Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali nchini kutekeleza majukumu kwa kuzingatia weledi, usawa na uadilifu ili kuhakikisha wananchi wanapata haki bila kujali hali zao za kiuchumi.

Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 21, 2024) wakati akifugua mkutano wa Mkuu wa Chama cha Mawakili wa serikali Tanzania, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi wote, imeendelea kuchukua hatua kadhaa zikiwemo ujenzi wa miundombinu, uendelezaji wa rasilimali watu, maboresho ya mifumo na sheria mahsusi.

Waziri Majaliwa pia amesema Serikali imetekeleza mpango wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama Jijini Dodoma, Vituo sita Jumuishi vya Utoaji Haki, Mahakama za Wilaya 27 pamoja na mahakama za mwanzo 14.

Ameeleza serikali inaendelea na ujenzi wa vituo jumuishi sita vya Geita, Simiyu, Njombe, Katavi, Songea na Songwe.

Amesema kutokana na maono na msukumo wa Rais Dk. Samia katika kipindi cha miaka mitatu kwenye tasnia ya sheria na utoaji wa haki,Serikali imewezesha Wananchi 415,280 na mahabusu 7,166 kufikiwa na huduma za kisheria bila gharama kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutoka Mitaa/Vijiji 1,348 kwenye mikoa sita nchini.

“Huduma ya msaada wa kisheria inayoendelea kutolewa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufahamu wa wananchi kuhusu masuala ya kisheria na kusaidia utatuzi wa migogoro na utoaji wa huduma za kisheria katika masuala mbalimbali,”amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dk. Pindi Chana amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk.Samia Tanzania imekuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya Kimataifa.

Amesema sababu ya Tanzania kuchaguliwa ni kutokana na uongozi bora chini ya Rais Dk.Samia.

Naye, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Juma ameeleza kuwa wataendelea kusimamia na kuhakikisha sheria zinatumika vyema katika utoaji wa haki kwa wananchi na kuyafikia malengo yaliyotajwa katika dira ya Maendeleo ya Taifa 2025

By Jamhuri