuo vingine, kwa sababu sifa anazopata huyu, akipata ajira ni sawa na yule mwingine, kwa hiyo tunataka sifa za kuingia zote ziwe sawa. Ile dhana ya ‘uhuria’ haipo tena.

Mfano, wakati wa kuondoa vyeti feki, kuna mtu ambaye alifaulu Form IV, lakini Form VI akaghushi cheti. Akaingia chuo kikuu, akasoma digrii ya kwanza akafaulu. Akasoma Masters akafaulu. Akasoma Doctorate akawa na PhD. Leo hii ameondolewa kwa sababu ya cheti cha Form VI. Sasa unajiuliza, tatizo liko wapi? Tatizo lipo kwenye mfumo wa elimu ya chuo kikuu au elimu ya sekondari, kama mtu ameingia chuo kikuu kwa sifa za Form IV na bado akafaulu ina maana Form VI ni irrelevant, kwa maana ambaye hata hakusoma Form VI ameweza kutoka amesoma chuo kikuu na amefaulu.

Inakuonyesha kwamba mfumo wetu wa elimu una shida. Ama useme na elimu ya chuo kikuu nayo ina shida, maana hata kilaza akiingia atafaulu tu, atapata digrii, atapata Masters, atapata PhD.

Kwa hiyo hilo ndilo tatizo tulilonalo. Sasa tunaambiwa wote lazima waingie na vigezo sawa, kwa hiyo wote hawa wa Open University wanaingia na vigezo sawa na wengine na matokeo yake ni kwamba sisi tuko kwenye receiving end. Kama hali hii ikiendelea kwa miaka mingine minne, mitano tutafunga chuo kwa sababu we are no longer open university – sisi siyo tena chuo kikuu huria. Ule uhuria haupo tena. Kwa nini tuendelee kuwa chuo kikuu huria wakati uhuria haupo?

Zamani tulikuwa tunaruhusiwa kudahili wanafunzi muda wowote – ni ‘open’, akiingia Oktoba, akiingia Machi aingie tu asome, lakini sasa hivi tunaambiwa lazima tuingize wanafunzi wakati mmoja na vyuo vingine, na sisi hatuwezi kushindana nao kwa sababu tunaowalenga ni waliomaliza Form VI na waliomaliza diploma. Wote wanapomaliza Juni wanataka Septemba waombe waingie vyuoni. Sisi wanaokuja labda ni wale waliokosa nafasi kule sasa waje. Kama tunafunga usaili wakati mmoja ina maana hatuwapati. Wanabaki wanang’aang’aa macho hawajui waende wapi na huku system ya admission imekwisha kufungwa.

Open University haiwezi ku-oparate namna hiyo. Ni open admission – maana yake ni kwamba wanafunzi wanaingia muda wowote na kutoka muda wowote, na kwamba wanaingia bila kuwauliza qualification zao. Ndivyo vyuo vikuu vyote [huria] vinavyofanya. Kwa mfano Chuo Kikuu cha Malaysia wana system nzuri sana. Wao wakiku – admit lazima ufanye Foundation courses – zile ndizo zinaamua kama wewe upo kwenye level gani. Nilishangaa kuambiwa kwamba kuna watu wanaoingia hawana digrii ya kwanza, lakini wakifanya ile Foundation course wanaonekana wanaweza kufanya Masters – wanaingia moja kwa moja kufanya Masters.

Ile Foundation course yao wana kitu wanaita Recognition of Prior Learning (RPL). Huwezi kufanya mtihani wa RPL kabla ya kufanya Foundation courses. Zile ndizo zinazoamua uwezo wako. Wanakupatia mafunzo kidogo halafu wanakupima, na wakishakupima wanasema wewe kasome Masters, wewe kasome diploma, wewe kasome certificate maana bado uko chini sana, wewe nenda kasome digrii. PhD huwa hawatoi. Sisi tulipendekeza mfumo kama huo. Hauwezi kutoa RPL bila Foundation course. Foundation course si ya kumfanya mtu aende akasome digrii, ukweli ni kuwa inaweza kumsaidia mtu akasome certificate, akasome diploma, digrii hata Masters.

Shida kubwa iliyopo kwenye kudumu kwa chuo hiki ni jinsi udhibiti wa mfumo wa ubora hauelewi dhana ya elimu huria. NACTE, TCU hawaelewi maana ya elimu huria ni kitu gani. Wao wanaiangalia katika jicho lile lile la face to face university.

Profesa Kuhanga [mwasisi wa Open University] ana machapisho mengi sana. Baadhi ya waliopo hawana uelewa wa elimu huria. Hata wakati sheria inapitishwa bungeni mwaka 1992…hansard tunayo. [Namna wabunge walivyojadili na kupitisha sheria ya chuo kikuu huria]. Waliopo wanapaswa wajue chuo kilianzishwa kwa madhumuni gani, vinginevyo wanakiua bila kujua. Wanatoa matamko ambayo yanaweza kukiua chuo.

By Jamhuri